Alhamisi, 4 Septemba 2025

JAJI MKUU AWAAGIZA MAJAJI, WATENDAJI WA MAHAKAMA KUANZA UTEKELEZAJI WA DIRA, 2050

·       Asisitiza pia uwajibikaji katika kazi

·       Atoa rai kwa Majaji, Watendaji kusimamia maadili ya watumishi walio chini yao

Na MARY GWERA, Mahakama- Dodoma

Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju amewataka Majaji na Viongozi wa Mahakama nchini kuanza maandalizi ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo, 2050 kwa kufuata miongozo iliyowekwa ya utekelezaji wa dira hiyo.

Akizungumza jana tarehe 03 Septemba, 2025 wakati akifunga Kikao Kazi cha siku tatu cha Majaji Wafawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania kilichofanyika kwenye ukumbi wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma, Mhe. Masaju alisema kuwa, eneo la Utawala bora na Haki ni kipaumbele cha kwanza kilichoainishwa katika Dira hiyo hivyo, ni muhimu kwa Mahakama kushiriki katika utekelezaji wake ili kuboresha eneo la utoaji haki.

“Niwaombe tufanye maandalizi sasa kwa ajili ya utekelezaji wa Dira hii kwa mujibu wa mwongozo tuliowekewa na hii dira imeweka pia mpango wa utekelezaji,” alisema Jaji Mkuu.

Mhe. Masaju alisema huku akirejea ukurasa wa 63 wa Dira hiyo ambao unasema, “ili kuhakikisha kuwa Dira 2050 inatekelezwa kwa ufanisi, Serikali imeweka mfumo imara wa usimamizi unaozingatia malengo yake mahsusi, mfumo huu umekusudia kuhimiza uwajibikaji, ukihitaji uongozi mahiri na ulio makini katika ufuatiliaji, aidha mfumo unahimiza matumizi ya mbinu zitakazotoa matokeo yanayopimika.”  

Aliwahimiza viongozi hao kwa kuwaeleza kuwa, ambao bado hawajasoma Dira hiyo, kuisoma ili kuielewa ipasavyo na kuanza utekelezaji wake. Akisisitiza kuwa, Dira hiyo inasisitiza kwamba, msingi wa mkakati huo ni mabadiliko makubwa ya kifikra ambayo yanalenga kwenye vitendo zaidi kuliko maneno na matokeo badala ya ahadi.

Akirejea Dira hiyo, Jaji Mkuu alisema, “Uongozi, Taasisi pamoja na watendaji na wadau wote wanapaswa kuwajibika kutimiza malengo la dira kwa ufanisi......”

Kadhalika, Jaji Mkuu aliwakumbusha Majaji hao kuendelea kuishi viapo vyao na kusimamia haki ipasavyo kwa kuzingatia Katiba na Sheria  za Nchi.

"Tutambue tunalo jukumu kubwa, kwanza Ibara ya 4 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 107A na Ibara ya 107B, sote tunazifahamu  lakini kubwa hapa sisi Mahakama ya Tanzania tumepewa jukumu ya kuwa mamlaka yenye kauli ya mwisho katika utoaji haki katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na katika hizi Ibara nilizozisoma hapa zimeweka na kanuni na mwongozo ukiacha yale maadili mengine ya utumishi wa Mahakama, niwaombe tuendelee kuzingatia haya," alisisitiza Mhe. Masaju.

Jaji Mkuu aliendelea kuwasisitiza Majaji na Mahakimu kutekeleza jukumu la utoaji haki ipasavyo kwani ni kazi ambayo wamekasimiwa na Mungu na inatambulika hata kwenye Vitabu Vitakatifu vya Mungu ikiwemo Biblia na Quran, na kuwasihi kusoma Biblia kwenye Kitabu vya ‘Kumbukumbu la Torati 4:2, 6, Kutoka 18:21-22 na 2 Mambo ya Nyakati 19: 6-7.

Aidha, Mhe. Masaju aliwataka pia Majaji hao kudumisha umakini katika utekelezaji wa majukumu ili Mhimili wa Mahakama ya Tanzania uwe moja ya Mhimili wenye hadhi duniani.

Katika hatua nyingine, Jaji Mkuu alitoa rai kwa Majaji, Mahakimu, watumishi wa Mahakama na wananchi wote kwa ujumla kuwajibikaji katika utekelezaji wa majukumu yao.

“Uzoefu wangu ni kana kwamba wengi serikalini tumekuwa tukidhani kwamba mambo ya Taifa hili yanamuhusu Rais wa nchi wa hii peke yake na Viongozi kama Mawaziri na viongozi wengine Wakuu wa Mihimili na Watendaji Wakuu katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na kwetu sasa mahakamani tunafikiri kwamba mambo haya yanamuhusu Jaji Mkuu, Jaji Kiongozi, Mtendaji Mkuu, Msajili Mkuu, Msajili wa Mahakama ya Rufani na hata Msajili wa Mahakama na wengine sisi sote hatuwajibiki,” alisema Mhe. Masaju.

Aliongeza kuwa, wengine wanadhani kwamba suala la uwajibikaji linawahusu makao makuu ya Mahakama ya Tanzania peke yake lakini wengine hatuhusiki na wakati fulani hata ambao wanahusika kwenye ngazi ya kanda wanadhani kwamba yanawahusu wao peke yao.

“Wakishatambua wajibu huo, kila mmoja atajiona ni mhusika kuanzia kiongozi wa juu kabisa mpaka mwananchi wa kawaida tukiwemo na sisi viongozi,” alisisitiza Mhe. Masaju.

Kadhalika, Jaji Mkuu alisema kuwa, ili kuboresha uwajibikaji ni muhimu watumishi wa Mahakama kuzingatia na kusimamia haki kwa kuhakikisha haki inatendeka, uadilifu, uwezo wa kumudu majukumu ipasavyo, kujiongeza, kuwa na ubunifu na kuwa na uzalendo wa nchi.

“Majaji Wafawidhi wasimamieni watumishi waliopo chini yenu kwa kutoa ushauri, kuwalea na inapobidi kutoa adhabu wanapokwenda kinyume na maadili,” alisisitiza Mhe. Masaju.

Katika kikao hicho ambacho kilihudhuriwa pia na baadhi ya Majaji wa Mahakama ya Rufani, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mtendaji Mkuu, Msajili Mkuu na Wajumbe wa Menejimenti ya Mahakama kwa pamoja walipata fursa ya kubadilishana uzoefu katika utendaji kazi, kushirikishana kuhusu mafanikio na changamoto.

Kikao hicho kimetoka na maazimio kadhaa baadhi yake ni kuwa na ushirikishwaji wa viongozi katika miradi ya ujenzi katika hatua zote, kuimarisha utatuzi wa migogoro kwa njia ya usuluhishi (mediation), haki za watumishi za kisheria zilipwe mapema ipasavyo na kikamilifu, ufanisi wa mifumo ya kielektroniki ya usikilizaji mashauri (TTS na e-CMS) ufanyiwe tathmini na kuboreshwa ili iwe rafiki zaidi kwa watumiaji na mengine.


Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju akizungumza na Majaji Wafawidhi na Menejimenti ya Mahakama ya Tanzania (hawapo katika picha) wakati akifunga Kikao Kazi cha siku tatu cha Majaji Wafawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania  jana tarehe 03 Septemba, 2025 kwenye ukumbi wa mikutano wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.




Washiriki wa Kikao Kazi cha Majaji Wafawidhi wakiwa katika kikao hicho jana tarehe 03 Septemba, 2025 kwenye ukumbi wa mikutano wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.





    Washiriki wa Kikao Kazi cha Majaji Wafawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania wakifuatilia kilichokuwa kikijiri katika kikao hicho kilichofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma tarehe 03 Septemba, 2025.

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni