Jumatano, 29 Mei 2024

KITUO CHA HUDUMA KWA MTEJA CHA MAHAKAMA CHATANGAZA HUDUMA ZAKE KIGOMA

Na Aidan Robert, Mahakama Kuu-Kigoma

Kituo cha Huduma kwa Mteja cha Mahakama ya Tanzania kimetoa elimu kwa wananchi waliojitokeza kupata huduma za Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma kuhusu namna ya kutoa malalamiko na mrejesho wa huduma wanazopatiwa wafikapo mahakamani.  

Akizungumza na wananchi wakati akitoa elimu kuhusu Kituo hicho, Hakimu Mkazi Mwandamizi na Mtaalamu wa Kuchakata na Kupitia Mrejesho wa Wananchi (Technical Supervisor-Call center), Mhe. Denice Mlashani alisema kuwa, Mahakama ilianzisha kituo hicho kwa lengo kubwa la kuiwezesha kupata mirejesho kutoka kwa wananchi na namna wanavyoridhika na huduma zitolewazo mahakamani.

Mhe. Mlashani alisema, hatua hiyo inaongeza uwazi juu ya huduma zitolewazo na Mahakama sambamba na kuleta uwajibikaji wa watumishi, ushirikishwaji wa Wadau na kujenga imani ya Wananchi juu ya huduma zinazotolewa na Mhimili wa Mahakama.

Wananchi hao wamefahamishwa kuwa malalamiko yanapokelewa kwa njia rahisi ya mawasiliano ya simu za mkononi ya 0752 500 400.

Aliongeza kuwa maboresho hayo ya uanzishwaji wa Kituo cha Huduma kwa Mteja yamelenga pia kuiwezesha Mahakama kutathimini na kutatua changamoto mbalimbali ikiwa ni kutekeleza Mpango Mkakati wa Mahakama kupitia nguzo ya tatu ya Kurudisha Imani ya wananchi juu ya huduma zinazotolewa katika Mahakama nchini Tanzania.

“Tunalenga pia kuhakikisha mwananchi anaridhika na huduma stahiki kwa wakati na yenye ubora uliokusudiwa na Mhimili wa Mahakama,” alisema Mhe.Mlashani.

Kwa upande wake, Kiongozi wa Timu ya Huduma kwa Mteja (Team Leader)-Mahakama ya Tanzania, Bi. Evetha Mboya aliwaeleza Wananchi hao kuwa, wanaweza kufikia Kituo hicho kwa njia ya Baruapepe ambazo ameweka bayana kwamba mwananchi anaweza kutumia, nazo ni pamoja na; maoni@judiciary.go.tz, ccamirathi@judiciary.go.tz na www.judiciary.go.tz.

“Mara baada ya kufungua Tovuti ya Mahakama (www.judiciary.go.tz) moja kwa moja kuna boksi la kutoa maoni juu ya huduma za Mahakama,” alieleza Bi. Evetha.

Aliongeza kwamba, Kituo kinapokea mrejesho kwa njia ya simu za mkononi, barua pepe na Tovuti ya Mahakama kwa saa 24, siku saba za wiki na wanapokea malalamiko, maoni, mapendekezo, maulizo na pongezi na kusisitiza kuwa, yote hayo hufanyika kwa njia ya namba za simu zilizowekwa bayana kwa wananchi ambazo ni 0752 500 400 na 0739 502 401.

“Simu hizo zipo hewani muda wote, tunapokea pia mirejesho kutoka kwa wananchi kwa njia ujumbe mfupi wa maneno (SMS) hivyo nawasihi wananchi kutumia huduma hii na kufaidi matunda ya Kituo hiki kwakuwa Mahakama ipo kiganjani mwenu ili kuokoa muda na gharama katika kuzifikia huduma za Mahakama,” amesisitiza Bi. Evetha.

Mkazi wa Kabanga Kasulu-Kigoma, Bw. Yamungu Nkamata mmoja kati ya wananchi walionufaika na elimu ya Kituo cha Huduma kwa Mteja aliipongeza Mahakama kwa maboresho makubwa yanayolenga kumpa Mwananchi nafuu ya kutatuliwa shida mbalimbali za kisheria na taratibu za huduma zaa Mahakama.

“Tunaishukuru na kuipongeza Mahakama kwa hatua hii maana mwanzo haikuwa hivyo, Viongozi wanastahili pongezi kubwa kwa hatua hii ya maboresho ya Mahakama,” alisema Bw. Nkamata.

Nao, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe. Gadiel Mariki na Mtendaji wa Mahakama Kigoma Bw. Filbert Matotay, wameongoza watumishi wa Kanda hiyo kupokea elimu ya utumiaji wa huduma za Kituo hicho ambapo Viongozi hao wametoa pongezi kwa Kituo hicho na kwa kwenda Kigoma kutoa elimu ya namna Kituo hicho kinavyofanya kazi.


Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe. Gadiel Mariki (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi wa Kituo cha Huduma kwa Mteja cha Mahakama waliotembelea Mahakama Kuu Kigoma. Wa kwanza kushoto ni Mtendaji Mahakama Kuu ya Kigoma, Bw. Filbert Matotay, wa kwanza kulia ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mkoa Kigoma, Mhe.Rose Kangwa,  wa pili kushoto ni Hakimu Mkazi Mwandamizi na Mtaalamu wa Kuchakata na Kupitia Mrejesho wa Wananchi (Technical Supervisor-Call center), Mhe. Denice Mlashani na wa pili kulia ni Kiongozi wa Timu ya Huduma kwa Mteja (Team Leader),  Bi. Evetha Mboya. Waliosimama nyuma ni sehemu ya Watumishi wa Mahakama hiyo.

Hakimu Mkazi Mwandamizi na Mtaalamu wa Kuchakata na Kupitia Mrejesho wa Wananchi (Technical Supervisor-Call center), Mhe. Denice Mlashani akitoa elimu juu ya utumiaji wa Kituo cha Huduma kwa Mteja cha Mahakama kwa wananchi waliofika Mahakama Kuu Kigoma kupata huduma jana tarehe 28 Mei, 2024.

Mkazi wa Kabanga Kasulu-Kigoma, Bw. Yamungu Nkamata mmoja kati ya wananchi walionufaika na elimu ya Kituo cha Huduma kwa Mteja  akiipongeza Mahakama ya Tanzania kwa maboresho ya uanzishaji wa Kituo cha Huduma kwa Mteja.

Afisa Utumishi na Kiongozi wa Timu ya Huduma kwa Mteja (Team Leader),  Bi. Evetha Mboya (aliyesimama) akitoa elimu jinsi Kituo cha Huduma kwa Mteja cha Mahakama kinavyofanya kazi. Kushoto ni Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Hakimu Mkazi Kigoma, Mhe. Rose Kangwa na katikati ni Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda  Kigoma, Bw. Filbert Matotay wakifuatilia kwa makini elimu inayotolewa na Bi. Evetha.

Hakimu Mkazi Mwandamizi na Mtaalamu wa Kuchakata na Kupitia Mrejesho wa Wananchi (Technical Supervisor-Call center), Mhe. Denice Mlashani akitoa elimu kuhusu matumizi ya Kituo cha Huduma kwa Mteja kwa watumishi wa Kanda ya Kigoma katika ukumbi wa Mahakama Kuu Kigoma.

Wananchi wakifuatilia kwa makini elimu ya Huduma kwa mteja iliyokuwa ikitolewa na Maafisa kutoka Kituo cha Huduma kwa Mteja (Call Centre) (hawapo katika picha).

(Habari hii imehaririwa na Mary Gwera, Mahakama-Dodoma)


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni