Jumanne, 3 Februari 2026

MAHAKAMA KATAVI YAPONGEZWA KWA KUBORESHA MIUNDO MBINU YA UTOAJI HAKI

Na. Ally A. Ramadhani – Mahakama Katavi

Mkuu wa Wilaya ya Mpanda Mhe. Bi Jamila Yusufu Kimaro jana tarehe 2 Februari, 2026 alikuwa Mgeni Maalumu akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mhe. Mwanamvua Hoza Mlindoko na kuhutubia katika Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini na kuipongeza Mahakama kwa kuanzisha miradi mbalimbali ya ujenzi na miundo mbinu ya Mahakama inayoendelea Mkoani Katavi.

Mhe. Bi. Kimaro aliitaja miradi mbalimbali inyoendelea mkoani Katavimfano, Vituo vya Mahakama za Mwanzo kama vile Mamba, Sibwesa, Ugalla na Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Katavi ambavyo kwa wastani ujenzi unaendelea kukamilika.

Aidha, Mkuu huyo wa Wilaya ya Mpanda alisema “kukamilika kwa miradi yote ya ujenzi wa Mahakama inayoendelea mkoani Katavi itasaidia kwa kiwango kikubwa hasa kwa upande wa gharama za wananchi kutumia umbali mrefu kutoka eneo moja kwenda jingine akitolea mfano; kutoka Katavi kwenda Sumbawanga kwa ajili ya kusikiliza mashauri yao yanayoendelea Mahakama Kuu, pia kupunguza mashauri ya mlundikano (Backlog) pamoja na muda wa kumaliza mashauri kupungua”.

Kwa upande wake, Wakili wa kujitegemea Bw. Lutende Masinde akihutubia kwa niaba ya Mwenyekiti wa chama cha Mawakili Tanganyika Mkoa wa Katavi Bi. Sekela Amulike aliongeza kuwa, “Kutokana na kauli mbiu ya mwaka huu inayosema Mchango wa Mahakama katika Ustawi na Maendeleo ya Taifa, Mahakama inawajibu wa kulinda Haki na Wajibu kwa wananchi, hii itasaidia kutatua migogoro miongoni mwa wananchi, hivyo kuongeza uzalishaji kwa Taifa,” aliongeza Bw. Masinde.

Kama ilivyo Moja ya nguzo katika Mpango Mkakati wa Mahakama ya Tanzania ni utoaji haki kwa wakati. Mahakama inatekeleza mpango huo kwa kuboresha mazingira ya utoaji haki na kusogeza huduma za utoaji haki karibu zaidi na wananchi kwa kujenga miundombinu bora na wezeshi itakayochangia ufanisi mzuri wa utekelezaji wa nguzo hiyo.

Mkuu wa Wilaya ya Mpanda Mhe. Bi Jamila Yusufu Kimaro, ambaye ni Mgeni Maalum kwenye Maadhimisho ya siku ya Sheria nchini 2026 alipokuwa akiwahutubia wananchi na wadau mbalimbali wa Mahakama mkoani Katavi.

Sehemu ya Watumishi wa Mahakama mkoani Katavi wakitoa burudani kwenye Sherehe za Maadhimisho ya Siku ya Sheria Nchini

Hakimu Mfawidhi Mahakama ya Hakimu Mkazi Katavi Mhe. Gway K. Sumaye na Mgeni Rasmi wa Sherehe za Maadhimishi ya Siku ya Sheria nchini akitoa hotuba ya siku hiyo.

(Habari Hii Imehaririwa na Innocent Kansha-Mahakama)




Hakuna maoni:

Chapisha Maoni