Alhamisi, 4 Septemba 2025

BENKI YA DUNIA YAPONGEZA KASI YA UJENZI WA JENGO LA IJC KATAVI

Na. Ally Ally Ramadhani – Mahakama, Katavi

Kiongozi wa Msafara wa Benki ya Dunia Bi. Christine Owuor, amepongeza kasi ya maendeleo ya ujenzi wa jengo la Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Mkoa wa Katavi.

Ameyasema hayo jana tarehe 03 Septemba, 2025 wakati wa ziara ya hiyo iliyokuwa na lengo la kukagua mradi wa ujenzi jengo hilo la kisasa la Mahakama ya Tanzania ya litakalo tumika kutoa haki kwa wananchi wa Mkoa huo.

Akitoa taarifa ya  maendeleo ya mradi wa ujenzi wa jengo la hilo mkoani hapo Mhandisi  Victor Vedasto ambaye ni mwakilishi wa Mkandarasi kampuni ya AZHAR Construction Co. Ltd, alisema mradi huo umefikia asilimia 76.1 za utekelezaji wake na kuongeza kuwa tayari kazi za umaliziaji wa jengo zinaendelea.

Aidha, Mhandisi huyo aliongeza kuwa, mradi huo unahusisha sehemu tatu ambazo ni jengo Kuu, eneo la nje (uzio, mgahawa, chumba cha ulinzi) pamoja na Manzari (Landscaping).

Vilevile, akieleza kuhusu mradi huo, Mhandisi na mtaalam wa manunuzi Bw. Fedrick Nkya kutoka Benki ya Dunia alishauri kuzingatia uwepo wa mfumo wa mifereji ya kupitisha maji nje ya jengo ili kuzuia maji kuingia eneo la jengo hasa kipindi cha mvua za masika.

Naye, Mkuu wa Kitengo cha Maboresho ambaye pia ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Angelo Rumisha akiwa kwenye ziara ya Benki ya Dunia ya kukagua  mradi wa ujenzi wa jengo hilo la Mahakama, alisema jengo hilo linalojengwa na Kampuni ya AZHAR Construction Co. Ltd. linatarajiwa kukamilika Mwezi Novemba, 2025.

Jaji Rumisha aliongeza kuwa, ”tumepokea pongezi hili linatupa nguvu ya kuendelea kuongeza kasi kwa kushirikiana na timu nzima ili ifikapo mwezi Novemba 2025 mradi wetu uwe umekamilika kama tulivyo kubaliana na kampuni inayojenga jengo letu la IJC – Katavi”.

Mkuu wa Kitengo cha Maboresho ya Mahakama aliongeza kuwa, nguzo ya pili ya Mpango Mkakakati wa miaka mitano wa Mahakama ya Tanzania inasisitiza Utoaji Haki kwa wakati. Mahakama ya Tanzania inatekeleza mpango huu kwa kuboresha mazingira ya utoaji haki na kusogeza huduma za utoaji haki karibu zaidi na wananchi kwa kujenga miundombinu bora na wezeshi itakayochangia ufanisi mzuri wa utekelezaji wa nguzo hiyo.

Kiongozi wa msafara wa Benki ya Dunia Bi. Christine Owuor, (wa kwanza mbele) akikagua ujenzi wa IJC KATAVI.

Mhandisi Victor Vedasto, akitoa maelezo kuhusu maendeleo ya mradi wa ujenzi wa jengo la Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Katavi kwa kiongozi wa msafara wa Benki ya Dunia Bi. Christine Owuor.


Msanifu Linda Kasilima, mshauri wa mradi kutoka kampuni ya Crystal Consultant akielezea maendeleo ya Mradi wa ujenzi IJC KATAVI kwa timu ya msafara wa Benki ya Dunia.


Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Mkuu wa Kitengo cha Maboresho Mhe. Dkt. Angelo Rumisha akitoa maelezo kwa kiongozi wa Msafara wa Benki ya Dunia wakati wa ziara ya ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi wa IJC Katavi.


 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni