Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma ameshiriki katika mazishi ya aliyekuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mstaafu, Mhe. Fredrick Mwita Werema, yaliyofanyika leo tarehe 4 Januari, 2025 katika Kijiji cha Kongoto Wilaya ya Butiama Mkoa wa Mara.
Akitoa salamu za pole, Jaji Mkuu Prof. Juma ameeleza kuwa marehemu Jaji Werema enzi za uhai wake alikuwa na mchango mkubwa kwa Taifa kupitia nyazifa alizoshika Serikalini, hivyo amewaomba waombolezaji kuendelea kumuenzi kwa kusoma maandiko yake ikiwa ni pamoja na hukumu zake zikiwemo hotuba mbalimbali.
“Jaji Werema akiwa Jaji wa Mahakama Kuu kati ya mwaka 2006 hadi 2009, kuna mambo mengi ya kuyakumbuka kwani aliweza kuamua mashauri mengi na alisaidia kutatua migogoro. Vilevile akiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali mwaka 2009 hadi 2014, alichangia kuweka mazingira wezeshi ya Utawala wa Sheria kwa kuwa yeye alikuwa mshauri Mkuu wa Serikali kuhusu masuala ya kisheria,” Jaji Mkuu ameeleza”.
Viongozi wengine walioshiriki mazishi hayo kwa upande wa Mahakama ni Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Ferdinand Leons Katipwa Wambali, Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha, Mhe.Ilvin Claud Mugeta akimuwakilisha Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania.
Aidha Majaji wengine walioshiriki ni kutoka Kanda za Musoma, Mwanza, Shinyanga, Geita, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, akiwemo Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante Ole Gabriel, Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Chiganga Tengwa na viongozi waandamizi pamoja na watumishi wa Mahakama kutoka Makao Makuu, Kanda na Divisheni.
Kwa upande wa Serikali, viongozi mbalimbali walishiriki mazishi hayo wakiongozwa na Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Butiama Mhe. Jumanne Sagini, Mwanasheria Mkuu wa Serikali Bw. Hamza Johari na viongozi wengine wa Serikali kutoka Taasisi mbalimbali.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akitoa salamu za rambirambi.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali Hamza Johari akitoa salamu za rambirambi.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akiweka udongo kwenye kaburi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni