Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Arusha
Jaji Kiongozi wa Mahakama
Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani amewakumbusha Wadau wa Haki
Jinai kwenye uhifadhi wa Wanyamapori kuzigatia haki wanapotekeleza majukumu yao
katika ngazi mbalimbali.
Mhe. Dkt. Siyani ametoa
wito huo leo tarehe 9 Septemba, 2025 alipokuwa anazungumza kabla ya
kumkaribisha Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju, kufungua Kikao
Kazi cha Wadau hao kinachofanyika kwa siku tatu jijini hapa.
Jaji Kiongozi amewaambia
washiriki wa Kikao Kazi hicho kuwa Mahakama imepewa jukumu la mwisho la kutoa
haki, lakini haki haianzii mahakamani, bali huanzia kwenye hatua mbalimbali,
ikiwemo katika utoaji wa taarifa za makosa ya jinai.
‘Haki inatakiwa kuonekana
katika upelelezi, ukamataji, uamuzi wa kushtaki au la, uandaaji wa mashtaka na uendeshaji
wa mashauri yenyewe kabla ya Mahakama kutoa uamuzi. Kwa msingi huo, sisi sote
tunashiriki kazi ya kutoa haki katika hatua mbalimbali,’ Mhe. Dkt. Siyani
amesema.
Amebainisha kuwa msingi
wa kazi hiyo ni Mungu na Wadau hao wanajua vizuri kuwa Dini zote zinahubiri
haki na haki inayohubiriwa hawamtendei Mungu, bali wanapaswa kutendeana wao wenyewe
kama binadamu, lakini na viumbe vingine ambavyo Mungu kwa utashi wake
ameviumba.
Jaji Kiongozi ametumia
fursa hiyo pia kuwakumbusha Wapelelezi katika vyombo vyote nchini na Waendesha Mashtaka
kuwa wanapotekeleza wajibu wao, Katiba inawataka kuongozwa na mambo matatu
makubwa, ikiwemo dhamira ya kutenda haki.
‘Kwa kila kinachofanyika,
katika hatua zote za kusimamia haki, kila mmoja wetu atangalize swali hilo
kwenye nafsi yake; la kwanza ni nini dhamira yake. Je, amebeba dhamira ya kutenda
haki, amejiepusha na matumizi mabaya ya taratibu za kutoa haki…
‘… na je, anachokifanya
kinabeba maslahi ya umma? Rai yangu kwenu ni kuwa kila wakati tuzielekeze
dhamira zetu ndani ya mipaka hiyo na kufanya chochote nje yake ni kukosa
uzalendo kwanchi yetu,’ Mhe. Dkt. Siyani amesema.
Akizungumzia umuhimu wa Wanyamapori,
Jaji Kiongozi ameeleza kuwa kibailojia, na kwa mujibu wa Convention of
Biological Diversity (CBD) 1992, thamani inayoletwa na Wanyamapori ni pamoja na
thamani za kiikolojia, thamani za kijenetiki, kijamii, kisayansi, kielimu,
kitamaduni, burudani, na thamani za kisanii.
Hata hivyo, amesema, ingawa
wamejaribu kuwapa Wanyamapori thamani ya kifedha, ukweli ni kwamba thamani ya Wanyamapori
haiwezi kufafanuliwa kwa fedha.
‘Thamani hii kubwa ndiyo
iliyotufanya tukutane kwa ajili ya kuhakikisha mgongano wa maslahi ya sasa ya
mwanadamu unaotishia uwepo wa wanyama unashughulikiwa kwa wivu na nguvu kubwa
ya pamoja,’ Mhe. Dkt. Siyani amesema.
Amebainisha pia kuwa Wanyamapori
ni zawadi kwa nchi nyingi duniani na kwa Tanzania wana sifa nyingine za kipekee
mbazo zinautofautisha urithi huo na nchi nyingine na kutoa mfano uhamaji wa
Nyumbu Serengeti ni tukio la aina yake lenye mkusanyiko mkubwa zaidi wa Wanyama
duniani.
Mifano mingine ni uwepo
wa viumbe adimu kama vile Faru weusi waliohatarini kutoweka, Tumbili wa
Kipunji, Simba wengi zaidi barani Afrika, kundi kubwa la Tembo huko Tarangire,
na moja ya ngome kubwa za mbwa mwitu wa Kiafrika huko Selous.
‘Kutokana na umuhimu huu
wa kipekee, tumekutana hapa kujadiliana na kubadilishana uzoefu juu ya namna
bora ya kulinda urithi huu kwa kila mmoja wetu kama Taasisi kutimiza wajibu
wake,’ Jaji Kiongozi amesema.
Kikao Kazi hicho
kinawaleta pamoja Majaji Wafawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania,Viongozi Waandamizi
wa Mahakama ya Tanzania, Wadau wa Haki Jinai kutoka Shirika la Hifadhi za Taifa
[TANAPA], Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Jeshi la Polisi, Taasisi ya Kudhibiti na
Kupambana na Rushwa [TAKUKURU] na Viongozi na Watendaji wengine kutoka Mahakama
Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi.
Kauli mbiu ya Kikao Kazi
hicho inasema, ‘Haki kwa mazingira: Kuongeza ushirikiano kati ya Mahakama na Teknolojia
katika kupambana na uhalifu wa Wanyamapori nchini Tanzania [Justice for Nature:
Enhancing Judicial and Technological synergy in combating wildlife crime in Tanzania.]
Mada mbalimbali
zitawasilishwa na Wawezeshaji ambao waliobobea kwenye masuala ya uhifadhi,
ikiwemo mafanikio na changamoto katika ulinzi wa Wanyamapori Tanzania, matumizi
ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano [TEHEMA] katika mfumo wa haki jinai na ulinzi
wa wanyamapori.
Mada nyingine ni, Mianya, Changamoto na fursa za maboresho na matumizi ya sayansi katika uendeshaji wa mashauri yahusishayo uhalifu dhidi ya Wanyamapori, mchango wa Mahakama katika ulinzi na matumizi anuai ya rasilimali zetu, kukuza utalii, lakini pia tahadhari dhidi ya msongo wa mawazo utokanao na kazi.

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni