Jumatano, 21 Agosti 2024

MTENDAJI MKUU WA MAHAKAMA ATEMBELEA MRADI WA UJENZI KITUO JUMUISHI GEITA

Na CHARLES NGUSA-Mahakama, Geita

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya TanzaniaProf. Elisante Ole Gabriel jana tarehe 20 Agosti, 2024 alitembelea ujenzi wa Kituo Jumuishi Mkoani Geita ili kujionea maendeleo ya mradi huo ambao unatarajiwa kukamilika ndani ya kipindi cha miezi mitatu ijayo.

Akizungumza na  Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Geita, Mhe. Kevin David Mhina baada ya kuwasili ofisini kwake, Mtendaji Mkuu alimpongeza kwa usimamizi bora wa mradi huo kwani umeonekana kuwa na maendeleo mazuri na kasi, ikilinganishwa na miradi mingine inayojengwa kwenye Kanda zingine.

Prof. Ole Gabriel alisema, “Nakupongeza sana Jaji Mfawidhi kwa kuendelea kusimamia kwa ukaribu mradi huu. Inaonesha kabisa kuwa kuna usimamizi wa karibu sana kwa sababu ujenzi huu unaenda vizuri ikilinganishwa na miradi mingine inayoendelea kwenye Kanda zingine.

Vile vile alipongeza juhudi zinazoendelea kuoneshwa katika Kanda hiyo na hasa matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kwani kuna mwenendo mzuri wa kuondoa matumizi ya karatasi katika shughuli zote za uendeshaji. 

Sambamba na hilo, Mtendaji Mkuu alipongeza ushirikiano unaoendelea kati ya Mahakama na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita, kwani kutokana na ushirikiano huo ameipatia Mahakama viwanja kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za Majaji.

Baada ya mazungumzo na Jaji Mfawidhi, Prof. Ole Gabriel alielekea katika eneo la mradi kwa ajili ya kujionea kazi zinavyoendelea na kuzungumza na Mkandarasi pamoja na Mhandisi Mshauri kwa pamoja.

Akiwa katika eneo la mradi, aliwaeleza kuwa jengo hilo linatarajiwa kuzinduliwa mwezi Disemba 2024 na kwamba amekuja kujiridhisha na kuona kazi inaendelea kwa hatua gani mpaka sasa.

Hata hivyo, Mtendaji Mkuu aliwatahadharisha kwamba ujio wake unamaanisha mradi hauendi kwa kasi inayotakiwa, hivyo akawahimiza kuwa makini na kuongeza kasi ya ujenzi.

“Fanyeni kazi masaa 24, kwa maana ya usiku na mchana, vinginevyo matokeo hayatakuwa rafiki sana kwenu na kwetu pia, alisema.

Prof. Ole Gabriel alimweleza Mkandarasi kuwa hajafurahishwa na kasi ya ujenzi inavyoendelea na hajapata sababu ya msingi kwa nini hakuna vifaa vya ujenzi vya kutosha katika eneo la mradi ilihali tayari fedha alishalipwa.

Mtendaji Mkuu alimwelekeza mpaka kufikia Ijumaa vifaa vya ujenzi vinavyohitajika viwe vimefika kwenye eneo la mradi na apewe taarifa juu ya jambo hilo. 

Pia alisisitiza kuwa vifaa vyote vinavyo paswa kusafirishwa kutoka nje ya nchi kama vile “Air conditioners” viletwe mapema ili kuepuka kuvisubiri baada ya kufikia hatua hiyo.

Kwa upande wake, Meneja Mradi  kwa upande wa Mhandisi Mshauri, Bw.  Nkini alimweleza Mtendaji Mkuu maendeleo ya mradi, ikiwa ni pamoja na hatua walizokubaliana kufikiwa katika kikao kilichopita kuwa mpaka sasa wanaendelea vizuri.

Mhandisi Nkini alisema, “Katika kikao kilichopita tulikubaliana kazi ya kuzungusha uzio ianze na ujenzi wa tofali katika jengo uende kwa kasi zaidi, jambo ambalo mpaka sasa linaendelea kutekelezwa kwa asilimia kubwa kama ambavyo inaonekana.

Naye Mwakilishi wa Mkandarasi, Bw. Lee Mancheer, ambaye ndiye Mkurugenzi Mtendaji Tanzania wa Kampuni ya ujenzi ya Shandong High Speedalisema kuwa kwa pamoja wamejipanga vizuri  ili kuhakikisha kuwa wanakamilisha mradi ndani ya kipindi kilichokubalika ili kutokwamisha matarajio.

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (wa kwanza kulia) akiwa katika Ofisi ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Geita, Mhe. Kevin David Mhina alipowasili mkoani Geita.

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Majaji wa Mahakama Kuu, Kanda ya Geita ambapo wa kwanza kulia ni Jaji MfawidhiMhe. Kevin David Mhina na aliyepo kushoto ni Mhe. Jaji Griffin Mwakapeje.

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (aliyevaa overall ya blue) akiendelea na ukaguzi wa mradi wa ujenzi wa jengo la Kituo Jumuishi Geita.

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel akiwa katika kikao cha majumuisho baada ya kumaliza kufanya ukaguzi wa mradi huo.

(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam)


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni