Alhamisi, 2 Januari 2025

JAJI FREDRICK MWITA WEREMA AAGWA DAR ES SALAAM

Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma leo tarehe 2 Januari, 2025 ameungana na Viongozi wengine wa kitaifa kumuaga Jaji Mstaafu wa Mahakama Kuu ya Tanzania na aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Frederick Mwita Werema, aliyefariki Dunia tarehe 30 Desemba, 2024 katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Shughuli hiyo ya kiserikali ya kumuaga Jaji Werema imefanyika katika Viwanja vya Karimjee, Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam na kuongozwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa.

Mwili wa Marehemu Werema uliwasili katika Viwanja hivyo saa 4.30 asubuhi na kufuatiwa na ibada fupi kabla ya Viongozi mbalimbali wa Taasisi, Mahakama, Bunge na Serikali kutoa salamu za pole.

Katika salamu zake fupi, Jaji Mkuu amemwelezea Mhe. Werema kama mtumishi aliyekuwa na msimamo na uwezo mkubwa wa kutetea Sheria na Katiba. Amesema kuwa nafasi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ni muhimu katika Nchi ambayo Jaji Werema aliimudu vizuri katika utumishi wake.

“Huyu anagusa Mihimili yote ya Dola, ni Mbunge, Wakili namba moja, Mjumbe wa Tume ya Utumishi wa Mahakama. Kwa hiyo, unaweza kuona Rais anapomteua mtu kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali anatakiwa kuwa na sifa na uwezo wa aina gani. Jaji Werema nalikuwa na uwezo huo,” amesema.

Naye Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani, akiwasilisha salamu kwa niaba ya Mahakama ya Tanzania, amesema wamepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za msiba wa Mhe. Werema, siyo kwa sababu ya ukubwa wa nafasi yake, bali utendaji mzuri na mchango alioutoa kwa Mahakama wakati wa utekelezaji wa majukumu kama Jaji.

“Kama familia ya Mahakama ya Tanzania tutamkumbuka Jaji Mstaafu Werema kama Kiongozi na mtoa uamuzi. Tangu alipoamimiwa kuutumikia umma wa Watanzania kwa kuteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu tarehe 28 Novemba, 2006, Marehemu alihudumu kwa uadilifu na weledi mkubwa katika nafasi hiyo,” amesema.

Mhe. Dkt. Siyani amewelezea Marehemu Werema kama mtumishi aliyesimamia misingi ya haki, uwajibikaji na kuheshimu utu wa watumishi wengine bila kujali nafasi zao na kwamba alikuwa mtu mwenye msimamo katika uamuzi wake.

“Marehemu aliamini pia kuwa ushirikiano sehemu ya kazi ni msingi wa mafanikio, kwa kuamini hivyo na hata baada ya kuteuliwa kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Werema aliendelea kushirikiana na Mahakama kwa karibu kuhakikisha kuwa huduma za utoaji haki zinaendelea kuboreshwa,” amesema.

Viongozi wengine waliotoa salamu za pole ni Waziri Mkuu kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungani wa Tanzania, Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Hamza Johari, Mwakilishi wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Wakili Mkuu wa Serikali na Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais Mstaafu, Mhe. Joseph Sinde Warioba.  

Shughuli hiyo ya kiserikali imehudhuriwa pia na Viongozi wengine waandamizi wa Mahakama ya Tanzania, wakiwemo Majaji wa Mahakama ya Rufani, Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Majaji Wastaafu wa Mahakama ya Rufani na Mahakama Kuu, Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Msajili wa Mahakama ya Rufani, Naibu Wasajili, Mahakimu na wengine wengi.

Alikuwepo pia Jaji Mkuu Mstaafu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Mohamed Chande Othman, Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Anna Makinda, mwakilishi wa Wizara ya Katiba na Sheria na Chama cha Mawakilli Tanganyika.

Mwili wa Marehemu Werema utasafirishwa kuelekea Musoma, Mkoa wa Mara kwa mazishi yatakayofanyika tarehe 4 Januari, 2025 katika Kijiji cha Kongote, Butiama.

Mhe. Werema alijiunga na Mahakama tarehe 28 Novemba, 2006 alipoteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania na kuhudumu katika Kanda ya Iringa na baadaye kuhamishiwa katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Biashara.

Jaji Werema aliteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali mwaka 2019 hadi tarehe 16 Desemba, 2014 alipojiuzulu baada ya kutoeleweka kwenye ushari alioutoa kuhusiana na kutokana na kashfa ya Tegeta Escrow katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Mhe. Werema alianza utumishi wa umma mwaka 1984 alipojiriwa kuwa Wakili wa Serikali na baadaye kuteuliwa kuwa Msaidizi wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambaye kwa wakati huo alikuwa pia Waziri wa Sheria. Mwaka 1998, Jaji Werema aliteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Masuala ya Katiba na Haki za Binadamu katika Wizara ya Katiba na Sheria na baadaye mwaka 2006 akateuliwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akitoa pole kwa familia  katika shughuli ya kiserikali ya kumuaga Marehemu Jaji Fredrick Mwita Werema iliyofanyika leo tarehe 2 Januari, 2025 jijini Dar es Salaam.

Viongozi mbalimbali wa kitaifa wakiwa katika maombolezo. Picha chini ni Majaji wa Mahakama ya Rufani na Mahakama Kuu ya Tanzania pamoja na Viongozi wengine Wastaafu.

Mwili wa Marehemu Fredrick Mwita Werema ukiwa katika Viwanja vya Karimjee Dar es Salaam

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa akizungumza katika mambolezo ya kiserikali kumwaga Mhe. Werema. Picha chini ni Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma.



Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani akiwasilisha salamu za pole kwa niaba ya Mahakama ya Tanzania. Picha chini ni  Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akiwasilisha salamu za pole.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa akiuaga mwili wa Mhe. Werema katika Viwanja vya Karimjee Dar es Salaam. Picha chini ni Rais Mtaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete na Mke wake, Mama Salma Kikwete.



(Picha na Bakari Mtaula-Dar es Salaam)



 

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni