Jumanne, 9 Septemba 2025

VUMBI LATIMKA SHIMIWI MWANZA HUKU MAHAKAMA SPORTS IKING’ARA

  • Juster Tibendelena Apeperusha Bendera Mita 3000

Na EUNICE LUGUIANA-Mahakama, Mwanza

Mwanariadha wa Timu ya Mahakama ya Tanzania [Mahakama Sports], Justa Tibendelana (Atugonza) amepeperusha vyema bendera ya Mahakama kwa kuwa mshindi wa kwanza katika mbio za mita 3000 baada ya kutumia dakika 12 kwenye Mashindano ya Shirikisho la Michezo kwa Wizara, Idara, Wakala za Serikali na Ofisi za Wakuu wa Mikoa (SHIMIWI) yanayofanyika jijini Mwanza.

Mbio hizo zimefanyika jana tarehe 8 Septemba, 2025 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba na kuwakutanisha wanaridha kutoka idara mbalimbali.

Katika mbio za mita 200, Mahakama Sports iliwakilishwa na Mwajabu Bwire na Yunus Mkurukute  kwa kuwa washindi wa tatu nay a pili, mtawalia, wakati kwenye mita 100 Mahakama Sports iliwakilishwa na Leah Ndanda na kushika nafasi ya tatu na katika Mita 400 mwakilishi Edger Maiko Mtimba alishika nafasi ya kwanza.

Katika mbio za kupokezana vijiti (relay), Timu ya Mahakama Wanawake ilifanikwa kushika nafasi ya kwanza na Wanaume nafasi ya pili.

Kutokana na matokeo hayo, Mahakama Sports imefanikiwa kuingia fainali katika mashindano mbio kwa mita 100, 200, 400 na mbio za kupokezana vijiti.

Wakati huo huo, Timu za Kamba Wanawake na Wanaume zimefanikiwa kuingia robo fainali ambapo upande wa Wanawake wamevuta na Timu kutoka Ofisi ya Wakili Mkuu na kufanikiwa kuwavuta mivuto yote miwili na kwa upande wa Wanaume ikavutana na Ofisi ya Mashtaka na kufanikiwa kuwavuta.

Mkimbiaji wa mita 3,000, Justa Tibendelana, maarufu Atugonza akikimbia katika mshindano hayo.

Timu ya Ridha Wanawake na Wanaume ya Mahakama katika picha ya pamoja kabla ya kuanza mashindano.

 

Sehemu ya wachezaji wa Timu ya Kamba Wanawake wakijiandaa kukabiliana na timu kutoka Ofisi ya Wakili Mkuu (hawapo pichani).

 

Sehemu ya wachezaji wa Timu ya Kamba Wanaume wakijiandaa kukabiliana na timu kutoka Ofisi ya Mashtaka.

Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Arusha.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni