Na ABDALLAH SALUM, Mahakama-Njombe
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe na Mgeni Rasmi wa Maadhimisho ya Siku ya Sheria Nchini mkoani humo, Mhe. Liadi Chamshama amesema hali ya mashauri imepungua kwa asilimia 85 ukilinganisha na miaka ya nyuma hali iliyotokana na kujiwekea Mpango Mkakati wa kuyamaliza mashauri kwa wakati kuanzia Mahakama za Mwanzo.
Mhe. Chamshama alibainisha hayo katika Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini tarehe 02 Februari, 2026 wakati akizungumza na wageni waalikwa pamoja na wadau wa Mahakama walioshiriki katika sherehe hizo.
Mhe.Chamshama aligusia Dira ya Mahakama isemayo; 'Haki Sawa kwa Wote Mapema Ipasavyo,' na kusema kuwa, “Mahakama ikiwa ni mojawapo ya Mhimili wa Dola imekuwa ikitoa haki kwa wote bila kujali hali ya mtu kijamii au kiuchumi, kutochelewesha haki bila sababu ya msingi, kutenda haki bila kufungwa kupita kiasi na masharti ya kiufundi hivyo kutoa haki kwa wakati ili kuiwezesha jamii kushiriki kikamilifu katika shunghuli za kiuchumi kwa lengo la kujiongezea kipato cha mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla kwa kufanya hivyo, Mahakama ina mchango mkubwa wa kukuza ustawi na maendeleo ya Taifa kiujumla.”
Kwa upande wake Mtendaji wa Mahakama ya Hakimu
Mkazi Njombe, Bw. Richard Mbambe akizungumza wakati wa Maadhimisho hayo, aliwakaribisha wananchi na wadau wa Mahakama
waliofika katika viwanja vya Jengo la Mahakama ya Hakimu Mkazi jombe
huku akiwajuza juu ya Kauli Mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu 2026 isemayo; 'Mchango wa
Mahakama katika Ustawi na Maendeleo ya Taifa'.
Naye, Wakili wa Serikali, Mhe. Elise James alieleza kuwa, Mahakama ni Uti wa Mgongo wa Taifa kwa kuwa Dunia yote kwa sasa ipo katika vita vya Kiuchumi wa Kijiografia na ya kisiasa kwa kuwa, kila Nchi inachukua hatua za makusudi kutumia nguvu ya kisiasa au kiuchumi ama rasilimali za asili kama vile hali ya hewa ya eneo kuhusiana na nchi nyingine katika kukuza na kuendeleza uchumi na kuleta maendeleo ya Taifa lake.
"Vilevile
kumekuwepo na ushaidi wa kufunguliwa kwa miradi mikubwa hapa nchini katika
sekta mbalimbali ikiwemo uchukuzi, ujenzi, nishati, madini na huduma za jamii na
kadhalika hii ni ishara kuwa Serikali yetu kwa kushirikiana na Mhimili wa
Mahakama na Bunge ni kuweka mazingira rafiki ya kuanzisha uwekezaji na hivyo
kukuza uchumi na maendeleo ya Nchi yetu," alisema Wakili James.
Katika hatua nyingine, Kiongozi wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) Mkoa wa Njombe, Bw. Innocent Kibadu alizungumzia kuhusu Kaulimbiu ya mwaka huu katika Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini isemayo, 'Mchango wa Mahakama katika Ustawi na Maendeleo ya Taifa.'
Aliendelea kusema kuwa, "hakuna maendeleo ya kweli bila ulinzi wa haki, Utawala wa Sheria na Misingi ya Utawala Bora na Mahakama ni moja ya Mhimili kati ya Mihimili mitatu ya Dola ambayo imeundwa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhimili huu unatupa mwelekeo wa haki, uaminivu na utulivu wa Taifa pamoja na kuwepo na maslahi ya wananchi pasipo kuwepo upendeleo na kuleta matumaini kwa wananchi katika ustawi wa kiuchumi na maendeleo ya Taifa kiujumla."
Naye Mgeni Mahsusi Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Njombe, Mhe. Joseph Rutashubilwa aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Njombe alisema kuwa, Serikali ya awamu hii imeweza kutambua mchango mkubwa unaoendelea kutolewa na Mahakama na kuendelea kusisitiza utekelezaji wa majukumu kwa kuzingatia falsafa ya kazi na utu kwa Mahakama na wadau wote wa Mahakama wana nafasi ya msingi ya kuhakikisha haki inatendeka kwa wakati na kwa uwazi.
Mhe. Rutashubilwa aliwaeleza wananchi kuwa, kwa kuzingatia utu wa mwananchi, Mkoa wa Njombe unathamini na kutambua Mhimili wa Mahakama na Taasisi zote za Haki Jinai kwa kuwa na ushirikiano na mshikamano kwani ni nguzo muhimu. Pamoja na hayo aliwataka wananchi wote watumie fursa ya Siku ya Sheria kujifunza masuala ya Kisheria.
Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe, Mhe. Liadi Chamshama akihutubia mbele ya wananchi (hawapo katika picha) wakati wa hafla ya Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini. Nyuma yake ni kulia ni Mgeni Mahsusi Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Njombe, Mhe. Joseph Rutashubirwa pamoja na Viongozi wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa wa Njombe.
Sehemu ya Mahakimu, Mawakili wa Serikali, Mawakili wa Kujitengemea, Watumishi na wananchi wakisikiliza hotuba zilizotolewa na Viongozi wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini.
Mgeni rasmi ambaye ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe, Mhe.Liadi Chamshama (wa pili kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya Njombe, Mhe. Matilda Kayombo (kulia), kushoto ni Mgeni Mahsusi Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Njombe, Mhe.Joseph Rutashubirwa wakati wa hafla ya Maadhimisho ya Siku ya Sheria Nchini tarehe 02 Februari, 2026.
Mtendaji wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe, Bw. Richard Mbambe akizungumza wakati Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini mkoani humo.
Mgeni Mahsusi Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Njombe, Mhe. Joseph Rutashubirwa Mhe. Joseph Rutashubirwa akihutubia mbele ya wananchi (hawapo katika picha) wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini tarehe 02 Februari, 2026.
Kwaya ya Watumishi wa Mahakama Mkoa wa Njombe wakiburudisha kwa kuimba nyimbo maalum waliyoitunga inayohusu Haki na Utawala Bora.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni