· Awasisitiza Majaji, Mahakimu Wanawake kusimamia maadili ya jamii
· Asisitiza usawa kati ya Mwanamke na Mwanaume
Na MARY GWERA,
Mahakama-Dodoma
Jaji Mkuu wa Mahakama ya
Tanzania, Mhe. George Masaju amesema Majaji na Mahakimu Wanawake nchini wana
wajibu mkubwa wa kusimamia haki za binadamu, maadili ya jamii na usawa wa
kijinsia ili kuleta ustawi katika jamii.
Akizungumza jana tarehe 23
Oktoba, 2025 wakati akifungua Mafunzo kwa Waratibu wa Chama cha Majaji na
Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA) kwenye ukumbi wa Mikutnao wa Makao Makuu ya
Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma, Mhe. Masaju alisema kupitia mafunzo hayo ni
muhimu wakaweka mikakati thabiti itakayowezesha kufikia ustawi katika jamii.
“Ninachoona ni kwamba
ninyi TAWJA mnajitambua, wajibu wenu leo ni kuja na mikakati ambayo itawezesha
kutatua hizi changamoto ambazo zimekuwa zinajitokeza kwenye haya masuala yanayowahusu
na hasa haki za binadamu wote ambao humo wanajumuishwa Wanawake na Wanaume
wakiwa wa umri mbalimbali, wengine watu wazima, wengine wazee na wengine Watoto
kwa mfano kuna changamoto hii ya makosa unyanyasaji wa kijinsia,” alisema Jaji
Mkuu.
Mhe. Masaju alibainisha kuwa,
kumekuwa na makosa ya unyanyasaji wa kijinsia na wakati fulani kumekuwa na
tafsiri ambayo sio sahihi kwamba jinsia inawahusu Wanawake tu, lakini ni pamoja
na wanaume, na hata wanaume kwa wakati au namna fulani nao wananyanyaswa na wa
jinsia tofauti.
“Ninatambua kwamba tatizo
la unyanyasaji wa wanawake pengine ni wa kiwango kikubwa kuliko ukilinganishwa
na unyanyasaji wa wanaume, lakini na wanaume wananyanyaswa isipokuwa tu
wanavumilia, jamii yetu imeweka mfumo ambao mwanaume hapaswi kuonekana kama ni
dhaifu vile lakini wanavumilia tu na wakati fulani wanapoteza maisha mapema na
wakishapotea ndio tunawatambua umuhimu wao, mimi nawashauri muendelee kuwajali
wakiwa hai, nawahakikishia kila mmoja anamuhitaji mwenzake, mwanaume
anamuhitaji sana mwanamke na mwanamke anamuhitaji sana mwanaume,” alisisitiza
Jaji Mkuu.
Aidha, Mhe. Masaju
aliongeza kwa kusisitiza kuhusu usawa wa kijinsia ambapo amesema hata Nembo ya
Taifa ya Tanzania nayo imeonesha umuhimu kwa kuwa ina Bibi na Bwana, “Mimi si
mtaalamu sana wa masuala ya nembo za Taifa japo najua nembo za taifa za Mataifa
yote Duniani lakini Tanzania ni ya pekee, Nembo ya Taifa letu inamtambua
Mwanaume na Mwanamke na usawa unaanzia pale kama binadamu na wote wanapewa
uhuru wa rasilimali za Nchi, hawa ndio wananchi wanaounda Taifa la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania kama inavyoelezwa kwenye Ibara ya 1 ya Katiba ya Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania ambayo inasema (i) Tanzania ni Nchi moja nayo ni
Jamhuri ya Muungano na Ibara ya 2 (1) inaeleza; Eneo la Jamhuri ya
Muungano ni eneo lote la Tanzania Bara na eneo lote la Tanzania Zanzibar na
pamoja na sehemu yake ya Bahari ambayo Tanzania inapakana nayo.”
