Na Ally Ally Ramadhani –Mahakama, Katavi
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya
Sumbawanga, Mhe. Fedrick Manyanda amewataka wajumbe wa Kamati ya Maadili ya
Maafisa Wilaya ya Mlele mkoani Katavi kuzingatia maadili wanaposhughulikia
malalamiko yanayowahusu Mahakimu.
Jaji Mfawidhi wa Kanda ya Sumbawanga aliyasema hayo tarehe
19 Mei, 2025 alipokuwa akimuapisha Mkuu wa wilaya ya Mlele Bw. Majid Mwanga
kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya Maafisa Mahakama wa wilaya hiyo pamoja
na wajumbe Kamati hiyo.
Akizungumza mara baada ya kuwaapisha wajumbe hao, Jaji
Mfawidhi wa Kanda hiyo alisema kuwa Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama hazina
budi kutekeleza majukumu yake kwa Uadilifu na kwa kufanya hivyo itasaidia
kuimarisha amani na usalama katika wilaya husika na Taifa kwa ujumla.
Mhe. Manyanda pia aliikumbusha kamati kupitia tangazo la
Serikali, tangazo Namba 1001 la mwaka 2020, na kuona jinsi lilivyo ainisha
mienendo ya Maafisa Mahakama.
Kamati ya Maadili ya Maafisa Mahakama wilaya ya Mlele inaundwa
na Mhe. Majid Hemed Mwanga (Mkuu wa wilaya ya Mlele na Mwenyekiti wa Kamati),
Bw. Yusuf Mwenda (Katibu Tawala wa
wilaya ambaye ni Katibu wa Kamati) Mhe. Lilian Moses Ndelwa (Mjumbe), Mhe.
Nickson Temu (Mjumbe), Mhe. Fahamu Kibona (Mjumbe), Shekhe Awamu Kasoma
(Mjumbe), Chief Michael Mbogo (Mjumbe).
Tume ya Utumishi
wa Mahakama ni chombo cha kikatiba kilichopewa jukumu la kusimamia uendeshaji
wa Mahakama ya Tanzania. Moja ya jukumu lake ni kusimamia Maadili ya
Maafisa Mahakama ili kuhakikisha Mhimili wa Mahakama unatekeleza jukumu lake la
msingi na la kikatiba la kutoa haki kwa wananchi.
Jukumu la kusimamia Maadili ya Maafisa Mahakama,
pamoja na majukumu mengine ya Tume, yameainishwa katika Ibara ya 113 (1) ya
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kifungu cha 29 cha Sheria ya
Usimamizi wa Mahakama Sura ya 237.
Ili
kutekeleza jukumu la kusimamia Maadili ya watumishi wa Mahakama ya
Tanzania, Tume inazo Kamati zilizoundwa kuisaidia kwenye jukumu hili. Kifungu
cha 33 (1) cha Sheria ya Usimamizi wa Mahakama Namba 4 Sura ya 237 kimeiruhusu
Tume kukasimu utekelezaji wa majukumu yake kwenye kamati zilizoundwa chini ya
sheria hiyo. Baadhi ya kamati hizo ni Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama za
Mikoa na Wilaya.
Caption 2: Pichani ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga Mhe: Fedrick Kapela, akiwa na kamati ya maadili ya Maafisa wa Mahakama Wilaya ya Mlele.
Mhe. Majid Hemed Mwanga – Mkuu wa wilaya Mlele, akiapishwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu kanda ya Sumbawanga Mhe. Fedrick Kapela Manyanda, Kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya maafisa wa mahakama wilaya ya Mlele.
(Habari hii imehaririwa na Lydia Churi-Tume ya
Utumishi wa Mahakama)
.jpg)
.jpg)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni