Jumanne, 3 Februari 2026

MAHAKAMA KUU KANDA YA SIMIYU YAADHIMISHA SIKU YA SHERIA NCHINI, 2026

 ·       Jaji Mfawidhi asisitiza mwisho wa matumizi ya karatasi katika uendeshaji wa mashauri

Na NAUMI SHEKILINDI, Mahakama-Simiyu

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Simiyu, Mhe Wilbert Chuma amewaongoza watumishi wa Kanda hiyo na WanaSimiyu katika kuadhimisha Siku ya Sheria nchini 2026.

Mhe. Chuma ambaye alikuwa Mgeni rasmi katika sherehe za Maadhimisho ya Siku ya Sheria mkoani humo aliambatana na Mgeni Maalum Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anamringi Macha KATIKA sherehe hizo zilizofanyika tarehe 02 Februari, 2026 katika viwanja vya Mahakama Kuu Kanda ya Simiyu.

Akizungumzia kuhusu Kauli Mbiu ya Siku ya sheria nchini, 2026 isemayo; ‘Mchango wa Mahakama katika ustawi na maendeleo ya Taifa’ Jaji Mfawidhi alisema kuwa, Kauli Mbiu hiyo ina dhamira ya kutambulisha kwa umma nafasi ya Mahakama katika kuleta maendeleo na ustawi wa Taifa na kudhihirisha kuwa haki na maendeleo havitengani.

Mhe. Chuma alisisitiza kuwa, haki inapopatikana kwa wananchi kwa uwazi na kwa kufuata misingi ya sheria hujenga imani kwa Taasisi za Haki na kuweka mazingira bora ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Aidha, Mhe. Chuma alizungumzia juu ya matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ili kuepukana na matumizi ya karatasi na kusema kuwa, “huduma za Mahakama kwa njia ya mtandao zimeimarishwa, hatua iliyosaidia kusogeza haki karibu zaidi na wananchi bila gharama kubwa za usafiri.”

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anamringi Macha alisisitiza watumishi wa Mahakama kuwa na uadilifu, weledi na uwajibikaji ili kuweza kutoa haki kwa wananchi.

Naye Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Simiyu, Mhe. Elimo Massawe aliongoza wadau kwa ajili ya kwenda kusikiliza shauri la jinai la kwanza kusikilizwa katika Mahakama Kuu Kanda ya Simiyu.

 

Hotuba nyingine zilitolewa na Viongozi kutoka Ofisi ya Mwendesha Mashtaka na Ofisi ya Mawakili wa Kujitegemea wote wakisisitiza kwamba Mahakama ndio nguzo ya maendeleo na maendeleo ndio azma ya Serikali ili kuleta ustawi na haki kwa jamii, vilevile walieleza kuwa, ustawi wa maendeleo ni matokeo ya Mihimili yote mitatu yaani Mahakama, Serikali Kuu na Bunge.

Maadhimisho hayo yalihudhuriwa na watumishi pamoja na wadau kutoka Taasisi mbalimbali wakiwemo Wadau kutoka Ofisi ya Mwendesha Mashtaka, Mawakili wa Kujitegemea,Taasisi ya Kuzui ana Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), PSSSF, NHIF, TRA, Polisi, Uhamiaji na wananchi kwa ujumla.


Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Simiyu, Mhe.Wilbert Chuma akihutubia watumishi na wadau waliohudhuria sherehe za Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini tarehe 02 Februari, 2026.

   Sehemu ya Wadau wa Mahakama waliohudhuria sherehe za Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini wakiwa katika viwanja vya Mahakama Kuu Simiyu.

Meza Kuu ikiongozwa na Mgeni Rasmi Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Simiyu, Mhe. Wilbert Chuma (katikati) wakiwa katika picha ya pamoja na 
watumishi wa Mahakama Kuu Simiyu. Wa pili kulia ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Simiyu, Mhe. Elimo Massawe, wa kwanza kulia ni Mkuu wa Mashtaka Mkoa wa Simiyu, Mhe. Kainunula, wa pili kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anamringi Macha pamoja na wa kwanza kushoto ni Wakili wa Kujitegemea, Wakili Sabini.

Kwaya ya Watumishi wa Mahakama Kuu Kanda ya Simiyu wakitumbuiza mbele ya Mgeni Rasmi wakati wa sherehe za Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini.
   Gwaride tayari kwa ajili ya kukaguliuwa na Jaji Mfawidhi Mhe. Wilbert Chuma kuashiria ufunguzi wa mwaka mpya wa Kimahakama kwa mwaka 2026.


(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni