Jumanne, 3 Februari 2026

'DIRA YA MAENDELEO 2050 KICHOCHEO CHA HAKI NA MAENDELEO YA TAIFA NA MAHAKAMA'

Na AIDAN ROBERT, Mahakama-Kigoma

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Augustine Rwizile ameongoza watumishi na wadau wa Mahakama mkoani humo kusherehekea kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini katika viunga vya Mahakama hiyo.

Akizungumza katika hafla hiyo jana tarehe 02 Februari, 2026, Mhe. Rwizile alisema kuwa, Mahakama inayo malengo na mikakati inayoendana na kasi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 katika kuimarisha mifumo mbalimbali ya haki, maendeleo ya uchumi wa Taifa na kuboresha   utendaji kazi wa Mahakama.

“Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 imetoa fursa kwa wananchi wake kufanya kazi kwa uhuru, kuishi kwa mshikamano na utengamano katika kudumisha haki, amani na kuheshimiana. Dira hiyo pia imelenga wananchi wenye maarifa, ujuzi unaohitajika katika Karne ya 21 ya Sayansi na Teknolojia ili waweze kushiriki kikamilifu shughuli za maendeleo kwa makundi yote ya Wazee, Wanawake, Vijana, watu wenye ulemavu na makundi yote maalum, Dira hiyo imewapa nafasi,” alisema Jaji Rwizile.

Jaji Rwizile alisema kuwa, Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050, imesimamia misingi mikuu mitano ambayo ni Demokrasia, Haki na Uhuru, Amani na Umoja kama msingi wa maendeleo ambapo Mahakama huchukua jukumu kubwa la kutatua migogoro inayotokana na misingi hiyo katika maisha ya kila siku.

Aidha, aliongeza kwa kusema kwamba, “Dira hiyo inatathmini na kulinda muungano wetu, ambao ni tunu ya Taifa na watu wote kuheshimiana na kuchangia katika kufanikisha malengo ya pamoja ya Kitaifa, vilevile utajiri na rasilimali za nchi zitumike kikamilifu rasilimali zake kwa manufaa ya Taifa na ustawi wa wananchi wake, kwamba rasilimali tulizonazo zinapaswa kulindwa ili zitunufaishe wote kwa pamoja na msingi wa mwisho ni Utamaduni na Maadili ya Taifa ambapo Dira hiyo inatuhimiza kuhifadhi utamaduni uliopo kulinda, kukuza maadili na utamaduni chanya unaotutambulisha Kitaifa kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.”

Mhe. Rwizile aliongeza kuwa, Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 imeonesha kuwa, miaka 25 ijayo  Tanzania itakuwa na Mahakama zenye hadhi na kuheshimika Dunia nzima, ili kufikia hilo lazima Mahakama itende haki bila kuona hali ya mtu kiuchumi, katika jamii, kutochelewesha haki bila sababu za msingi, kutoa fidia stahiki kwa watu waliofanyiwa makosa na watu wengine kwa mujibu wa sheria iliyotungwa na Bunge, kukuza usuluhishi kwa migogoro inayoletwa Mahakamani, kutenda haki bila kufungwa na masharti ya kiufundi katika utoaji haki.

Kwa upande wake Wakili wa Serikali, Bw. George Kalenda alisema kuwa, Kaulimbiu ya Siku ya Sheria ya mwaka huu isemayo, ‘Mchango wa Mahakama katika Ustawi na Maendeleo ya Taifa,’’ inazitaka Taasisi zinazosimamia haki kujipanga kutekeleza malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050 kwa kushirikiana kwa pamoja ili kuisaidia Mahakama kutenda haki na kutoa mchango wa Mahakama katika ustawi na maendeleo ya Taifa.

“Tunatakiwa kuwajibika katika shughuli zetu za kila siku ili kufikia malengo yetu jumuishi katika kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo katika ustawi wa Taifa, Utawala wa Sheria, kutenda haki, kuheshimu haki za binadamu, uhuru wa Mahakama, weledi na uadilifu katika kusimamia haki Mahakamani,” alisema Bw. Kalenda.

Naye, Mwenyekiti wa Jukwaa la Mawakili wa Kujitegemea, Bw. Eliutha Kivyiro alisema kuwa, malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo  2050 ni pamoja na kukuza Taifa jumuishi lenye ustawi wa haki na linalojitegemea, hivyo, Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) ni Taasisi muhimu katika kufikia malengo ya Dira hiyo katika kuisaidia Mahakama kutenda haki mapema ipasavyo.

Aliongeza kuwa, ili kufikia malengo ya Mahakama ya kuchangia ustawi na maendeleo ya Taifa ameshauri kuimarisha uwezo wa Wanataaluma na Taasisi katika utatuzi wa migogoro kwa njia zote ikiwemo usuluhishi, “Aidha Mahakama inatoa mwongozo wa kisheria katika vyombo vingine ili kuendenda katika misingi ya sheria ili kuleta ustawi wa Taifa na maendeleo ya wananchi, inapotoa haki kwa wakati bila kupoteza muda kwa namna yoyote.”

Wadau waliohudhuria Maadhimisho ya Kilele cha Siku ya Sheria nchini ni pamoja na Watumishi wa Kanda hiyo, Mawakili wa Serikali, Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS), Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa, Viongozi wa Dini, Wakuu wa Taasisi za Umma, Chuo cha Mafunzo Kigoma (KTC), Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Mlole,  Wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Wavulana Kigoma, wananchi kutoka sehemu mbalimbali ya Mkoa wa Kigoma, Ubalozi mdogo wa Burundi na wengine. 


Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma,  Mhe. Augustine Rwizile akitoa hotuba wakati wa hafla ya Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini kwa mwaka 2026 iliyofanyika katika viwanja vya Mahakama Kuu Kigoma tarehe 02 Februari, 2026.

Wakili Mfawidhi wa Serikali, Bw. George Kalenda akitoa salamu katika hafla ya Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini iliyofanyika jana tarehe 02 Februari, 2026 katika viwanja vya  Mahakama Kuu Kigoma.

Mwenyekiti wa Jukwaa la Mawakili wa Kujitegemea Tanganyika (TLS), Bw. Eliutha Kivyiro akitoa salamu zake wakati wa hafla ya Kilele cha Siku ya Sheria nchini iliyofanyika katika viunga vya Mahakama Kuu Kigoma.


Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. John Francis Nkwabi akikagua  kikosi maalum cha Askari wa (FFU) wakati wa sherehe za  Siku ya Sheria nchini ikiwa ni ishara ya ufunguzi rasmi wa shughuli za Mahakama kwa mwaka huu.


Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma,  Mhe. Augustine Karichuba Rwizile (kulia), Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe. John Nkwabi (katikati) na Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe. Projestus Kahyoza (kushoto), watumishi wengine wa Mahakama na Wadau wakiwa pamoja na Mgeni wa Heshima Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Kigoma ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Buhigwe, Mhe. Michael Ngayalina (nyuma ya Jaji Mfawidhi) katika maandamano ya Maadhimisho ya Siku ya Sheria Nchini. 

Picha ya pamoja katikati ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma,  Mhe. Augustine Rwizile, wa pili kushoto ni Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe. John Nkwabi, wa pili kulia ni Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe. Projestus Kahyoza, wa kwanza kushoto ni Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Kigoma ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Buhigwe, Mhe. Michael Ngayalina na wa kwanza kulia ni Wakili Mkuu wa Serikali Mfawidhi, Bw. George Kalenda.

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni