Jumatano, 3 Septemba 2025

MAHAKAMA SPORTS YAANZA KIBABE MASHINDANO YA SHIMIWI JIJINI MWANZA

Na EUNICE LUGIANA, Mahakama-Mwanza

Timu za Kamba (wanaume na wanawake), Mpira wa Pete na Mpira wa Miguu zimeanza vema michuano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara, Idara, Wakala za Serikali na Ofisi za Wakuu wa Mikoa (SHIMIWI) inayoendelea kwenye viwanja mbalimbali jijini Mwanza.

Katika michezo ya siku ya kwanza wanawake walivutana na Ofisi ya Katibu Tawala (RAS) Kagera na kutoka na ushindi wa bao mbili (2) kwa 0 katika mchezo huo wa vuta nikuvute Mahakama wanawake walifanikiwa kuvuta mivuto yote miwili na kupata ushindi.

Na katika siku ya pili Mahakama walivutana dhidi ya Timu ya Wizara Katiba na Sheria na kufanikiwa kuwavuta mivuto yote miwili hivyo kuondoka na ushindi.

Akizungumza baada ya mechi hiyo jana tarehe 02 Septemba, 2025, Nahodha Msaidizi wa Timu ya Kamba Wanawake, Bi. Eva Mapunda alisema siri ya ushindi huo ni mazoezi na ndio maana wanapata matokeo mazuri.

Aidha, Nahodha huyo amemuahidi Mtendaji Mkuu wa Mahakama kuwa, watarudi na ushindi mnono na vikombe, kutokana na malezi mazuri wanayoyapata kambini hapo.

Kwa upande wa mchezo wa kamba wanaume ambapo siku ya kwanza walivutana na timu kutoka Viwanda na kufanikiwa kuwavuta mivuto yote miwili kama karatasi na kujichukulia pointi mbili  lakini katika mchezo wa pili baada ya kuona viwanda walivyovutwa kama karatasi Timu ya Kilimo waliingia mitini na kutokutokea uwanjani na hivyo kusababisha ushindi.

Katika michezo hiyo ya kamba kwa wanawake na wanaume iliyofanyika katika viwanja vya Furahisha jiji Mwanza timu za Mahakama wameshinda mechi zote mbili katika hatua hii ya makundi.

Nayo Timu ya Mpira wa Pete ya Mahakama imefanikiwa kushinda katika mchezo wake wa kwanza kwa kuifunga Timu ya GST magoli 41 kwa 11 katika mchezo uliofanyika katika viwanja vya CCM Kirumba, Nahodha wa timu hiyo, Akanganyila Theophil alisema wapinzani hao walikuwa wa kawaida na hivyo kusababisha ushindi huo kupatikana na kuongeza kuwa wamejiandaa vizuri kwa mechi ijayo ambapo wanatarajia ushindi mnono.

Katika mtanange uliofanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Mabatini B kati ya Timu ya Mahakama na Kilimo, kilimo walichokikimbia asubuhi kwenye kamba wanaume wamekutana nacho kwenye mpira wa miguu kwa kuchabangwa bao mbili kwa nunge, magoli hayo yalifungwa dakika ya 17 na ya 26 ya kipindi cha pili. Magoli hayo yote yalifungwa na mchezaji Muhamadi Ghafuru.

Kocha wa Timu ya Mpira wa Miguu, Spear Dunia Mbwembwe alisema ushindi huo uliopatikana ni salamu za shukrani kwa Mtendaji Mkuu wa Mahakama, Prof. Elisante Ole Gabriel kwa kuwezesha timu kuishi vizuri kupata malazi mazuri, chakula na mavazi kwa kupindi chote tangu wamefika kambini hapo na hivyo Kocha huyo kuahidi kurudi na  vikombe.

Mashindano ya SHIMIWI yalianza tarehe 01 Septemba, 2025 na yanatarajiwa kufunguliwa rasmi tarehe 06 Septemba 2025. Mahakama ya Tanzania imepeleka jumla ya timu tisa ambazo ni Timu za Mpira wa Miguu, Mpira wa Pete, Kamba (wanawake na wanaume), Riadha, Baiskeli, Tufe, Karata na Bao.

Kikosi cha Timu ya Mpira wa Miguu cha Mahakama kabla ya mtanange.


Timu wa kamba wanawake baada ya mechi dhidi ya Ofisi ya Katibu Tawala (RAS) Kagera.

Timu ya Kamba Wanaume baada ya mechi dhidi ya Viwanda.

Kikosi cha Timu ya Mpira wa Pete kabla ya mechi kuanza.

Mfungaji wa Timu ya Mahakama akifunga goli.

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni