Alhamisi, 12 Desemba 2024

JAJI MKUU WA TANZANIA AWAPOKEA, AWAKUBALI MAWAKILI 524 WAPYA

  • Awataka kuzingatia nguzo tano za uweledi za uwakili

Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma leo tarehe 12 Desemba, 2024 amewapokea na kuwakubali Mawakili wa Kujitegemea 524 wapya na kuwataka kuzingatia nguzo tano za uweledi za uwakili wanapotekeleza majukumu yao, ikiwemo kuwa waaminifu na kujisimamia.

Akizungumza katika sherehe hiyo iliyofanyika katika Viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam, Mhe. Prof. Juma ametaja nguzo nyingine kama kuwa na uwezo, kupata heshima, kuwa na ujasiri na kufanya kazi kwa uhuru bila shinikizo.

“Uweledi katika kazi ya Uwakili ni kanuni, tamaduni, tabia, mazoea na taratibu ambazo zimekubaliwa kuwa zinawaongoza Mawakili katika kazi na zinawatambulisha, kuwapambanua na kuwatofautisha na taaluma zingine,” amesema.

Akizungumzia nguzo hizo, Jaji Mkuu amesema kuwa lazima kila Wakili anatakiwa kutambua kuwa uaminifu na kuaminika itampambanua kuwa ni Mawakili mwenye uweledi au la.

“Vipimo na vigezo vya uaminifu na kuaminika kwenu vimetajwa katika Kanuni za Kimaadili, Kiweledi, Nidhamu na Tabia Njema za Mawakili. Kanuni ya 6 ya Kanuni hizi imeainisha mifano ya Mawakili wasio na uaminifu na kukosa uaminifu ni kukosa Uweledi na ukimuona wakili huyo, muepuke,” amesema.

Kuhusu nguzo ya uwezo, Mhe. Prof. Juma amebainisha kuwa kwa vitendo, kwa kauli na kwa viwango vya huduma, lazima Wakili aonyeshe kuwa kweli umesoma Sheria na Shahada ya Sheria na kwamba maandishi na fikra zake zijionyeshe kuwa yeye ni mwanasheria na ni Wakili.

Ameeleza kuwa Kanuni za Kimaadili, Kiweledi, Nidhamu na Tabia Njema za Mawakili za mwaka 2018 zinataka huduma za Wakili zionyeshe uwezo na ujuzi unaotarajiwa kutoka kwa Wakililinganifu na mwanasheria aliyesoma chuo kikuu na kuiva.

“Kanuni za 8 hadi 14 za Kanuni za Kimaadili, Kiweledi, Nidhamu na Tabia Njema za Mawakili, 2018 zinasisitiza wateja wenu, Mahakama na wananchi wanayo haki ya kutarajia kuwa mnao uwezo kufanya kazi ya uwakili itakayokuwa inawakabili,” Jaji Mkuu amesema.

Mhe. Prof. Juma amebainisha pia kuwa kupitia Chama cha Mawakili, Mawakili wanatakiwa kujisimamia, kujiendesha na kujiangalia kiuweledi, kimaadili na kitaaluma bila kuingiliwa na Taasisi za Dola kama Serikali, Bunge na Mahakama.

“Kila Wakili, anao wajibu wa kujisimamia na kuwasimamia Mawakili wenzake ili watekeleze kanuni zinazosimamia Uweledi na Uadilifu wa Mawakili. Kudharau au kutokutekeleza Kanuni zenu wenyewe, ni kuhujumu Uhuru wa Taaluma ya Uwakili na pia manufaa ya umma ambayo Kanuni zenu za Uweledi na Uadilifu zinalenga,” amesema.

Jaji Mkuu amewaambia Mawakili hao pia kuwa katika safari yao ya kufikia uweledi, watatafuta nguzo muhimu ya kupewa “Heshima” bila ya kuiomba au kuidai.

“Heshima hapa ni kwa tabia na mwenendo wa Wakili, kila siku na kila wakati. Jamii inampa heshima, anaheshimika, anawaheshimu Mawakili wenzake, anawaheshimu wateja wake, anawaheshimu Majaji, Mahakimu na anawaheshimu watumishi wote katika mfumo mzima wa utoaji wa haki,” amesema.

Mhe. Prof. Juma amebainisha pia kuwa Wakili mwenye Uweledi au Ubobezi ni kama jengo imara lisilo na nyufa na wananchi watakaofuata huduma za Wakili, hawatakuwa na sababu za kuhofia madhara yoyote. Amesema kuwa zifa zake humtangaza Wakili aliyetimiza safari na kufikia nguzo zote za uweledi na uadilifu.

Akizungumza katika sherehe hiyo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Hamza Johari amewaambia Mawakili hao kuwa wanayo nafasi kubwa katika kuhakikisha jukumu la utoaji haki linatekelezwa kwa ufanisi na Mahakama.

Amesema kuwa kama Maafisa wa Mahakama Mawakili wanapaswa kuhakikisha wanaisadia Mahakama kutekeleza jukumu la utoaji haki nchini kwa kutoa tafsiri sahihi za sheria ili kutenda haki na kuhakikisha wananchi wanapatiwa haki zao wanapokwenda mahakamani au kwenye vyombo vingine vya kisheria.

Katika harakati zenu za kusimamia haki, ni muhimu kujua kuwa jukumu lenu ni kubwa zaidi ya kuwawakilisha wateja. Ninyi ni walinzi wa haki, wawakilishi wa uadilifu, na watetezi wa sheria katika jamii yetu. Malalamiko ya wananchi kuhusu kutotendewa haki yatapungua kwa kiasi kikubwa mkitimiza wajibu wenu kikamilifu,” Mhe. Johari amesema.

Naye Rais wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS), Wakili Msomi Boniface Mwambukuzi amewaeleza Mawakili hao kujenga tabia ya kuheshimu maamuzi yanayotolewa na Mahakama katika ngazi mbalimbali.

“Ukiona haujaridhika, kata rufaa,” amesema na kuwasisitizia Mawakili hao wapya kuwa lazima watambue kuwa kazi yao inatokea ndani ya mfumo wa Mahakama, ambayo ni nguzo muhimu katika utawala wa sharia na utoaji wa haki.

“Kama wawakilishi wa sharia, mnajukumu la kuheshimu Mahakama kama Taasisi. Mahakama siyo tu nisehemu ya kutoa hukumu, bali pia ni chombo cha kuhifadhi na kutetea haki za kila mtu.

Kupokelewa kwa Mawakili hao wapya 524 kunafanya idadi ya Mawakili wa Kujitegemea nchini kufikia 12,995. Kati ya Mawakilinhao wapya 524, wa kiume ni 296 na wa kike ni 228. Mawakili 214 wamepata msamaha wa kutohudhuria Shule ya Sheria Tanzania, 16 walifaulu Mtihani wa Uwani na 294 wamemaliza masomo yao katika Shule ya Sheria.

Miongoni mwa Mawakili wapya waliokubaliwa na kupokelewa leo na Jaji Mkuu ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Wilfred Dyansobera, Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Nkya, Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Chiganga Tengwa, Katibu wa Jaji Mkuu, Mhe. Venance Mlingi, Naibu Wasajili na Mahakimu mbalimbali pamoja na wananchi wengine.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (juu na chini) akizungumza katika sherehe za kuwapokea na kuwakubali Mawakili wapya leo tarehe 12 Desemba, 2024 jijini Dar es Salaam.




Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Hamza Johari akizungumza kwenye sherehe hizo.

Rais wa Chama cha Mawakili Tanganyika, Wakili Boniface Mwambukuzi akizungumza kwenye sherehe hizo.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Hamza Johari (katikati) akiwa na Viongozi wengine wakati wa sherehe hizo.

Wajumbe wa Baraza la Elimu ya Sheria nao walikuwepo.

Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania wastaafu nao walihudhuria sherehe hizo.

Sehemu ya Mawakili wapya waliopokelewa (juu na picha mbili chini).



Sehemu ya Mawakili wapya ikila kiapo. Picha chini wakitoa heshima kwa Jaji Mkuu (hayupo kwenye picha).

Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania waliohudhuria sherehe hizo wakiwa katika picha ya pamoja na Meza Kuu inayongozwa na Jaji  Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati waliokaa).

Meza Kuu inayoongozwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma ikiwa katika picha ya pamoja na Viongozi mbalimbali (juu) na sehemu ya Mawakili wapya (chini).


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni