Jumatatu, 12 Oktoba 2026

JAJI MKUU WA UGANDA AFANYA ZIARA YA KIKAZI MAKAO MAKUU YA MAHAKAMA

Na HABIBA MBARUKU-Mahakama Dodoma

Jaji Mkuu wa Uganda, Mhe. Dkt. Flavian Zeija, pamoja na ujumbe wake leo tarehe 12 Oktoba, 2026 ametembelea Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma na kujionea hatua kubwa zilizopigwa katika utoaji haki nchini, ikiwemo matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), ujenzi wa miundombinu ya kisasa inayorahisisha utendaji wa Mahakama huku ikitekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo, 2050.

Alipowasili Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania, Mhe. Dkt. Zeija alipokelewa na Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju akiwa pamoja na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Dkt. John Jingu pamoja na Wajumbe wa Menejimenti ya Mahakama ya Tanzania.

Katika ziara hiyo, ugeni huo ulipata fursa ya kutembelea ukumbi mpya wa kisasa wa Mahakama ya Tanzania, pamoja na Chumba Maalum cha Usimamizi wa Taarifa za Mahakama (Judiciary Situation Room) kinachotumika kufuatilia na kuratibu shughuli za Mahakama nchi nzima.

Aidha, ugeni huo ulipata nafasi ya kufanya majadiliano na kubadilishana uzoefu juu ya matumizi ya TEHAMA, pamoja na kufahamu mifumo mbalimbali inayotumiwa na Mahakama katika kufanikisha upatikanaji wa haki mapema ipasavyo ambapo Mkurugenzi wa Mipango na Uratibu wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Erasmus Uisso, aliwasilisha mada iliyoeleza muundo, dira, na maboresho mbalimbali yanayoendelea kutekelezwa na Mahakama ya Tanzania.

Akiwasilisha Muundo wa Mahakama, Bw. Uisso amebainisha kuwa, mfumo wa Mahakama nchini umejengwa katika ngazi kuu nne kuanzia Mahakama za Mwanzo, Mahakama za Wilaya na Hakimu Mkazi, Mahakama Kuu yenye divisheni maalum ambazo ni Divisheni ya Kazi, Ardhi, Biashara, Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, hadi Mahakama ya Rufani ambayo ndiyo ngazi ya juu kabisa ya Mahakama.

Bw. Uisso ameeleza kuwa, Mahakama inatekeleza azma yake ya kutoa haki sawa kwa wote mapema ipasavyo kupitia teknolojia, ikiongozwa maadili ya msingi, ambayo ni uadilifu, kutokuwa na upendeleo, uwajibikaji, uwazi, na utaalamu kupitia uadilifu, uwazi, na uwajibikaji, huku kipaumbele kikubwa kikiwa ni kuwaweka wananchi mbele (citizen-centric) ili kujenga imani ya umma.

“Tunatazamia kutoa haki kwa wote kupitia teknolojia, na mwelekeo wetu uko kwa wananchi, yaani unaoweka wananchi mbele (citizen-centric). Hilo ndilo lengo letu, kuhakikisha kwamba wananchi wanapata kile wanachokitazamia kutoka kwetu, tunajikita sana katika kujenga imani ya umma, kwa sababu kama huna imani ya umma, basi watu hawawezi kutumia au kupata kile wanachokitazamia kutoka kwetu,” ameeleza Bw. Uisso.

Akizungumza kuhusu mageuzi ya Mahakama, Bw. Uisso ameeleza kuwa mageuzi ya Mahakama yalianza takribani miaka 10 iliyopita, yaani mwaka 2015 ambapo kuanzia mwaka huo Mahakama imemaliza mpango wa mageuzi ya sekta ya sheria, uliokuwa ukijumuisha Taasisi zote za sekta ya sheria kwa kuongozwa na Wizara, jambo ambalo limeonesha mafanikio kwa Mahakama.

Ameeleza kuwa, eneo lililopewa kipaumbele katika mageuzi ni mabadiliko ya kidigitali ambapo Mahakama ilihakikisha inafanya shughuli za ke kidigitali kwa kujenga mifumo kama vile mfumo wa usimamizi wa mashauri, Mahakama Mtandao Pamoja na mfumo wa kufuatilia takwimu za kiutendaji za Mahakama.

Ameongeza kuwa, eneo lingine lililopewa kipaumbele ni mageuzi ya kisheria na kiutaratibu, ambapo kanuni na taratibu zilianza kurahisishwa pia uanzishaji wa kanuni za ufunguzi wa mashauri kwa njia ya mtandao kanuni za uendeshaji wa mashauri kwa mtandao ili kuwezesha usikilizaji wa mashauri kwa njia ya mtandao.

Aidha, kipaumbele cha miundombinu ya Mahakama ambapo Mahakama imefanikiwa kujenga Vituo Jumuishi vya Utoaji Haki, Mahakama za Hakimu Mkazi, Pamoja na ukarabati wa majengo ya Mahakaman nchi nzima, sambamba na kuimarisha rasilimali watu kwa kuanzisha mafunzo ili kukuza ujuzi na kuboresha mazingira ya kazi kwa kutoa vifaa vya kufanyia kazi, kuwezesha usafiri kwa wafanyakazi.

Sambamba na hayo, Bw. Uisso ameyataja mafanikio yaliyofikiwa kuwa ni ujenzi wa Vituo Jumuishi vya Utoaji Haki 15 nchi nzima, ambavyo vinakusanya huduma zinazopatikana katika ngazi zote za Mahakama chini ya pamoja.

Ameyataja Mafanikio mengine kuwa, ni Matumizi ya TEHAMA yanayohusisha matumizi ya Mfumo wa Kielektroniki wa usimamizi wa mashauri (e-case management), usikilizaji wa mashauri kwa njia ya mtandao (virtual hearings), na mfumo wa kurecord kumbukumbu kidijiti ili kuongeza uwazi na ufanisi pamoja na kujenga uwezo wa rasilimali watu kupitia mafunzo endelevu kwa watumishi ili kuendana na mabadiliko ya kiteknolojia.

Bw. Uisso amefafanua kuwa, katika miundombinu ya TEHAMA kuna intaneti ya mkongo wa baharini yenye kasi ya gigabiti 1.28 kwa sekunde pia mtandao wa nyuzi za fiber (fiber cable) ambao sasa umefika zaidi ya kilomita 7,000 na unafika hadi kwenye makao makuu ya kila wilaya kwa sasa, kwa hiyo inapatikana vizuri, lakini pia inaunganisha baadhi ya nchi jirani ikiwemo Uganda.

Akihitimisha wasilisho lake, Bw. Uisso amesema kuwa katika muelekeo wa Dira 2050, Mahakama ina mpango wa maendeleo wa miaka mitano, mfumo wa kimakakati wa Uchumi wa kidigitali ambayo yatalisha sheria za kitaifa za TEHAMA ambapo ipo Sheria ya Serikali ya Mtandao , Sheria ya Miamala ya Kielektroniki, pamoja na sheria nyingine zinazosimamia sekta hiyo, ambazo zitaielekeza Mahakama, kufaidika na mipango hiyo, hasa mpango mkakati, pamoja na sera ya TEHAMA huku akiongeza kuwa maboresho haya ya Mahakama yanaingiliana kwa karibu na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, inayolenga kujenga uchumi imara na jamii yenye haki, amani na utawala bora.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya TEHAMA-Mahakama ya Tanzania, Bw. Kalege Enock, ameelezea mifumo mbalimbali ya Mahakama na namna inavyofanya kazi kieletroniki ikiwa ni pamoja na mifumo ya e-Case Management, Virtual Court pamoja na namna Chumba Maalum cha Usimamizi wa Shughuli za Mahakama (Judicial Situation Room) kinavyofanya kazi kama Data Hub.

Katika ziara hiyo ambayo Mhe. Dkt. Flavian Zeija, ameambatana na baadhi ya Viongozi wa Mahakama Uganda ambao ni pamoja na Maureen Kasande, Ssinabulya Joseph pamoja na Oryema Brian.

Ziara hiyo imethibitisha ushirikiano madhubuti wa kisheria na kimahakama kati ya nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, huku Uganda na Tanzania zikishirikiana kubadilishana uzoefu katika uboreshaji wa mifumo ya utoaji haki kwa wananchi.

Jaji Mkuu wa Uganda, Mhe. Dkt. Flavian Zeija (kulia) pamoja na ujumbe wake leo tarehe 12 Oktoba, 2026 ametembelea Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma na kupokelewa na mwenyeji wake, Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju pamoja na Viongozi Waandamizi wa Mahakama.


Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju (kulia) akiwa katika picha ya pamoja na Jaji Mkuu wa Uganda, Mhe. Dkt. Flavian Zeija.


Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju (aliyesimama mbele kushoto) akimuonesha Jaji Mkuu wa Uganda, Mhe. Dkt. Flavian Zeija picha za Majaji Wakuu waliopita hadi wa sasa. 

Jaji Mkuu wa Uganda, Mhe. Dkt. Flavian Zeija akisaini Kitabu cha wageni mara baada ya kuwasili ofisini kwa Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju (hayupo katika picha). 

Jaji Mkuu wa Uganda, Mhe. Dkt. Flavian Zeija, (kulia kochi mbele) akiwa anateta jambo mara baada ya kuwasili ofisini kwa Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju (kushoto) kwa ziara ya kikazi. 

Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju (kulia) akiwa katika picha ya pamoja na Jaji Mkuu wa Uganda, Mhe. Dkt. Flavian Zeija mara baada ya kuwasili ofisini kwake jijini Dodoma leo tarehe 12 Oktoba 2026.

Mkurugenzi wa TEHAMA-Mahakama ya Tanzania, Bw. Kalege Enock akitoa maelezo kuhusu (Judiciary Situation Room).

Majadiliano yakiendelea.

Jaji Mkuu wa Uganda, Mhe. Dkt. Flavian Zeija, pamoja na ujumbe wake wakiwa ndani ya Ukumbi wa Mikutano wa Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju (kulia) ili kufuatilia mawasilisho ya taratibu za ujenzi wa mifumo ya TEHAMA  na Miundombinu.

Mkurugenzi wa Mipango na Uratibu wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Erasmus Uisso (kulia), aliwasilisha mada iliyoeleza muundo, dira na maboresho mbalimbali yanayoendelea kutekelezwa na Mahakama ya Tanzania. 


Mkurugenzi wa Mipango na Uratibu wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Erasmus Uisso (kulia), aliwasilisha mada iliyoeleza muundo, dira na maboresho mbalimbali yanayoendelea kutekelezwa na Mahakama ya Tanzania. 

Jaji Mkuu wa Uganda, Mhe. Dkt. Flavian Zeija akifuatilia wasilisho kutoka kwa Mkurugenzi wa TEHAMA Mahakama ya Tanzania, Bw. Kalege Enock (hayupo katika picha).

Jaji Mkuu wa Uganda, Mhe. Dkt. Flavian Zeija (wa pili kushoto), pamoja na ujumbe wake wamepata pia fursa ya kutembelea Ujenzi wa Nyumba ya Makazi ya Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju. 

Jaji Mkuu wa Uganda, Mhe. Dkt. Flavian Zeija, pamoja na ujumbe wake wamepata pia fursa ya kutembelea Ujenzi wa nyumba ya Makazi ya Jaji Mkuu Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju. 

Jaji Mkuu wa Uganda, Mhe. Dkt. Flavian Zeija pamoja na ujumbe wake wamepata pia fursa ya kutembelea Ujenzi wa nyumba ya Makazi ya Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju. 

(Picha na MARY GWERA & INNOCENT KANSHA, Mahakama-Dodoma)



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni