Jumanne, 3 Februari 2026

JAJI MANYANDA ATOA RAI KWA WANANCHI KUSHIRIKI KATIKA UJENZI WA MAHAKAMA

Na.  Fredrick Mahava-Mahakama, Sumbawanga

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Sumbawanga Mhe. Fredrick Kapela Manyanda ameongoza watumishi na wadau wa Mahakama kusherehekea kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini katika viwanja vya Mahakama Kuu Sumbawanga ikiwa ni ishara ya kuanza kwa mwaka mpya wa shughuli za kimahakama.

Akizungumza katika hafla hiyo jana tarehe 02 Februari, 2026, Mhe. Manyanda alitoa rai kwa wananchi Mkoa wa Rukwa kwa kushirikiana na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kushiriki katika ujenzi wa Mahakama hasa Mahakama za Mwanzo  kama Muze, Ilemba, Kate, WampembeKipande  ambazo hazina majengo ya Mahakama na zinaendesha shughuli zake kwenye ofisi za Kata na Maghala ya kijiji.

Mhe. Manyanda alisema Kauli mbiu  ya mwaka 2026 inasema “Mchango wa Mahakama katika ustawi na maendeleo ya Taifa” inatukumbusha na kutuonyesha kuwa, ili Taifa liweze kusonga mbele kimaendeleo, Mahakama pia inayo nafasi ya kushiriki katika kuhakikisha hilo linafanikiwa na hivyo taifa linahitaji kuwa na Mahakama iliyo imara, huru na yenye kusimamia haki kwa mujibu wa mamlaka iliyopewa na Katiba.

Vilevile, Mhe. Manyanda amehimiza matumizi ya usuluhishi katika ngazi mbalimbali kwa lengo la kutatua migogoro mapema zaidi na kwa njia ambayo haithiri mahusiano ya wadaawa na hivyo kusaidia kujenga jamii yenye amani na kusisitiza juu ya matumizi ya mifumo mbalimbali kuanzia ngazi ya familia hadi Mahakama kuhakikisha kuwa migogoro inayoweza kutatuliwa kwa usuluhishi itatuliwe kwa njia hiyo.

Kwa upande wake, Mwanasheria Mkuu wa serikali, Bw. Mjahidi B. Kamugisha alisema kuwa, Mahakama kama mlezi wa Katiba, Mlinzi wa haki za binadamu na utawala wa sheria ni nguzo muhimu katika kukuza na kuendeleza ustawi na maendeleo ya Taifa. Mahakama iliyo huru na yenye kuheshimika na kuaminika huhakikisha utekelezaji thabiti wa mikataba, ulindaji wa haki za mali na kudhibiti matumizi  mabaya ya madaraka ili kukuza imani ya wawekezaji hivyo kuwezesha ukuaji imara na endelevu wa uchumi wa Taifa.

Aliongeza kuwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Taifa ya Mashitaka na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali zitaendelea kushirikiana na Mahakama katika kuhakikisha watu wote wanapata huduma kwa weledi ubora, uadilifu ili kiu ya kila anayekimbilia haki ikatimiekwa wakati.

 Kwa upande wake, Wakili kutoka Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) Bi, Tunu Mahundi alisema kuwa, kwa sasa TLS inahudumia wananchi mbalimbali wanaohitaji huduma za Msaada wa Kisheria kwa wenye uhitaji na kuhakikisha wananchi wasio na uwezo wa kumudu gharama za mawakili wanapata haki bila vikwazo katika ofisi zake zilizopo kwenye chapter 21 Tanzania nzima.

Vilevilie, aliipongeza Mahakama kwa kuendelea kuboresha Mifumo ya TEHAMA ambayo imewawezesha Mawakili kuweza kufanya shughuli zao mahali popote kwa kupitia mfumo wa e-Filing na Virtual court na pia TLS itaendelea kushiriki katika matukio mbalimbali yanayohusu utoaji elimu ya sheria kama vile wiki ya sheria, maonyesho ya sabasaba na kampeni ya msaada wa kisheria (Samia legal Aids)

Naye, Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Bw. Makongoro Nyerere aliwashukuru na kuwapongeza Viongozi wa Mahakama Kanda ya Sumbawanga kwa Maandalizi mazuri ya Siku ya Sheria nchini na kuipongeza Mahakama kwa kuwa mstari wa mbele katika kutimiza Dira ya maendeleo ya Taifa na kuhimiza umuhimu wa wananchi kujitokeza kujenga Mahakama ili kusogeza huduma kwa Wananchi

Wadau waliohudhuria Maadhimisho ya kilele cha Siku ya Sheria nchini ni pamoja na Watumishi wa Kanda ya Sumbawanga, Mawakili wa Serikali, Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS), Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Rukwa, Viongozi wa Dini, Wakuu wa Taasisi za Umma, TAKUKURU, Madalali wa Mahakama na Wasambaza Nyaraka za Mahakama na wananchi kutoka sehemu mbalimbali ya Mkoa wa Rukwa.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Sumbawanga Mhe. Fredrick Kapela Manyanda akiwahutubia wadau wa Mahakama na wananchi mbalimbali waoshiriki katika kilele cha maadhimisho ya siku ya sheria nchini jana tarehe 2 Februari, 2026.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Sumbawanga Mhe. Fredrick Kapela Manyanda akikagua gwaride maalum la uzinduzi wa siku ya sheria nchini.

Mwakilishi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mkoa wa Rukwa Bw Mjahidi B. Kamugisha akitoa hotuba yake ya Siku ya Sheria Nchini kwa Mwaka 2026 mbele ya Wananchi na wadau waliohudhuria katika viwanja vya Mahakama Kuu Sumbawanga.

Mwakilishi wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) Bi.Tunu Mahundi  akisoma hotuba  yake ya Siku ya Sheria Nchini kwa Mwaka 2026 mbele ya Wananchi na wadau waliohudhuria katika viwanja vya Mahakama Kuu Sumbawanga.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Sumbawanga Mhe. Fredrick K. Manyanda (Katikati), Mkuu wa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhe, Makongoro Nyerere (Kushoto) na Katibu Tawala na Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya Mhe, Masinga (kulia) wakiwa kwenye picha ya pamoja na Mahakimu 

Wakuu wa Taasisi mbalimbali, Viongozi wa Dini wakisiliza hotuba kutoka kwa Jaji mfawidhi, TLS na Mwakilishi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

(Habari Hii Imehariri na Innocent Kansha - Mahakama)


 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni