Jumatatu, 10 Juni 2024

KIKAO CHA MAHAKAMA KUU SINGIDA KUONDOSHA MASHAURI 10 YA JINAI

Na Eva Leshange- Mahakama, Singida

Jumla ya mashauri 10 ya jinai yanatarajiwa kuondoshwa katika kikao maalum ndani ya mwezi mmoja kuanzia leo tarehe 10 June, 2024 hadi tarehe 9 Julai, 2024 Mkoani Singida.

Hayo yamebainishwa na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma, Mhe. Sylivia Lushasi alipokuwa anawasilisha taarifa kwenye ufunguzi wa kikao hicho chini ya Jaji wa Mahakama Kuu kutoka Kanda hiyo, Mhe. Edwin Kakolaki.

“Mashauri tisa yanatoka Singida na shauri mmoja linatoka Iramba. Mkoa wa Singida una mashauri 21 ambayo yanasubiri kusikilizwa ambapo Mahakama ya Wilaya Singida kuna mashauri tisa, Iramba sita na Manyoni sita,” alisema.

Mhe. Lushasi amebainisha kuwa mashauri tajwa hayahusishi mashauri yanayosubiri washtakiwa kusomewa mashitaka kwa mara ya kwanza (plea taking).

Amewashukuru wadau kwa ushirikiano wao kwani vikao hivyo havijawahi kukwama kwa Mkoa wa Singida. 

Alisema kuwa mashauri yanayopangwa yamekuwa yakisikilizwa na thamani ya fedha inayotengwa kuendesha vikao hivyo hutumika kwa malengo yaliyokusudiwa.

Kwa upande, Mkuu wa Gereza la Singida, aliyewakilishwa na Kopolo Mabula Mabula, aliipongeza Mahakama ya Tanzania, hasa Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma kwa kuwa na vikao hivyo ambayo vimesaidia kupunguza msongamano wa Mahabusu gerezani.

Katika taarifa yake alibainisha kuwa hadi kufikia leo tarehe 10 Juni, 2024, Gereza lake lilikuwa na Mahabusu 129, huku wafungwa wakiwa 147, ukilinganisha na uwezo wa Gereza wa kuhifadhi Mahabusu na Wafungwa 330, hivyo kuwezesha kutokuwa na mlundikano.



Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma, Mhe. Edwin Kakolaki (aliyeketi katikati) akieleza jambo katika kikao cha kusikiliza mashauri jinai Mkoani Singida. Aliyeketi kushoto kwa Jaji ni Naibu Msajili Mahakama Kuu Dodoma, Mhe. Sylivia Lushasi na kulia kwake ni Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Hakimu Mkazi Singida, Mhe. Allu Nzowa.


Naibu Msajili Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma, Mhe. Sylivia Lushasi akisoma taarifa fupi mbele ya wadau katika kikao hicho.


Kopolo wa Magereza Mabula Mabula akiwasilisha taarifa ya Gereza kwa niaba ya Mkuu wa Gereza la Singida katika kikao hicho.

Viongozi kutoka Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma waliohudhuria kikao hicho. Aliyesimama wa kwanza kushoto ni Naibu Msajili Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma, Mhe. Upendo Ngitiri na aliyesimama wa kwanza kulia ni Mtendaji wa Mahakama Kuu kanda ya Dodoma, Bw. Sumera Manoti.

(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Musoma)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni