Jumatano, 29 Mei 2024

CHAMA CHA WANAWAKE WAJANE CHAIMWAGIA SIFA MAHAKAMA KWA KUSIMAMIA HAKI

Na Evelina Odemba – Mahakama Morogoro

 

Kuelekea maadhimisho ya Siku ya Wajane Duniani tarehe 23 Juni, 2023, Chama cha Wanawake Wajane Tanzania wameipongeza Mahakama ya Tanzania kwa kusimamia haki hususani kwenye mashauri ya Mmrathi ambayo yanagusa maslahi ya wajane moja kwa moja.

 

Pongezi hizo zimetolewa na Katibu wa Chama hicho, Bi. Sabrina Tenganamba alipofika ofisini kwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Latifa Mansoor.

 

“Ni ukweli usiopingika kuwa Mahakama inafanya kazi kubwa katika kutenda haki na kusimamia mashauri, yakiwemo ya mirathi ambayo yanatugusa moja kwa moja sisi wajane na tunapata haki zetu stahiki,” alisema Bi. Sabrina.

 

Akizungumza baada ya kupokea pongezi hizo kwa niaba ya Mahakama ya Tanzania, Jaji Mfawidhi naye aliwapongeza wajane hao kwa kuanzisha Chama ambacho kinalikutanisha kundi hilo maalum.

 

Alisema kuwa licha ya kuadhimisha siku hiyo kitaifa wajane hao pia huonesha shughuli za ujasiliamali ambazo zinachangia kumuinua mwanamke mjane na kumuondoa kwenye kundi la utegemezi.

 

“Tumezipokea pongezi zenu nasi Mahakama tunapenda kuwaahidi wananchi kuwa tutaendelea kutekeleza wajibu wetu kwa kutoa maamuzi ya haki kwa kuzingatia misingi ya sheria,” Mhe. Mansoor alisema.

 

Alitumia fursa hiyo kuwahimiza wadawa wote wenye mashauri ya mirathi iliyokwisha kutolewa maamuzi wafike kwenye Mahakama husika ili kufunga mirathi hiyo.

 

Maadhimisho ya Siku ya Wajane Duniani yanategemewa kufanyika kitaifa mkoani hapa. Maadhimisho hayo yataanza kwa maonesho kuanzia tarehe 21 Juni, 2024 ambapo Mahakama Kanda ya Morogoro imepewa mwaliko wa kushiriki.

 


 Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Latifa Mansoor akizungumza na Viongozi wa Chama cha Wanawake Wajane Tanzania (hawapo pichani) wakati walipotembelea ofisini kwake.


 

Katibu wa Chama cha Wanawake Wajane Tanzania, Bi. Sabrina Tenganamba akizungumza wakati alipotembelea ofisini kwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Morogoro, Mhe. Latifa Mansoor.


 

Katibu wa Chama cha Wanawake Wajane Tanzania, Bi. Sabrina Tenganamba akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya waandaaji wa maadhimisho ya Siku ya Wajane Duniani wakati walipotembelea ofisini kwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Morogoro.


 

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Morogoro, Mhe. Mary Kallomo (kulia) akitoa utambulisho mfupi kwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Morogoro, Mhe. Latifa Mansoor wakati Viongozi wa Chama cha Wanawake Wajane Tanzania walipomtembelea ofisini kwake.


 

Baadhi ya Viongozi wa Chama cha Wanawake Wajane Tanzania wakiwa ndani ya Ofisi ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Latifa Mansoor (hayupo pichani).

(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam)

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni