Alhamisi, 6 Juni 2024

KAZI INAENDELEA SIMIYU

  • Ujenzi Kituo Jumuishi wapambamoto 

 

Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Simiyu.

 

Ujenzi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Mkoani Simiyu kitakachogharimu takribani Shilingi Bilioni 7.2 za Kitanzania umefikia asilimia 30 ambapo Mkandarasi ameahidi kukamilisha mradi huo kwa wakati katika kipindi walichokubaliana kwenye mkataba. 

 

Hayo yamebainishwa na Mtendaji wa Mahakama Mkoani Simiyu, Bw. Gasto Kanyairika alipokuwa anazungumza na Mkuu wa Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano cha Mahakama ya Tanzania, Ndg. Gerard Chami alipofanya ziara fupi hivi karibuni mkoani humo. 

 

"Mkandarasi alikabidhiwa eneo la ujenzi wa mradi tarehe 21 Novemba, 2023. Ujenzi wa Kituo ulianza tarehe 01 Desemba, 2023 na Mkandarasi anatakiwa kukabidhi jengo likiwa limekamilika ifikapo tarehe 31 Agosti, 2024. Tunaendelea kufuatilia kwa karibu ili kazi ikamilike kwa wakati," alisema. 

 

Alieleza kuwa kukamilika kwa ujenzi wa mradi huo kutawasaidia Wananchi wa Mkoa wa Simiyu mambo mengi, ikiwemo kusogeza huduma ya Mahakama Kuu karibu na Wananchi, kwani kwa sasa wanalazimika kusafiri umbali wa kilometa takribani 200 kufuata huduma hiyo Mahakama Kuu Shinyanga. 

 

Bw. Kanyairika alisema pia kuwa Kituo Jumuishi hicho kitapungiza gharama za Wananchi na kurahisisha wadaawa kukata rufaa katika ngazi ya Mahakama Kuu pale wanapokuwa hawajaridhishwa na uamuzi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi. 

 

Naye Mhandisi wa Mradi, Elirehema Shirima, akizungumza katika eneo la tukio alimweleza Mkuu wa Kitengo huyo kuwa wakati wa kutekeleza mradi huo wameajiri watalaam 16, vibarua 40, msimamizi mmoja, mtaalamu wa mahusiano ya jamii mmoja, muuguzi mmoja, mkadiliaji majenzi mmoja na mhasibu mmoja. 

 

"Tunaendelea vizuri na majukumu yetu. Kwa sasa tunamwaga zege ghorofa ya kwanza. Tumeshaandaa nguzo za kutoka ghorofa ya kwanza kwenda ya pili na tunajiandaa kumwaga zege. Tutajitahidi ili twende na kasi na ubora unaotakiwa ili tuweze kukamilisha kazi hii kwa mujibu wa Mkataba, " alisema. 

 

Akizungumzia jiografia ya eneo la Kimahakama, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Bariadi, Mhe. Caroline Kiliwa alieleza kuwa Mkoa wa Simiyu kwa sasa una Mahakama za Wilaya tano; Bariadi, Busega, Itilima, Maswa na Meatu na Mahakama za Mwanzo 36 zinazofanya kazi vema. 

 

Alisema kuwa hapo awali Mahakama ya Wilaya Bariadi ilikuwa inahudumia pia Wilaya za Busega na Itilima kabla ya kuanzishwa kwake katika Wilaya hizo husika. 

 

"Baada ya ujenzi wa Mahakama za Wilaya 18 kwa ufadhili wa Benki ya Dunia ambazo zilizinduliwa kwa pamoja tarehe 25 Novemba, 2022 na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma nasi tukapata Mahakama za Wilaya ya Busega na Itilima…

 

“…Hii imetupunguzia sana mzigo wa mashauri hapa kwetu. Tunamshukuru sana Jaji Mkuu kwa kutoa Tangazo la Serikali kuzipa mamlaka Mahakama hizi ili zijitegemee, mzigo wa mashauri kwetu umepungua sana," Mhe. Kiliwa alisema.


Ujenzi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Mkoani Simiyu unaendelea. Mwonekano wa jengo kwa nje ya uzio. Picha chini inaonesha bango la wahusika wote kwenye utekelezaji wa mradi huo.


Mwonekano wa jengo kwa mbele (juu na picha mbili chini).



Mhandisi wa Mradi, Elirehema Shirima (kushoto) akimwonyesha kitu Mkuu wa Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano cha Mahakama ya Tanzania, Ndg. Gerard Chami walipokuwa kwenye sehemu ya kuingilia kwenye jengo hilo.
Upande wa Kusini wa jengo hilo (juu na chini).


Upande wa Mashariki wa jengo hilo. Picha chini ni upande wa Kaskazini wa jengo.



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni