Jumanne, 13 Oktoba 2026

MAHAKAMA KUU NJOMBE, NMB WASHIRIKIANA KUIMARISHA HUDUMA KWA WATEJA

  • Watumishi   wapatiwa mafunzo ya kuboresha utoaji wa huduma kwa wateja na namna bora ya kushughulikia malalamiko

 Na ABDALLAH SALUM, Mahakama-Njombe

Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Njombe kwa kushirikiana na Benki ya NMB-Tawi la Njombe, imeendesha mafunzo maalum kwa Watumishi wa Mahakama kuhusu utoaji wa huduma bora kwa wateja na namna ya kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazojitokeza wakati wa kuwahudumia wateja.

Mafunzo hayo yalifanyika hivi karibuni ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Wateja, yakiwa na lengo la kuongeza uelewa, kubadilishana uzoefu na kuwajengea watumishi uwezo wa kutoa huduma bora mapema ipasavyo na kwa weledi.

Mratibu wa mafunzo hayo, Hakimu Mkazi na Msaidizi wa Sheria wa Jaji Mfawidhi wa Masjala Ndogo ya Njombe, Mhe. Elisha Mwasomola aliwakaribisha watumishi wote waliohudhuria na kuwatambulisha Maofisa kutoka Benki ya NMB waliokuwa wamealikwa kwa ajili ya kutoa mafunzo hayo.

Mafunzo hayo yalihusisha watumishi wa Mahakama Njombe pamoja na wengine kutoka Wilaya mbalimbali walioshiriki kwa njia ya mtandao, hatua iliyowezesha watumishi wengi zaidi kunufaika na maarifa yaliyotolewa.

Akitoa neno la utangulizi, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Njombe, Mhe. Joseph Luambano alisisitiza juu ya umuhimu wa watumishi kutoa huduma bora kwa wateja wote wanaofika Mahakamani kupata huduma mbalimbali.

Alieleza kuwa, huduma kwa wateja ni sehemu muhimu ya utekelezaji wa majukumu ya Mahakama na kwamba kila mteja anapaswa kuhudumiwa kwa kiwango cha juu ili kuhakikisha anaridhika na huduma anayoipata.

“Tunawahudumia wateja mbalimbali wanaohitaji huduma za Mahakama. Hivyo, tunapaswa kuhakikisha tunatoa huduma kwa kiwango cha juu ili wateja wetu waridhike. Mahakama inaelekezwa kutoa huduma bora, na msingi wa maelekezo hayo unatokana na mkataba wa huduma tuliojiwekea na wateja wetu,” alisema Mhe. Luambano.

Kwa upande wake, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Njombe, Mhe. Victoria Nongwa aliyekuwa mgeni mzungumzaji katika mafunzo hayo, aliwakaribisha Wawezeshaji wa mafunzo hayo na kusisitiza kwamba, mafunzo hayo ni fursa muhimu ya kujifunza na kubadilishana uzoefu katika kuboresha huduma kwa wateja.

 Aidha, alibainisha kuwa, kitengo cha huduma kwa wateja ni kielelezo cha taswira ya taasisi, kwani namna mteja anavyopokelewa inaweza kuathiri mtazamo wake kuhusu ubora wa huduma zinazotolewa na taasisi husika.

“Ningependa wote tutambue kuwa, huduma kwa mteja ni zaidi ya kujibu maswali badala yake, inahusisha pia namna maswali hayo yanavyojibiwa kwani, wakati mwingine mteja haulizi swali ili apate jibu sahihi pekee, bali anataka kuona shida yake imepokelewa kwa uzito upi na ni kwa namna gani yeye amejaliwa na mtoa huduma. Kwa sababu hiyo, kila mmoja wetu akitekeleza wajibu wake wa kutoa huduma bora kwa wateja, imani ya wananchi kwa Mahakama itazidi kuongezeka,” alisema Mhe. Nongwa.

Aidha, Mhe. Nongwa alieleza kwamba, huduma kwa wateja ni muhimu sana kwa kuwa inajenga imani ya wananchi (wateja) kwa taasisi, inapunguza malalamiko na kuimarisha ushirikiano baina ya taasisi na wadau wake.

Akizungumza kwa niaba ya Benki ya NMB, Meneja wa Huduma kwa Wateja wa NMB, Tawi la Njombe, Bi. Regina Kavishe aliishukuru Mahakama kwa kuwapa nafasi ya kushiriki katika mafunzo hayo na kueleza kuwa, huduma kwa wateja ni jukumu linalohitaji kujituma, uvumilivu na moyo wa kujali mahitaji ya wengine. Kwa sababu hiyo, alieleza, watumishi wanapaswa kutumia Wiki ya Huduma kwa Wateja kutafakari namna wanavyotekeleza majukumu yao na kutafuta njia bora za kuongeza thamani katika huduma wanazozitoa kila siku.

Bi. Kavishe alifafanua kuwa, huduma ina sifa ya kutokushikika, kutokutenganishika na mtoa huduma na kutohifadhika kwa ajili ya matumizi ya baadaye. Aidha, alisisitiza kwamba, ili kutoa huduma bora mtumishi anapaswa kumkaribisha mteja vizuri, kumsikiliza kwa makini hadi amalize kueleza mahitaji yake, kumuelewa, kutafakari hatua zinazofaa kuchukuliwa, kutekeleza majukumu kwa wakati na kutoa mrejesho kwa mteja.

Naye Mshauri wa Ubora wa Huduma kwa Wateja wa NMB, Tawi la Njombe, Bw. Erick Luhwago, alieleza kuwa huduma bora kwa mteja ni kumhudumia mtu kwa namna ambayo mtumishi mwenyewe angependa kuhudumiwa.

Bw. Luhwago alielezea kwa kina hatua zinazopaswa kufuatwa katika kushughulikia malalamiko ya wateja. Alizitaja hatua hizo kuwa ni pamoja na kupokea malalamiko, kumsikiliza mlalamikaji kwa makini na kumpa muda wa kueleza tatizo lake, kuandika malalamiko, kufanya tathmini, kuwasilisha malalamiko katika Idara/kitengo husika, kufanya uchunguzi, kutafuta suluhisho na kumpa mteja mrejesho kuhusu hatua zilizochukuliwa.

Bw, Luhwago alisisitiza kuwa, mchakato wa kushughulikia malalamiko unapaswa kuzingatia misingi ya uwazi, uharaka, haki na usiri ili kuhakikisha kila mteja anapata nafasi ya kusikilizwa na kushughulikiwa kwa usawa.

Akizungumzia namna ya kuwahudumia wateja wagumu (difficult customers), Bw. Luhwago alieleza kuwa, watumishi wanapaswa kuwasikiliza wateja hao hadi mwisho, kuwatuliza wanapokuwa na hasira, kuuliza maswali ya ufafanuzi, kufanya uchunguzi wa kina, kutafuta suluhisho linalofaa na kuwashukuru kwa kueleza changamoto zao.

Zaidi ya hayo, Mshauri huyo wa Ubora wa Huduma kwa Wateja wa NMB alibainisha kuwa, baadhi ya wateja wanaweza kuhitaji mbinu maalum za mawasiliano kama vile, wanaopaza sauti, wanaolalamika mara kwa mara, walio na hasira, wanaodai kujua kila kitu, wanaotarajia kupata huduma bila malipo na wale wanaotumia lugha ya matusi au vitisho.

Akihitimisha mafunzo hayo, Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Njombe, Bw. Richard Mbambe, aliwashukuru Wawezeshaji kutoka Benki ya NMB pamoja na watumishi wote wa Mahakama kwa kushiriki kikamilifu katika mafunzo hayo na alieleza kuwa maarifa yaliyopatikana yatawasaidia watumishi kuboresha namna ya kuwapokea na kuwahudumia wateja wa aina mbalimbali kwa weledi, utulivu na ufanisi.

Aidha, aliwataka watumishi kuendeleza na kudumisha ushirikiano uliopo kati ya Mahakama na Benki ya NMB ili kuendelea kujifunza na kubadilishana uzoefu utakaosaidia kuboresha utoaji wa huduma kwa umma.

Mafunzo hayo ni sehemu ya jitihada za kuimarisha utamaduni wa utoaji wa huduma bora kwa wateja, huku yakisisitiza juu ya umuhimu wa kusikiliza mahitaji ya wateja, kushughulikia malalamiko kwa wakati na kuhakikisha kila mteja anahudumiwa kwa heshima, haki na weledi.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Njombe, Mhe. Victoria Nongwa akizungumza na watumishi wa Mahakama Kanda ya Njombe (hawapo katika picha) alipokuwa akifungua mafunzo ya Huduma kwa Wateja yaliyofanyika hivi karibuni.


Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Njombe, Mhe. Joseph Luambano (aliyesimama) akitoa pongezi kwa Maofisa wa Benki ya NMB kwa mafunzo ya waliyoyatoa. Aliyesimama kulia ni Mratibu wa Mafunzo, Mhe. Elisha Mwasomola, na aliyeketi wa kwanza (mwenye miwani) ni Mtendaji wa Mahakama Kuu Njombe. Wengine wanaoonekana ni sehemu ya washiriki wakifuatilia mafunzo hayo.

Meneja wa Huduma kwa Wateja wa NMB, Tawi la Njombe, Bi. Regina Kavishe (kulia) pamoja na Mshauri wa Ubora wa Huduma kwa Wateja wa NMB, Tawi la Njombe, Bw. Erick Luhwago, wakisikiliza na kujibu maswali yaliyokuwa yanaulizwa na watumishi wa Mahakama Njombe (hawapo katika picha).

Mshauri wa Ubora wa Huduma kwa Wateja wa Benki ya NMB-Tawi la Njombe, Bw. Erick Luhwago (kushoto) na Ofisa Mikopo ya Watumishi wa Umma wa Benki ya NMB, Tawi la Njombe, Bw. Noel Urio (kulia) wakifuatilia mada iliyokuwa ikiwasilishwa na Meneja wa Huduma kwa Wateja wa Benki ya NMB, Tawi la Njombe, Bi. Regina Kavishe (hayupo katika picha).

Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Njombe, Bw. Richard Mbambe akizungumza na Washiriki (hawapo katika picha) alipokuwa akifunga mafunzo hayo.

Baadhi ya Watumishi wa Mahakama Njombe, walioshiriki mafunzo ya Huduma kwa Wateja wakiwa ndani ya ukumbi uliotumika katika mafunzo hayo. Walioketi meza ya mbele ni Wawezeshaji wa mafunzo hayo kutoka Benki ya NMB, Tawi la Njombe. Na aliyesimama ni Mratibu wa Mafunzo hayo ambaye ni Hakimu Mkazi na Msaidizi wa Sheria wa Jaji, Mhe. Elisha Mwasomola.


Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Masjala ndogo ya Njombe, Mhe. Victoria Nongwa (wa pili kutoka kulia), Naibu Msajili Mahakama Kuu Njombe, Mhe. Joseph Luambano (aliyeketi kulia kwa Jaji Mfawidhi) pamoja na washiriki wengine wa Mafunzo ya Huduma kwa Mteja wakifuatilia mjadala wakati wa mafunzo hayo. Walioketi meza ya mbele ni Wawezeshaji wa mafunzo hayo kutoka Benki ya NMB, Tawi la Njombe.


(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni