Jumanne, 2 Septemba 2025

NAIBU MSAJILI MAHAKAMA ARUSHA ASISITIZA USHIRIKIANO NA JESHI LA POLISI

Na SETH KAZIMOTO, Mahakama-Arusha

Naibu Msajili Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha, Mhe. Amir Msumi amesema kuwa ushirikiano baina ya Mahakama na Jeshi la Polisi ni muhimu ili kuhakikisha mashauri ya jinai yanayoletwa mahakamani yanasikilizwa mapema ipasavyo kuepuka kuchelewesha haki za watu pamoja na kuzuia mlundikano wa mashauri usio wa lazima.

Mhe. Msumi aliyasema hayo hivi karibuni alipokuwa akifungua Mafunzo ya Kubadilishana Uzoefu Kuhusu Utaratibu wa Ufunguaji na Uendeshaji wa Mashauri ya Jinai katika Mahakama za Mwanzo yaliyofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) jijini Arusha.

Akizungumza wakati wa ufunguzi, Naibu Msajili alieleza kuwa, mafunzo hayo yalilenga kuongeza uelewa, kuimarisha weledi na kukuza ushirikiano kati ya Mahakama na Jeshi la Polisi lengo likiwa ni kuhakikisha mashauri ya jinai yanashughulikiwa kwa haraka, ufanisi na kwa mujibu wa sheria.

“Nawaomba washiriki kutumia kikamilifu fursa hii ya mafunzo kwa kuuliza maswali, kujadili changamoto na kubadilishana mbinu bora zinazoweza kusaidia kuboresha huduma za utoaji haki katika ngazi ya Mahakama za Mwanzo,” alisisitiza Mhe. Msumi.

Akiwasilisha mada, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Mwanzo Themi, Mhe. Julieth Mbise alieleza kuwa, zipo changamoto nyingi zinazokwamisha uendeshaji wa haki jinai, ikiwemo kasoro katika hati za mashtaka, ucheleweshaji wa vielelezo, kutokuwepo kwa walalamikaji mahakamani na kutofuatwa kwa taratibu za upelelezi.

Mhe. Mbise alisisitiza kwamba, ushirikiano madhubuti kati ya Mahakama na Polisi ni muhimu ili kuhakikisha haki inatolewa kwa wakati na kuimarisha imani ya wananchi kwa vyombo vya utoaji haki.

Naye Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya ya Arusha, ASP Mahita Omary alizungumzia changamoto zinazolikabili Jeshi la Polisi katika kushughulikia mashauri kuwa, ni pamoja na watuhumiwa kujidhamini, adhabu ndogo zinazotolewa na Mahakama pamoja na Mahakama kuahirisha mashauri bila kujali kwamba mashahidi wameletwa kwa ajili ya shauri husika kusikilizwa.

Akizungumzia kuhusu suala la watuhumiwa kujidhamini wenyewe katika Mahakama za Mwanzo, ASP Mahita alisema kuwa, pamoja na kwamba dhamana ni haki ya mtuhumiwa kwa makosa yenye dhamana, Mahakama imekuwa ikitoa dhamana bila kuwa na taarifa za kina za mtuhumiwa na mdhamini wake, hali ambayo husababisha mtuhumiwa kutorudi mahakamani na Mahakama kulazimika kutoa tena hati ya kukamatwa mtuhumiwa huyo kwa Jeshi la Polisi.

Akitoa neno la kufunga mafunzo hayo, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Arusha, Mhe. Sheila Manento aliwahimiza washiriki kuzingatia uadilifu na weledi katika utekelezaji wa majukumu yao, akibainisha kuwa hakuna haki bila uaminifu.

Aliwataka pia washiriki kuendeleza kujifunza kila mara ili kuendana na mabadiliko ya dunia ya sasa na kuwapongeza waandaaji wa mafunzo hayo kwa maandalizi bora na kuwashukuru washiriki wote kwa nidhamu na ushirikiano waliouonesha.

Kikao hicho kililenga kujadili changamoto, kueleza athari zake katika upatikanaji wa haki na kutoa mapendekezo ya uboreshaji, ikiwemo kuongeza ushirikiano kati ya Mahakama na Jeshi la Polisi, mafunzo endelevu kwa askari na matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika kutoa taarifa kwa walalamikaji.

Mafunzo haya yaliandaliwa na Mahakimu Wafawidhi wa Mahakama za Mwanzo katika Wilaya ya Arusha, ambazo ni Mahakama ya Mwanzo Themi, Arusha Mjini na Terat na kuratibiwa na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Arusha.

Wajumbe mbalimbali walihudhuria mafunzo hayo wakiwemo Mahakimu Wakazi wote wa Mahakama za Mwanzo katika Wilaya ya Arusha pamoja na wawakilishi kutoka Jeshi la Polisi.


Naibu Msajili Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha, Mhe. Amir Msumi(aliyesimama) akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo baina ya Mahakama za Mwanzo wilayani Arusha na Jeshi la Polisi, mafunzo hayo yalifanyika hivi karibuni kwenye ukumbi wa mikutano wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC). Kulia kwake ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Arusha, Mhe. Sheila Manento na kushoto ni Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya ya Arusha, ASP Mahita Omary.

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Arusha, Mhe. Sheila Manento akizungumza wakati wa mafunzo kati ya Mahakama za Mwanzo wilayani Arusha na Jeshi la Polisi, mafunzo hayo yalifanyika hivi karibuni kwenye ukumbi wa mikutano wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Arusha.

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Mwanzo Themi, Mhe. Julieth Mbise akiwasilisha mada wakati wa mafunzo baina ya Mahakama za Mwanzo wilayani Arusha na Jeshi la Polisi yaliyofanyika hivi karibuni kwenye ukumbi wa mikutano wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC).

Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya ya Arusha, ASP Mahita Omary akichangia jambo wakati wa mafunzo baina ya Mahakama za Mwanzo wilayani Arusha na Jeshi la Polisi, mafunzo hayo yalifanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Arusha tarehe 29 Agosti, 2025.

Mkuu wa Kituo Msaidizi, Inspekta Hassan Ibrahim akiwasilisha taarifa ya Jeshi la Polisi wakati 
 wa mafunzo baina ya Mahakama za Mwanzo wilayani Arusha na Jeshi la Polisi yaliyofanyika hivi karibuni kwenye ukumbi wa mikutano wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC).

Washiriki wa mafunzo baina ya Mahakama za Mwanzo wilayani Arusha na Jeshi la Polisi wakiwa katika picha ya pamoja. Mafunzo hayo yalifanyika hivi karibuni kwenye ukumbi wa mikutano wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Arusha.

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)

 

 



 

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni