Ijumaa, 24 Oktoba 2025

MAHAKAMA MOROROGO YAWEKA MIKAKATI MBADALA KUHUSU UFUNGAJI MIRATHI

Na AYSHER JUMA-Mahakama, Morogoro

Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Morogoro, imeweka mikakati mbadala ya kushughulikia changamoto ya kutofungwa kwa mashauri ya mirathi kwa wakati.

Mikakati hiyo imewasilishwa katika kikao cha menejimenti kilichoongozwa na Kaimu Mwenyekiti wa kikao, Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Stephen Magoiga.

Kikao hicho kilifanyika tarehe 22 Oktoba, 2025 katika ukumbi namba mbili wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC), Morogoro.

Kikao hicho kililenga kufuatilia kwa karibu mwenendo wa mashauri na hali ya kiutawala katika Mahakama zote ndani ya Kanda ya Morogoro.

Katika uchambuzi wa mashauri mbalimbali, mashauri ya mirathi yalibainika kuwa mengi hayajafungwa kutokana na sababu mbalimbali kama vifo vya wasimamizi wa mirathi, matatizo ya kiafya, migogoro ya kifamilia, kesi kuingia kwenye mchakato wa rufaa na zaidi ya yote, ukosefu wa uelewa wa kisheria juu ya hatua ya mwisho ya kufunga mirathi.

Kutokana na changamoto hizo, kikao kiliazimia kuanzisha kampeni maalum iitwayo “Oparesheni Funga Mirathi” ambayo inalenga kuwafikia wananchi kupitia vyombo vya habari, mitandao ya kijamii, Viongozi wa mitaa, Viongozi wa kimila, pamoja na kuwasiliana na warithi au wasimamizi wa mirathi kupitia simu ili kuhamasisha na kurahisisha hatua ya kufunga mashauri husika.

Akisoma taarifa ya Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Morogoro, Hakimu Mfawidhi wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Mary Kallomo alieleza kuwa baadhi ya mikakati iliyowekwa katika robo ya tatu ya mwaka 2025 imetekelezwa kwa mafanikio makubwa.

Alisema utekelezaji wa adhabu mbadala umechangia kwa kiasi kikubwa kupungua kwa idadi ya wafungwa, pia  mahabusu kwa Mahakama za Hakimu Mkazi na Mahakama za Wilaya na kutokuwa na Mahabusu  wa Mahakama za Mwanzo, hivyo kufanya maelekezo ya Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju kutekelezeka kwa asilimia 100.

Mbali na mikakati ya kuondoa changamoto ya ufungaji mirathi, Kanda ya Morogoro kupitia kikao hicho kimeazimia kuingia na baki sifuri kwa Mahakama zote za Mwanzo na  baki single digit  kwa Mahakama za Wilaya.

Kwa upande wa maendeleo ya kiutawala, taarifa kutoka kwa Mtendaji wa Mahakama Kanda ya Morogoro, Bw. Ahmed Ng’eni ilieleza hali ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwa ni pamoja na maendeleo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano [TEHAMA], majengo mapya ya Mahakama, viwanja vya Mahakama na uboreshaji wa miundombinu.

Alisema kuwa Mahakama mpya zinaendelea kujengwa katika maeneo ya Bwakila, Minepa, Ngoheranga, Kilosa na Magubika, ambapo baadhi ya miradi hiyo inafadhiliwa na Benki ya Dunia, na mingine ni sehemu ya mipango ya ndani ya Mahakama ya Tanzania, hususan kutumia fedha kutoka serikalini.

Kikao hicho kilihudhuriwa na wajumbe mbalimbali wakiwemo Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Morogoro, Mahakimu Wafawidhi wa Mahakama za Wilaya zote, Maofisa Utumishi kutoka Wilaya mbalimbali, Mkaguzi wa Ndani, Maofisa TEHAMA na Wahasibu wa Mahakama. 

Wajumbe hao walielezea kuunga mkono kampeni ya “Oparesheni Funga Mirathi” na kuahidi kutoa ushirikiano ili kuhakikisha kuwa mashauri yote yaliyosalia yanafungwa kwa wakati na kwa mujibu wa sheria.



Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Stephen Magoiga akiongoza kikao hicho.

Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Morogoro, Bw. Ahmed Ng’eni  akisoma taarifa ya hali ya utekelezaji wa miradi mbalimbali.


Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Morogoro, Mhe. Mary Kallomo akisoma taarifa ya  Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Morogoro.

Sehemu ya wajumbe walio hudhuria kikao hicho.

Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni