- Wanawake kama viongozi timizeni wajibu wa kulinda amani, usawa katika jamii
- Asema kila Mtanzania ana haki ya kutambulika kwa jinsia yake
Na
HABIBA MBARUKU, Mahakama-Dodoma
Jaji
Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju amesema kuwa bila amani
hakuwezi kuwa na ustawi wa wananchi jambo ambalo litasababisha jamii kushindwa
kutekeleza shughuli zake za kila siku mfano kilimo na uvuvi.
Mhe.
Masaju aliyasema hayo jana 23 Oktoba, 2025 kwenye ukumbi wa mikutano wa Makao
Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma,wakati alipokuwa akifungua Mafunzo
kwa Waratibu wa Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA) huku
akiwataka Majaji na Mahakimu kama wanawake kama viongozi kutimiza wajibu wao wa
kulinda amani hasa wanawake wanaofanya kazi katika Mahakama kudumisha Utawala
wa Sheria.
“Hivyo bila kuwepo amani, hakuwezi kuwa na ustawi wa wananchi huwezi kwenda shambani, huwezi kwenda kulima, huwezi kwenda kuvua, huwezi kufunga ndoa, huwezi kwenda kwenye ibada huwezi kufanya hata na mambo ya uongozi, huwezi kufanya kazi, utafanyaje kazi wakati hakuna amani kwa hiyo wajibu wa wanawake katika kazi zenu na kama viongozi ni kusisitiza haya na hasa nyinyi wa Mahakamani ambao mna jukumu kubwa sana la kudumisha utawala wa sheria,” alisisitiza Jaji Mkuu.
Mhe.
Masaju alisema kuwa, amani ndio nguzo muhimu ya ustawi wa jamii na kuwataka
wanawake ambao ni viongozi kusisisitiza kuhusu amani katika kutekeleza majukumu
yao na hasa Mahakama ambayo ina jukumu kubwa la kudumisha utawala wa sheria.
Aidha,
Jaji Mkuu, alizungumzia msingi wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kwenye utawala,
amani, utulivu na usalama pamoja na vipengele vyake vikuu vinne ikiwa ni pamoja
na Utawala Bora na Haki, Serikali za mitaa imara zenye ufanisi pamoja na
vingine ambavyo vina mchango mkubwa katika kutunza na kuendeleza usalama na
ustawi wa Taifa.
Akizungumza
kuhusu suala la Utawala wa Sheria, Mhe. Masaju alisema kuwa, “Utawala wa Sheria
uliwekwa kwa sababu gani ni kutaka kushamirisha na kuhakikisha kwamba kunakuwa
na ustawi wa wananchi ili watu waweze kufanya shughuli zao za kisiasa, kiuchumi
na kijamii kwa amani na wakiwa huru lakini sizungumzii utawala wa sheria ambao
sisi tumeutaja katika Ibara ya 26 katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania.”
Katika
upande mwingine, Jaji Mkuu alieleza kuwa Serikali na Vyombo vyote vya Umma
vinatoa haki sawa kwa raia wote bila kujali rangi, kabila au dini ya mtu kama
inavyotambulika katika Ibara ya 12 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
kwamba binadamu wote huzaliwa huru na wote ni sawa.
“Vyombo
vyote vya umma vinatoa nafasi iliyo sawa kwa raia wote wake kwa waume bila
kujali rangi kabila, dini au hali ya mtu, kwa kuangalia mtu unasema huyu wa
dini fulani, sasa hiyo ni changamoto, kwa aina zote za dhuluma, vitisho,
ubaguzi, rushwa, uovu au upendeleo vinaondolewa nchini, kwamba matumizi ya
utajiri wa Taifa yanatilia mkazo maendeleo ya wananchi na hasa zaidi
yalielekezwa kwenye jitihada za kuondoa umasikini, ujinga na maradhi,” alisema
Mhe. Masaju.
Aliongeza
kuwa, kila Mtanzania ana haki ya kutambulika kwa jinsia yake, na kuthaminiwa
kupewa haki kama ilivyotajwa katika Ibara ya 12 (2) kwamba kila mtu anastahili
heshima ya kutambuliwa na kuthaminiwa utu wake.
“Mimi
naamini tunapaswa kutambua na kuthamini hizi jinsia zetu kwa jinsi
wanavyozaliwa anayezaliwa mwanaume ataitwa mwanaume, anayezaliwa mwanamke
ataitwa mwanamke, vinginevyo tutashindwa kupata haki iliyotajwa katika Ibara ya
12 kwa sababu binadamu wote tumezaliwa huru na wote ni sawa,” alisema Jaji Mkuu.
Aidha, Mhe. Masaju aliwasisitiza pia TAWJA kusimamia uhuru wao wa kufanya maamuzi na kwamba wawe huru kufanya kazi kwa kuzingatia Katiba na Sheria bila kuburuzwa na mtu yoyote ili kuendelea kujenga jamii yenye ustawi amani na usawa.
Wanachama wa Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA) wakimsikiliza Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju wakati wa hafla ya Ufunguzi wa Mafunzo kwa Waratibu wa Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA) jana tarehe 23 Oktoba, 2025 kwenye ukumbi wa mikutano wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.
Wanachama wa Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA) wakifuatilia hotuba ya Ufunguzi wa Mafunzo kwa Waratibu wa Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA) iliyokuwa ikitolewa na Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju (hayupo katika picha).
(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)












Hakuna maoni:
Chapisha Maoni