Jumatano, 21 Agosti 2024

MAHAKAMA KUU KANDA YA GEITA YAVUTIA WATUMISHI KUJIFUNZA MATUMIZI YA TEHAMA

Na CHARLES NGUSA-Mahakama, Geita.

Jumla ya watumishi 15 kutoka Mahakama ya Rufani   Tanzania wameshiriki katika mafunzo ya kubadilishana uzoefu katika Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Geita kwenye ziara iliyofanyika hivi karibuni.

 

Watumishi hao waliongozwa na Naibu Msajili wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Agatha Chugulu ambapo malengo ya ziara hiyo ilikuwa ni kujifunza namna bora ya uendeshaji wa mashauri na shughuli zingine za kiofisi kwa kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano(TEHAMA).

 

Awali akizungumza na watumishi hao baada ya kuwasili katika Mahakama hiyo, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Geita, Mhe.  Kevin David Mhina alisema “Geita kwa sasa hatutumii karatasi katika shughuli zetu za uendeshaji wa mashauri na shughuli zingine za kiofisi kama vile shughuli za kiutawala ambazo zote zinafanyika kwa kupitia mfumo wa  kusajili mashauri(CMS) na ofisi mtandao ,hivyo kwa kiasi kikubwa tumeweza kuepuka matumizi ya karatasi kabisa na kuokoa kiasi kikubwa cha pesa ambacho kilikuwa kinatumika kununua shajara na badala yake fedha hizi kuelekezwa katika motisha za watumishi wetu ili kuwaongezea morali ya kufanya kazi.”

 

Watumishi hao, waliweza kupitishwa katika ofisi mbali mbali na kuoneshwa namna shughuli zinavyoendeshwa katika Mahakama hiyo ikiwa ni pamoja na ofisi inayotumika kwa ajili ya “Visual court” pekee  ambapo Mhe. Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Geita, Mhe.Fredrick Lukuna  alisema  chumba hiki ni kwa ajili ya kuendeshea mashauri kwa njia ya mtandao yaani  “Visual Court  “ hivyo hakuna shughuli nyingine inayofanyika. Katika chumba hiki huwa tuna Tv kubwa ambayo kwa mfano labda nyie huko mnaweza kuwa na shahidi yuko huku kwetu hivyo mkiwasiliana nasi tunamwita anaingia katika chumba hiki na anaendelea kutoa ushahidi wake bila wasiwasi.”

 

Aidha, watumishi hao baada ya kumaliza kupitia katika kila ofisi waliweza kuingia ukumbi wa Mahakama ambapo walijifunza mambo mbalimbali ikiwemo mchakato mzima wa ufunguaji wa mashauri mpaka kufikia hatua ya mwisho. 


Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Geita, Mhe. Lukuna aliwaeleza kuwa mchakato unaanza kwa wakili au ofisi ya mashitaka na pengine kupitia kiosiki cha Mahakama kwa wale ambao hawana barua pepe (email) au hawana wakili hivyo hulazimika kuja kwenye kiosiki cha Mahakama kusaidiwa kupandisha nyaraka zao kwenye mfumo na kutumwa kwenda kwa Msajili kwa ajili ya kufanyiwa usajili. 


Mhe. Lukuna aliongeza kwamba baada ya shauri kutoka kwa msajili kama ni la madai, huelekezwa kwenda uhasibu kwa ajili ya kutoa namba ya malipo yaani ‘control’namba kwa ajili ya kulipia  na baadae kwenda kwa Mhe. Jaji Mfawidhi kwa ajili ya kupangiwa Jaji na upangaji wa mashauri hufanywa na mfumo wenyewe.

 

Mhe .Msajili alieleza kuwa katika Mahakama hiyo hawapokei nyaraka ngumu bali wanapokea pokea nakala laini pekee ambazo zinakuja kupitia mfumo wetu na kufanyiwa kazi isipokuwa tu kama mteja hana wakili na wala barua pepe, hivyo huwasilisha nyaraka zake kwenye kiosiki  ili ziweze kupandishwa kwenye mfumo na kuendelea na utaratibu wa kawaida.


Akizungumza kwa niaba ya watumishi hao waliokuja kujifunza, Mkuu wa msafara huo, Mhe.Chugulu amepongeza juhudi zinazoendelea katika Kanda hiyo na kuwashukuru kwa namna ambavyo wameweza kuwa Mahakama ya mfano katika matumizi ya TEHAMA na kwamba wamejifunza mengi na wataenda kuyafanyia kazi yale yote waliyojifunza ili kuboresha huduma katika maeneo yao ya kazi.

 

Baada ya hapo watumishi hao wakiongozwa na wenyeji wao waliweza kutembelea eneo la mradi wa ujenzi wa jengo la Mahakama Kuu Kanda ya Geita ambalo ni kwa ajili ya Mahakama Jumuishi na kwamba kukamilika kwa jengo hilo kutasaidia  kuboresha huduma katika  Kanda hiyo, kwani huduma 

zote zitakuwa zinapatikana katika jengo hilo.


Baadhi ya watumishi wa Mahakama ya Rufani Tanzania waliokuja kujifunza kuhusu namna bora ya matumizi ya TEHAMA wakiwa katika ofisi ya Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Geita, Mhe.Fedrick Lukuna (ambaye hayupo katika picha.

Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Geita, Mhe. Fedrick Lukuna akitoa elimu ya namna mchakato wa ufunguaji wa mashauri kwa njia ya mtandao kuanzia hatua ya kwanza hadi hatua ya mwisho.

Baadhi ya washiriki wakiwa ukumbini wakiendelea kupata elimu kutoka kwa Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Geita, Mhe. Fedrick Lukuna.


Washiriki wakiwa pamoja na wenyeji wao wakitembelea eneo la mradi  wa ujenzi wa jengo la Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Geita.
(Habari hii imehaririwa na Magreth Kinabo)


 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni