Ijumaa, 24 Oktoba 2025

TAWJA KUIMARISHA UONGOZI, HAKI ZA KIJINSIA KWA WARATIBU KIKANDA

      Yafanya mafunzo yazingatia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050

      Yadhamiria kuimarisha haki, usawa wa kijinsia nchini

Na HALIMA MNETE, Mahakama-Dodoma

Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA) jana tarehe 23 Oktoba 2025 kimeanza kufanya mafunzo maalum kwa Waratibu wa Kikanda wa chama hicho, ambayo yamelenga kuimarisha uongozi, usimamizi na uwajibikaji katika kulinda haki za kijinsia na za binadamu.

Mafunzo hayo yalifanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma, ambapo mgeni rasmi alikuwa Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mwenyekiti wa TAWJA ambaye pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Barke Sehel, alisema kuwa kufanyika kwa mafunzo hayo kuongeza uwezo wa Waratibu wa Mkoa katika uratibu, mawasiliano, na utekelezaji wa programu za kikanda.

“Tunatarajia kuwa kupitia waratibu hawa, TAWJA itaimarika na kuwa kinara katika ulinzi wa haki za binadamu na usawa wa kijinsia nchini,” alisema Mhe. Sehel.

Aliwataka washiriki wa mafunzo hayo kutumia fursa hiyo kujifunza, kubadilishana uzoefu na kuweka mikakati ya pamoja itakayosaidia kuboresha ushiriki wa wanawake katika uongozi, si tu ndani ya Mahakama bali pia katika jamii kwa ujumla.

Kwa mujibu wa Mhe. Sehel, TAWJA imejikita katika kupambana na unyanyasaji wa kijinsia kwa kutoa elimu, kuhamasisha jamii na kushirikiana na Taasisi mbalimbali ili kuhakikisha haki za wanawake na watoto zinalindwa.

Aliongeza kuwa, takwimu zinaonyesha mashauri ya unyanyasaji wa kijinsia bado ni changamoto nchini, jambo linalohitaji juhudi endelevu za wadau wote katika kutoa elimu na kufungua mashauri kwa wakati.

Mhe. Sehel alitumia nafasi hiyo kumshukuru Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania kwa kukubali mwaliko wa kuwa mgeni rasmi na kwa kuonyesha utayari wa kuunga mkono juhudi za chama katika kukuza nafasi ya mwanamke ndani ya mfumo wa Mahakama na jamii kwa ujumla.

Mafunzo hayo ya siku mbili yamefadhiliwa na Mahakama ya Tanzania kupitia ofisi ya Mtendaji Mkuu wa Mahakama, hatua inayodhihirisha ushirikiano mkubwa unaolenga kutimiza Ibara ya 9 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayosisitiza heshima ya utu, usawa wa binadamu na haki sawa kwa wote bila ubaguzi.

Mada mbalimbali zitawasilishwa kwenye mafunzo hayo ya siku mbili, ikiwemo Dhamira na Vipaumbele vya Kimkakati vya TAWJA, Uimarishaji wa Uanachama na Ushiriki wa Kikanda, Haki za Kijinsia na Uongozi, Ufuatiliaji na Tathmini, pamoja na Uhamasishaji wa Rasilimali na Uendelevu. Mada hizo zinalenga kuendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025/2050 inayohimiza utawala bora, amani, usalama, na fursa sawa kwa wote.


Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania na Mwenyekiti wa Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzani (TAWJA),  Mhe. Barke Sehel akitoa neno la utangulizi mbele ya Mgeni Rasmi Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju (hayupo katika picha) wakati wa hafla ya ufunguzi wa Mafunzo maalum kwa Waratibu wa Kikanda wa chama hicho jana tarehe 23 Oktoba, 2025 kwenye ukumbi wa mikutano wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.


Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju (katikati) akiwa kwenye hafla ya ufunguzi wa Mafunzo kwa Waratibu wa Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA) jana tarehe 23 Oktoba, 2025. Kushoto ni Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania na Mwenyekiti wa TAWJA, Mhe. Barke Sehel na kulia ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mbeya na Makamu Mwenyekiti wa Chama hicho, Mhe. Victoria Nongwa.


Wanachama wa Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA) wakifuatilia kinachojiri wakati wa hafla ya ufunguzi 
wa Mafunzo kwa Waratibu wa Chama hicho.

(Picha na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni