Ijumaa, 10 Januari 2025

TAWJA YAKUTANA NA KUFANYA MAZUNGUMZO NA MAKAMU WA RAIS IKULU CHAMWINO

Na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma

Uongozi wa Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA) wakiongozwa na Mwenyekiti wa Chama hicho, Mhe. Barke Sehel jana tarehe 09 Januari, 2024 walikutana na kufanya mazungumzo na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango. 

Wakiwa katika mazungumzo hayo yaliyofanyika Ikulu Chamwino  jijini Dodoma, Viongozi hao walipata fursa ya kumueleza Makamu wa Rais kuhusu historia, malengo pamoja na mikakati ya Chama hicho.

Aidha walieleza kuwa, Dira kuu ya TAWJA ni kukuza haki za binadamu na usawa kwa wote. Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ambayo inalenga kuwa na mifumo imara ya kisheria na kitaasisi na kwamba TAWJA inaangazia zaidi kukuza haki na usawa kwa wanawake, watoto na makundi mengine hatarishi kama wazee. 

Walimueleza Kiongozi huyo kwamba, TAWJA ina Mpango Mkakati wake wa miaka mitano ulioainisha maeneo 10 muhimu ya ufuatiliaji hadi kufikia mwaka 2028/2029 ambayo maeneo hayo ni pamoja na kukuza Haki za Binadamu na usawa kwa wote hasa kwa wanawake, wasichana na makundi mengine hatarishi nchini Tanzania Bara na Zanzibar, kukuza upatikanaji wa haki kwa wanawake wote.

Kuimarisha taaluma kwa Maafisa Sheria wanawake katika ngazi zote za mahakama na kusambaza taarifa zinazohusu Maafisa sheria wanawake, kuwezesha Wanawake kwenye Mahakama kukabiliana na upendeleo wa kijinsia katika Sheria na Utekelezaji wake.

Maeneo mengine ya Mkakati huo ni kubuni na kuunga mkono programu na shughuli za kupinga na kuondoa aina zote za ukatili na dhuluma katika jamii, kwa kujikita zaidi kuhusu ukatili dhidi ya wanawake, watoto, na makundi mengine hatarishi.

Kushiriki katika Mikutano ya Kitaifa, Kikanda, na Kimataifa, kubadilishana Uwezo kupitia vikao, semina, na programu za mafunzo kwa Maafisa wa kisheria wanawake ili kuongeza uelewa wao kuhusu mambo mbalimbali ya kijamii, kiuchumi, na kitamaduni yanayoathiri wanawake katika majukumu yao katika utendaji wa haki.

Viongozi wengine walioambatana na Mhe. Sehel ni  pamoja na Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mbeya na Makamu Mwenyekiti wa TAWJA, Mhe. Victoria Mlonganile Nongwa, Naibu Mrajis Mahkama Kuu Pemba, Mhe. Chausiku Kuya na Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya Kinondoni na Mweka Hazina wa TAWJA, Mhe. Nabwike Ezekiah Mbaba. Kadhalika Viongozi hao waliambatana na  Jaji Mstaafu wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Sophia Wambura. 

Zifuatazo ni picha mbalimbali za Viongozi wa Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA) walipokutana na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango.




Hakuna maoni:

Chapisha Maoni