Alisema kupitia Nembo
hiyo, kila mmoja anaonekana akiwa ameshika Pembe ya Ndovu ambayo ndio utajiri
urithi wa Taifa la Tanzania na kiwango cha pembe walichoshika ni sawa kwa
hazitofautiani kwa urefu ama ufupi, juu ya nembo hiyo pia kuna Taifa la
Tanzania ambao ndio wanamiliki rasilimali za Taifa na nyingine zilizomo kwenye
nembo hiyo....
Jaji Mkuu alisema,
misingi ya umoja kati ya umoja Mwanaume na Mwanamke ilishawekwa tangu Taifa
lipate uhuru na ndio ilipokuja kauli ya ‘Uhuru na Umoja’ hivyo, Mwanaume na
Mwanamke wanaounda Taifa la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakiwa
wanaheshimiana, watakuwa huru na wamoja, na kila mmoja amepewa fursa ya kufaidi
matunda ya uhuru na rasilimali za nchi na stahili zake nyingine zote.
“Sasa wajibu wetu sisi
TAWJA ni kutambua changamoto zinazofanya tusifikie hayo malengo ambayo yapo
tangu kuasisiwa na kwa Taifa hili na yamesisitizwa pia katika Katiba Ibara ya
7, 8, 9, 11 lakini pia Ibara ya 22; Ibara ya 22 na 24 zinasema; kila mtu anayo
haki ya kufanya kazi; hivyo; mtaendelea kutambua changamoto zipi zinazofanya
kwa mfano wanawake wakose hizo fursa,” alisisitiza Mhe. Masaju.
Aliongeza kwamba, Ibara (2) inasema; ‘kila raia anastahili fursa na haki sawa kwa
masharti ya usawa ya kushika nafasi yoyote ya kazi na shughuli yoyote iliyo
chini ya mamlaka ya Nchi; “hivyo nyie kama Viongozi mtajifunza ni namna gani
mtaweza kuimarisha fursa ya ku ‘access’ hivi vitu maana havitakuja kwa
upendeleo,” alisisitiza Jaji Mkuu.
Mhe. Masaju alisema,
Majaji na Mahakimu hao wao kama Wanasheria wanaofahamu Katiba na Sheria
mbalimbali wana nafasi kubwa ya kuwa chachu ya mabadiliko chanya katika
kuimarisha usawa na heshima ya kijinsia katika Taifa.
“Ibara ya 24 ya Katiba ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhusu kumilika mali inasema; ‘kila mtu anayo
haki ya kumiliki mali na haki ya hifadhi ya mali yake aliyo nayo kwa mujibu wa
sheria’,” alisema Jaji Mkuu huku akiongeza kuwa hata mwanamke ana haki ya
kumiliki mali kama vile Ardhi na kadhalika.
Aidha, Mhe. Masaju
alibainisha kwamba, Ibara ya 7 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
inasema, ‘Bila kujali masharti ya Ibara (2) ya Ibara hiyo, Serikali,
vyombo vyake vyote na watu wote au mamlaka yoyote yenye kutekeleza mamlaka ya
utawala, Madaraka ya kutunga sheria au Madaraka ya Utoaji haki watakuwa na
jukumu na wajibu wa kuzingatia, kutia maanani na kutekeleza masharti yote ya
sura hiyo, na Ibara ya 8 inasema Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni Nchi
inayofuata misingi ya demokrasia na haki ya kijamii...’
Mhe. Masaju
amekihakikishia Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA) kuwa Mahakama
ya Tanzania itaendelea kuwaunga mkono jitihada zinazofanywa na Chama hicho
katika kuleta usawa wa kijinsia.
Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju (katikati) akiwa katika picha za pamoja na makundi mbalimbali ya Wanachama na Waratibu wa Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA) wakati wa hafla ya ufunguzi wa Mafunzo kwa Waratibu wa Chama hicho. Aliyeketi kushoto ni Jaji wa Mahakama ya Rufani na Mwenyekiti wa Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA), Mhe. Barke Sehel na kulia ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mbeya na Makamu Mwenyekeiti wa Chama hicho, Mhe. Victoria Nongwa.










Hakuna maoni:
Chapisha Maoni