Jumatatu, 26 Agosti 2024

WANAFUNZI KIDATO CHA NNE MLOLE WAFANYA KAZI MRADI MAHAKAMA KUU KIGOMA

Na AIDAN ROBERT, Mahakama-Kigoma 

Jumla ya wanafunzi kumi (10) wa kidato cha nne kutoka Shule ya Sekondari Mlole iliyopo mkoani Kigoma wamefanya kazi mradi (Project) yenye mada isemayo ‘Ni kwa jinsi gani Mahakama inalinda na kutetea haki za makundi maalumu kama vile walemavu, wazee, watoto’ ikiwa ni mchakato wa kuhitimisha masomo yao katika ngazi hiyo ya masomo.

Msaidizi wa Sheria wa Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Victor Kagina akishirikiana na Msaidizi wa Sheria wa Jaji wa Kanda hiyo, Mhe. Valerian Msola, walitoa elimu kwa wanafunzi hao waliofika mahakamani hapo tarehe 23 Agosti, 2024 kuhusu sheria mbalimbali na nafasi ya Mahakama katika kutetea na kulinda haki za makundi maalum ya walemavu, wazee na watoto.

Mhe. Kagina, alisema kuwa, Mahakama inatoa haki kwa mujibu wa Katiba na Sheria na kwamba hujikita katika usahihi wa shauri lililopo mbele ya Mahakama husika ili kuhakikisha kila anaefikishwa au kufika mahakamani anapata haki yake kwa wakati.

Kwa upande wake, Mhe. Msola alisema kuwa, Mahakama ni kati ya Mihimili mitatu ya Dola kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inatimiza wajibu wake kisheria na ni Chombo pekee kinachotoa haki nchini, hivyo ina wajibu wa kulinda haki za makundi yote yakiwemo hayo ya wazee, walemavu na watoto. 

“Mahakamani tunasema haki inaenda na wajibu, haki pekee haiwezi kupatikana bila Mahakama na Wadau kufanya wajibu wao kila mmoja kwa nafasi yake hii italeta afya kwa mada yenu kufahamu juu ya Mahakama kulinda na kutetea makundi hayo,’ alisema Mhe. Msola.

Aidha, aliwataka wanafunzi wasome kwa bidii ili wafikapo katika ngazi ya elimu ya juu waweze kusoma Sheria na baadaye waweze kuwa Wanasheria wazuri na wenye maadili katika kuhudumia jamii ya Watanzania.

 Aliongeza kwa kuwaomba wanafunzi hao kuendelea kuipenda Mahakama na kwamba elimu waliyopata waipeleke katika jamii wanayoishi ili jamii ifahamu kuwa Mahakama ndio chombo pekee kinachotoa haki bila upendeleo wowote.

Kwa upande wake Kiongozi wa Wanafunzi hao, Bw. Imani Mfayokulela Mtondo ambaye naye ni mmoja kati ya wanafunzi hao aliushukuru Uongozi wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma kwa kuridhia wao kuja kujifunza mambo mengi ya historia ya Mahakama na umuhimu wa Mahakama katika jamii ya Watanzania.  

Msaidizi wa Sheria wa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma,  Mhe. Valerian Msola akisisitiza jambo wakati alipokuwa akitoa elimu kwa wanafunzi wa kidato cha nne wa Shule ya Sekondari Mlole iliyopo Kigoma Mjini wakati wanafunzi hao walipotembelea Mahakama hiyo tarehe 23 Agosti, 2024.

Msaidizi wa Sheria wa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe Victor Kagina akifafanua jambo fulani kwa wanafunzi wakati alipokuwa akiwasilisha mada kwa wanafunzi wa kidato cha nne wa Shule ya Sekondari Mlole iliyopo Kigoma Mjini.

Msaidizi wa sheria wa Jaji wa Mahakama kuu ya Tanzania kanda ya kigoma  Mhe. Valerian Msola, akitoa msisitizo kwa wanafunzi wa kidato cha nne wa shule ya sekondari Mlole, iliyopo Kigoma Mjini alipokuwa akitoa mada juu ya histori ya Mahakama ya Tanzania.

Mwanafunzi wa kidato cha nne wa Shule ya Sekondari Mlole, Bi. Victoria Gerald Wilbad akisikiliza kwa makini mada mbalimbali zilizokuwa zikitolewa na Wasaidizi wa Sheria wa Majaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma.

Picha ya pamoja kati ya Wasaidizi wa Sheria wa Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma na wanafunzi wa kidato cha nne kutoka Shule ya Sekondari Mlole Kigoma (waliosimama). Kulia ni Mhe. Victor Kagina na kushoto ni Mhe. Valerian Msola.

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)

 

 

 


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni