Ijumaa, 24 Oktoba 2025

MAHAKAMA MOSHI, ARUSHA NA MANYARA ZAUSIMAMISHA MJI WA MOSHI KWA BONANZA LA MICHEZO

  •  Mahakama Kuu Kanda ya Moshi yaibuka kidedea katika Bonanza hilo
  • Mamia ya wananchi wajitokeza viwanja vya ‘Moshi Club’ kushuhudia mtanange baina ya timu kutoka Moshi, Arusha na Manyara
  • Jaji Mfawidhi, Mhe. Dkt. Mongella asisitiza Michezo kuwa kipaumbele kwa watumishi wa Mahakama katika kukabiliana na Magonjwa yasioambukiza
  •  Michezo kuwa nyenzo ya ushirikiano kwa watumishi kwa Kanda ya Moshi, Arusha na Manyara

Na PAUL PASCAL, Mahakama-Moshi

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Moshi, Mhe. Dkt. Lillian Mongella amewataka watumishi wa Mahakama kuwa na utamaduni wa kukutana mara kwa mara na kufanya mazoezi na kushiriki kwenye michezo mbalimbali itakayowahusisha watumishi wa kada zote ili kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza pamoja na kuimarisha afya zao.

Mhe. Dkt. Mongella aliyasema hayo 18 Oktoba 2025 katika Uwanja wa Moshi (Moshi Club) wakati wa uzinduzi wa Bonanza maalum kwa watumishi wa Mahakama wa Kanda za Moshi, Arusha na Manyara ambapo alisema, lengo ni kuwakutanisha watumishi wote pamoja kufahamiana na kukumbushana wajibu wa kutekeleza majukumu yao ya kila siku. 

"Watumishi waliofika hapa ni sisi wenyeji Moshi na wageni wetu kutoka Kanda ya Arusha na Manyara lengo ni kufahamiana, kukosoana, kukumbushana na kufurahi, kwa kuwa michezo ni afya. Pia inafuta madaraja baina ya watumishi na Viongozi na kuweka uwanja wa kusikiliza changamoto, maoni na ushauri kutoka kwa watumishi wa vituo vyote, bonanza hili lina sura ya Siku ya Familia ya Watumishi wa Mahakama japo sisi tumeegemea kwenye mazoezi na michezo zaidi,” alisema Jaji Mfawidhi huyo. 

Mhe. Dkt. Mongella aliwataka watumishi wote kuwa na ratiba ya michezo katika vituo vyao ambapo alisema, “kwa sisi wa Mahakama Kuu Moshi tunafanya mazoezi kila siku ya Jumanne na Alhamisi kuanzia saa 10:30 Jioni, vema wote tukaiga utamaduni huu kwa maslahi ya afya zetu.”

Kwa upande wake Mgeni Rasmi katika Bonanza hilo ambaye alikuwa Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Manyara, Mhe. Ilvin Mugeta aliwahimiza watumishi kushirikiana katika maeneo ya kazi.

“Tukitaka kufanikiwa katika kufikia malengo yetu, suala la ushirikiano ni lazima liwepo kati yetu tutumie michezo na mazoezi kama nyenzo ya kujenga ushirikiano baina yetu na kukiwa na ushirikiano baina ya watumishi ni dhahiri tunakwenda kutimiza majukumu yetu yote kwa urahisi turejee methali isemayo, ‘umoja ni nguvu utengano ni udhaifu,” alisema Mhe. Mugeta.

Alisema, pasipokuwa na ushirikiano baina ya vituo hivyo vinakwenda kuanguka, hivyo aliwasisitiza watumishi hao kushirikiana katika maisha ya kazini, maisha ya baada ya kazi na jamii zinazowazunguka.

Katika Bonanza hilo, Mahakama Kuu Kanda ya Moshi iliibuka mshindi wa jumla kwa kufanikiwa kukusanya jumla ya medali 27 kati ya 38 zilizokuwa zikishindaniwa katika bonanza hilo. Washindi wote katika Bonanza hilo walipatiwa zawadi za makombe na medali.

Mahakama Kuu Kanda ya Moshi iliandaa na kufanya Bonanza la michezo lililokusanya washiriki na watazamaji wapatao 1,200 wakishuhudia na kushiriki michezo ya Riadha mita 1,200 kwa wanaume mita 1000 na kwa wanawake mita 100 kwa viongozi, mpira wa miguu wanaume, mpira wa pete wanawake, kukimbia na yai, mchezo wa karata, bao, drafti, ‘pool table’, kukimbia na gunia, mashindani ya kula tikiti, mashindani ya kufukuza kuku pamoja na kuimba muziki.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Manyara, Mhe. Ilvin Mugeta (Mgeni rasmi katika bonanza) akipiga penati katika viwanja vya Moshi Club tarehe 18 Oktoba, 2025 wakati wa ufunguzi wa Bonanza la Michezo lililowashirikisha watumishi wa Mahakama Kanda ya Moshi, Arusha na Manyara.


Wacheza bao, Timu ya Mahakama Kuu Moshi wakichuana vikali na wapinzani wao kutoka Timu ya Mahakama Kuu Manyara ambapo Mahakama Kuu Moshi iliibuka Mshindi wa kwanza katika mchezo huo.

Wacheza 'pool table' Timu ya Mahakama Kuu Kanda ya Arusha wakichuana vikali na wapinzani wao kutoka Timu ya Mahakama Kuu Moshi ambapo Mahakama Kuu Arusha waliibuka Mshindi wa kwanza katika mchezo huo.

Mshindi wa mbio Mita 1,500 wanaume, Bw. Godlisten Mwingereza (aliyebebwa) akishangilia pamoja na mashabiki wa Mahakama Kuu Kanda ya Moshi baada ya kuibuka mshindi katika mbio hizo.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Lillian Mongella (kulia) akipokea tuzo ya Mshindi wa jumla kutoka kwa Mkuu wa Mashtaka Mkoa wa Kilimanjaro, Bi. Esther Mfuse baada ya Mahakama Kuu Moshi kuibuka mshindi wa jumla katika mashindano hayo kwa kupata medali 27 kati ya 38.

Wachezaji wa Mbio za Magunia Timu ya Mahakama Kuu Moshi wakichuana vikali na wapinzani wao kutoka Timu ya Mahakama Kuu Manyara na Arusha ambapo Mahakama Kuu Moshi iliibuka Mshindi wa kwanza katika mchezo huo.

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)

 

 

 


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni