Jumanne, 9 Septemba 2025

WATUMISHI MBEYA WAPATA ELIMU YA MABORESHO YA KANUNI ZA MIRATHI

Na. Daniel Sichula-Mahakama, Mbeya

Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya Mhe. Said Kalunde hivi karibu alifungua mafunzo ya marekebisho ya kanuni za mirathi kwa Mahakama za Mwanzo za Mwaka 2025 kwa Mahakimu, Maafisa Utumishi na Wahasibu wa Mahakama ya Wilaya ya Mbeya.

Mafunzo hayo yaliendeshwa katika Ukumbi wa Mikutano wa Mahakama Kuu Mbeya kwa kuwajumuisha watumishi wa kada hizo yamelenga kuwajengea uelewa wa pamoja watumishi hao wanapokuwa wanashughulikia mashauri ya mirathi.

Akizungumza wakati wa kufungua mafunzo hayo Mhe. Kalunde aliwashukuru wakufunzi kwa kuandaa mafunzo hayo kwani yatasaidia katika kuelewa mabadiliko na kuboresha utendaji kazi katika kushughulikia mashauri ya Mirathi kwa Mahakama za Mwanzo.

“Mafunzo haya yanaweza kutuonesha tulikotoka na tunako kwenda na hii itasaidia kutujengea uelewa kwetu sisi sote, na kuweza kutoa elimu hii tutayoipata hapa kwa wengine huko ili tuweze kusaidia jamii katika suala zima la mirathi,” alisema Mhe. Kalunde

Aidha, wakufunzi wa mafunzo hayo Mhe. Adriano Julius Mtafya pamoja na Mhe. Mayonga Manyeresa walisema elimu hiyo kwa washiriki juu ya kanuni mbalimbali za mirathi zilizoboreshwa na vipengele vyake ni shirikishi hasa kwa wanufaika

“Itasaidia warithi kuitwa kuthibitisha orodha ya mali na hesabu za warithi, utaratibu wa kusikiliza mapingamizi, maombi ya kutengua msimamizi wa mirathi, kuongezwa kwa akaunti maalum za mirathi na maboresho katika usikilizwaji wa mapingamizi na kufungua mirathi pamoja na ujazaji wa fomu mbalimbali za mirathi,” alisema Mkufunzi huyo.

Katika majadiliano washiriki walitoa maoni juu ya maboresho ya kanuni mbalimbali zilizofanyika katika kushughulikia mashauri ya mirathi pamoja na changomoto zitakazo jitokeza kutoka kwa wadau mbalimbali.

“Ni muhimu mafunzo haya yawafikie pia wadau wengine kama vile maofisa wa benki, ardhi na jamii kwa ujumla ili uendashaji wa mashauri ya mirathi yaweze kutolewa maamuzi kwa haki na kwa wakati na kuondoa malalamiko kwa wanufaika wa mirathi,” alisema mmoja wa washiriki.

Akifunga mafunzo hayo, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Wilaya Mbeya Mhe. Teddy Mlimba kwa niaba ya Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya aliwashukuru wakufunzi kwa elimu ya maboresho ya kanuni mbalimbali za mirathi waliyoitoa na kwa washiriki wote waliohudhuria mafunzo.

“Kwa elimu iliyotolewa itatusaidia sana katika uendeshaji wa mashauri ya mirathi kwenye Mahakama zetu, hivyo basi nawasihi Mahakimu tuwe makini katika uendeshaji wa mashauri ya mirathi,” alisema Mhe. Mlimba

Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya Mhe. Said Kalunde alifungua mafunzo ya marekebisho ya kanuni za mirathi kwa Mahakama za Mwanzo za Mwaka 2025, kulia ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mbeya Mhe. Victoria Nongwa

Sehemu ya washiriki mafunzo ya marekebisho ya kanuni za mirathi kwa Mahakama za Mwanzo za Mwaka 2025.
Sehemu ya washiriki mafunzo ya marekebisho ya kanuni za mirathi kwa Mahakama za Mwanzo za Mwaka 2025.
Sehemu ya washiriki mafunzo ya marekebisho ya kanuni za mirathi kwa Mahakama za Mwanzo za Mwaka 2025.

Mkufunzi wa mafunzo Mhe. Adriano Mtafya akitoa elimu juu ya maboresho ya kanuni mbalimbali za mirathi kwa Mahakama za Mwanzo

Mkufunzi wa Mafunzo hayo Mhe. Mayonga Manyeresa akielezea maboresho ya matumizi ya fomu za mirathi kwa washiriki




Hakuna maoni:

Chapisha Maoni