Ijumaa, 7 Juni 2024

JAJI MAGOIGA AHIMIZA HAKI KUPONYA MAJERAHA YA WAATHIRIKA WA UKATILI KINGONO

Na Evelina Odemba – Mahakama, Morogoro

 

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Morogoro Mhe. Stephen Magoiga amewataka watoa maamuzi mahakamani kuzingatia haki ili kuponya majeraha ya waathirika wa ukatili wa kingono badala ya kuwakumbusha machungu waliyopitia.

 

Mhe. Magoiga alitoa wito huo wakati akifunga mafunzo tarehe 5 Juni, 2024 yaliyoandaliwa na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto kwa kushirikiana na Ubalozi wa Ireland yaliyotolewa kwa Mahakimu 15 toka Kanda ya Morogoro.

 

Mafunzo hayo yaliyokuwa yanafanyika katika ukumbi wa mikutano kwenye Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Morogoro yalibeba dhima ya namna ya kutotonesha majeraha kwa waathirika wa ukatili wa kingono. 

 

Akihitimisha mafunzo hayo kwa niaba ya Jaji Mfawidhi, Mhe. Magoiga waliwataka washiriki hao kuishi elimu waliyopewa ili kuleta mabadiliko makubwa katika usikilizaji na utoaji maamuzi kwa watu waliopitia ukatili wa kingono. 

 

Alisema kuwa kwa kufanya hivyo wataongeza imani ya Mahakama kwa wananchi kuwa ni chombo salama cha kukimbilia na sio kuikimbia.

 

“Napenda wote tufahamu kuwa ndani ya vyumba vyetu vya Mahakama tuna uwezo wa kuponya au kudhuru, sisi tumechagua kuwa wakala wa uponyaji, tulio na ujuzi na mbinu bora zaidi ambazo tumezipata kupitia mafunzo haya,” alisema Mhe. Magoiga. 

 

Alitumia nafasi hiyo kuipongeza Mahakama ya Tanzania chini ya uongozi wa Jaji Mkuu, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma kwa kuruhusu mafunzo hayo yenye kuleta mabadiliko chanya kufanyika.

 

Aliwasihi washiriki kulipa fadhira kwa wananchi kwa kutoa haki kwa kuzingatia viwango vya juu vya maadili ya maafisa kama ambavyo mfumo wa Mahakama unavywajenga.

         

Naye Mratibu wa mafunzo hayo kutoka Kanda ya Morogoro, Mhe. Agnes Mgaya alitoa shukurani kwa wawezeshaji, Mhe. Fadhili Mbelwa, Mhe. Mary Kallomo na Afisa Ustawi, Bi. Judy Mbelwa kwa kazi nzuri waliyoifanya.

 


 Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Stephen Magoiga akizungumza wakati akifunga mafunzo ya namna ya kutokutonesha vidonda kwa watu walioathirika na ukatili wa kingono.


 

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Stephen Magoiga akikabidhi vyeti kwa washiriki wa mafunzo (juu na chini).




 

Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Fadhili Mbelwa ambaye pia alikuwa sehemu ya wawezeshaji wa mafunzo hayo akitoa neno la ufupi kabla ya mgeni rasmi kufunga mafunzo hayo.


 

Mratibu wa mafunzo kwa Kanda ya Morogoro, Mhe. Agnes Mgaya akitoa neno la shukurani kwa washiriki wote wa mafunzo hayo.



 Mhe. Josia Obasi akitoa neno la shukurani kwa niaba ya washiriki wa mafunzo hayo.



 Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Stephen Magoiga (aliyeketi katikati) kushoto ni Naibu Msaji, Mhe. Fadhili Mbelwa na kulia ni Mtendaji wa Mahakama, Bw. Ahmed Ng’eni wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya washiriki wa mafunzo (wote kutoka kanda ya Morogoro) (juu na chini).



Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Musoma

 

 

 

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni