·
Wavutiwa
zaidi na maboresho ya matumizi ya TEHAMA ndani ya Mahakama ya Tanzania
·
Jaji Kiongozi
awashauri juu ya matumizi ya 'ADR' kutatua migogoro
·
Na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma
Ujumbe kutoka Mahakama ya Kenya umewasili nchini Tanzania lengo likiwa
ni kuitembelea Mahakama ya Tanzania ili kujifunza na kubadilishana uzoefu
kuhusu uboreshaji wa huduma ya utoaji haki kwa wananchi.
Ujumbe huo ambao umeongozwa na mkuu wa msafara
ambaye ni Msajili Mkuu wa Mahakama ya Kenya, Mhe. Winifrida Mokaya umewasili
Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma leo tarehe 20 Mei, 2025 na
kupokelewa na Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Kiaki Nkya na Maafisa
wengine wa Mahakama nchini.
Aidha, baada ya kuwasili katika viunga vya
Makao Makuu wa Mahakama, wageni hao walipata fursa ya kukutana na kufanya
mazungumzo na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher
Mohamed Siyani.
Akizungumza na ugeni huo, Mhe. Dkt. Siyani amesema
kuwa, ni muhimu kufanya maboresho ndani ya Mahakama kwakuwa Mahakama nyingi
ikiwemo za barani Afrika na hata Ulaya zimekuwa zikilalamikiwa kufuatia ucheleweshaji
wa utoaji haki.
“Kazi
zetu kama Mahakama, kazi za kutoa haki zimekuwa zikilalamikiwa, kote Kenya, Tanzania
na karibu kila nchi duniani, wakati fulani nilikuwa nikifanya tafiti nikifikiri
kwamba wenzetu katika nchi zilizoendelea hakuna ucheleweshaji wa utoaji haki lakini
hali haiko hivyo, kuna milundikano pia tuna matatizo yanayofanana karibu kila
mahali,” amesema Mhe. Dkt. Siyani.
Amesema kuwa, ili kuleta maboresho katika
huduma ya utoaji haki kuna umuhimu wa kuangalia upya michakato/ taratibu za utoaji
haki katika kila eneo (business process re-engineering).
Ametoa rai kwa ugeni huo kuhakikisha wanajua
wanachofanya ili kutekeleza jukumu la msingi ambalo Wakenya wamewapa la utoaji
haki kwa haraka. Ameongeza kuwa, eneo la matumizi ya Teknolojia ya Habari na
Mawasiliano (TEHAMA) ni muhimu kuzingatiwa katika kuhakikisha haki inapatikana kwa
wakati.
“Hakuna
namna yoyote tunaweza kuendesha au kubadili taratibu za utoaji huduma bila
kuhusisha matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), michakato
yetu ya utoaji haki ndio iliyofanya kuwa na ucheleweshaji pamoja na mambo mengine,
lakini kama tunaweza kubadili namna tunavyotoa haki tunaweza kuharakisha
upatikanaji wa haki,” amesisitiza Jaji Kiongozi.
Aidha, Jaji Kiongozi amesema kuwa, jambo lingine
ambalo linapaswa kuangaliwa ili kuharakisha huduma ya utoaji haki ni matumizi
ya utatuzi wa migogoro kwa njia mbadala/ usuluhishi (Alternative Dispute
Resolution) kwa kuwa inasaidia kupunguza muda wa kusikiliza mashauri kama
ilivyo katika usikilizaji wa mashauri kwa njia ya kawaida.
Kadhalika,
Mhe. Dkt. Siyani amewakumbusha wageni hao kutoka Mahakama ya Kenya juu ya umuhimu
wa Mahakama kupata imani ya wananchi, ambapo amesisitiza kwa kusema kuwa, “kwa Mahakama imani ya wananchi ni mtaji, chochote
mtakachofanya hakikisheni wananchi wanawaamini.”
Ameongeza kwa kuueleza ujumbe huo kwamba, ili
kuboresha huduma ya utoaji haki kuna umuhimu wa wao kuweka malengo yanayokubalika
ili kuwapima Maafisa Mahakama wakiwemo Majaji na Mahakimu waliokasimiwa jukumu
la kusikiliza mashauri ili waweze kusikiliza kwa wakati.
Kwa upande wake, Msajili Mkuu wa Mahakama ya
Kenya, Mhe. Winifrida Mokaya amesema kuwa, ziara yao imelenga katika kujifunza kuhusu maboresho
mbalimbali ikiwemo matumizi ya TEHAMA, masuala ya ushirikishwaji wa wadau
katika masuala ya Mahakama, Vituo Jumuishi vya Utoaji Haki (IJCs’) na kadhalika.
“Mahakama
tuna mipango kadhaa ya maboresho ya utoaji huduma ya haki kwa kuondoa vikwazo
vinavyozuia upatikanaji wa haki kwa wakati, ambayo hivyo ziara yetu imejikita
kujifunza kuhusu maboresho mbalimbali ambayo Mahakama ya Tanzania mmefanikiwa
kufanya ambayo ni pamoja na matumizi ya TEHAMA, utoaji huduma katika Mahakama
zinazotembelea (Mobile Court Services), Vituo Jumuishi vya Utoaji Haki (IJCs’),” amesema Mhe.
Mokaya.
Aidha, Mhe. Mokaya amesema kuwa, eneo lingine ambalo wanatamani kuliona na kujifunza jinsi linavyofanya kazi ni Chumba maalum cha kutolea taarifa za Mahakama (Judiciary Situation Room) kwakuwa nao wana mpango wa kuanzisha chumba hicho muhimu.
Kwa upande wake Msajili Mkuu wa Mahakama ya
Tanzania, Mhe. Nkya ameuhakikishia ujumbe huo kuwa, kile walichokusudia
kukipata kutoka Mahakama ya Tanzania watapata kwakuwa wamejipanga vizuri
kuhakikisha wanatoa majibu ya maswali yao kupitia mawasilisho mbalimbali
yaliyoandaliwa kwa ajili ya ujumbe huo.
Aidha, Msajili Mkuu ameueleza ujumbe huo kuwa,
historia ya maboresho ya Mahakama nchini ilianza miaka ya nyuma na
ripoti za Kihistoria, kama vile Tume ya Msekwa ya 1977 na Ripoti ya Bomani ya
1986, ziliangazia masuala muhimu ambayo yanazuia ufanisi wa Mahakama, ambapo zilipendekeza
juu ya marekebisho ya kimuundo na
ufadhili wa kutosha.
“Mabadiliko makubwa
yalikuja mwaka 2011 kwa kupitishwa kwa Sheria ya Utawala wa Mahakama, ambayo
ilianzisha ofisi za Msajili Mkuu na Mtendaji Mkuu wa Mahakama, pamoja na Mfuko
wa Mahakama, hii iliashiria mwanzo wa Mpango wa Mageuzi unaoongozwa na Mahakama
ambao unasisitiza kuboresha upatikanaji wa haki, kuongeza ufanisi wa mahakama,
kuhakikisha uwazi, na kukuza ushiriki wa raia,” amesema Mhe. Nkya.
Aidha, amewaeleza wajumbe
kutoka Mahakama ya Kenya kuwa, Mahakama ya Tanzania imepiga hatua kubwa katika
matumizi ya TEHAMA katika shughuli zake na hivyo kuwezesha upatikanaji wa haki
kwa haraka.
Baada ya hafla fupi ya
kuwakaribisha wageni hao, walipata wasilisho kutoka Mkurugenzi Msaidizi kutoka
Kurugenzi ya Usimamizi wa Mashauri Mahakama ya Tanzania, Mhe. Hawa Mnguruta ambaye
aliwasilisha kuhusu namna ambavyo Mahakama ilivyofanya marekebisho katika
mchakato mzima wa kuendesha shughuli zake (business process re-engineering) na
mada kuhusu Mfumo wa Unukuzi na Tafsiri (TTS) ambapo wamepata nafasi ya kuuliza maswali na kujibiwa.
Programu ya ujumbe huo kutoka
Mahakama ya Kenya ni ya siku tano. Siku
ya kwanza ya ziara yao tarehe 19 Mei, 2025 ujumbe huo ulipata fursa ya
kutembelea Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Msaidizi wa Usimamizi wa Mashauri Mahakama ya Tanzania, Mhe. Hawa Mnguruta akiwasilisha mada mbele ya wageni (hawapo katika picha) kutoka Mahakama ya Kenya uliopo nchini kwa lengo la kujifunza kuhusu Maboresho ya Mahakama.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni