Jumanne, 3 Februari 2026

JAJI MFAWIDHI MAHAKAMA KUU KANDA YA TABORA AONGOZA MAADHIMISHO YA SIKU YA SHERIA NCHINI

Na AMANI MTINANGI, Mahakama-Tabora

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora, Mhe. Dkt. Adam Mambi ameongoza sherehe za Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini yaliyofanyika katika viwanja vya Mahakama Kuu Kanda ya Tabora tukio ambalo limeashiria mwanzo rasmi wa shughuli za Mahakama kwa mwaka huu, 2026. 

Maadhimisho hayo yalianza kwa Viongozi wa Dini mbalimbali kufanya sala maalum, wakiombea amani na Mahakama kutekeleza vizuri jukumu la utoaji wa haki nchini.

Akihutubia wananchi, Wadau wa Sheria na Watumishi wa Mahakama waliojitokeza kwa wingi, Jaji Mfawidhi alisema Mahakama itaendelea kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia misingi ya sheria, haki na utu wa mwanadamu ili kuendelea kuchangia katika ustawi na maendeleo ya Taifa.

Kwa kutambua ukweli kuwa Mahakama ina nafasi kubwa katika kuchochea ustawi na maendeleo ya Taifa, tutahakikisha Mahakama inaendelea kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia misingi ya sheria, haki na utu wa mwanadamu,” alisema Mhe. Dkt. Mambi.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Mhe. Upendo Wella ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya Tabora aliipongeza Mahakama Kuu Kanda ya Tabora kwa kuimarisha ushirikiano na wadau wake muhimu katika mnyororo wa utoaji haki na hivyo kufanya jukumu zima la utoaji haki kufanyika kwa ufanisi mkubwa.

Mhe. Wella ameahidi kwamba, Serikali itaendelea kushirikiana na Mhimili wa Mahakama katika kuhakikisha wananchi wanapata haki kwa wakati na kwa gharama nafuu.

“Mahakama katika Kanda ya Tabora imeendelea kuimarisha ushirikiano na wadau wake muhimu katika mnyororo mzima wa utoaji haki na hivyo kufanya jukumu zima la utoaji haki kufanyika kwa ufanisi mkubwa. Napenda kuwaahidi kwamba, Serikali itaendelea kutoa ushirikiano kwa Mahakama kama ambavyo imeendelea kutoa ili kuhakikisha Mahakama inatekeleza majukumu yake kwa ufanisi,” alisisitiza Mwakilishi huyo wa Mkuu wa Mkoa wa Tabora.

Naye Wakili wa Serikali wa Mkoa wa Tabora kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali,  Carson Nkya akihutubia katika hafla hiyo, alieleza kuwa Kaulimbiu ya mwaka huu inaonesha Mahakama inachangia ustawi na maendeleo ya Taifa kwa kuchochea ukuaji wa uchumi na uwekezaji, kulinda Utawala wa Sheria na amani ya kijamii, kuimarisha uwajibikaji na uwazi pamoja na kuhakikisha upatikanaji wa haki kwa wote na kulinda haki za msingi za binadamu.

“Mahakama inatoa mchango mkubwa katika ustawi na maendeleo ya Taifa kwa kuwa kichocheo cha ukuaji wa uchumi na uwekezaji kupitia utekelezaji wa kisheria wa mikataba, ulinzi wa haki za mali na utatuzi wa migogoro kwa wakati. Mahakama inahakikisha utawala wa sheria na utulivu wa kijamii kwa kusimamia mgawanyo wa madaraka, kudhibiti matumizi mabaya ya madaraka ya Serikali, kulinda haki za msingi za binadamu na kudumisha amani katika jamii. Aidha, Mahakama inakuza uwajibikaji na kuzuia rushwa kwa kuhakikisha uwazi na utii wa sheria katika utekelezaji wa sera na maamuzi ya Serikali," alisema Wakili Nkya.

Aliongeza kuwa, Mahakama inawezesha maendeleo ya binadamu na jamii kwa kuhakikisha upatikanaji wa haki kwa wote, ikiwemo makundi yaliyo katika mazingira magumu pamoja na kutekeleza misingi ya kimataifa ya haki za binadamu na biashara, hivyo kuchangia maendeleo endelevu ya Taifa.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Mawakili Tanganyika Mkoa wa Tabora,  Wakili Kelvin Kayaga alitambua na kupongeza jitihada kubwa zinazofanywa na Mahakama Kuu Kanda ya Tabora kwa kufanya kazi kwa kiwango cha juu cha taaluma, weledi na nidhamu ya kazi.

Ni vema tukatambua na kupongeza jitihada kubwa zinazofanywa na Mahakama Kuu - Kanda ya Tabora, Kanda yetu imeendelea kuonesha kiwango cha juu cha taaluma, weledi na nidhamu ya kazi.” alisema Wakili Kayaga.

Maadhimisho hayo yalipambwa na burudani mbalimbali ikiwemo Kikundi cha JKT Msange, Kikundi cha Ngoma za Asili cha Uaridi na Igizo lililoandaliwa na Wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Tabora.

Baada ya shughuli za Maadhimisho kukamilika, shauri la kwanza la mwaka wa Mahakama lilisikilizwa ikiwa ni ishara rasmi ya kuanza kwa shughuli za kimahakama kwa mwaka huu.

Maadhimisho ya Siku ya Sheria hufanyika kila mwaka nchini na hutumika kama jukwaa la kutafakari mchango wa Mahakama katika kujenga jamii yenye haki, amani na utawala wa sheria.


Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora, Mhe. Dkt. Adam Mambi akihutubia wananchi katika viwanja vya Mahakama Kuu Kanda ya Tabora kwenye Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini tarehe 02 Februari, 2026.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora, Mhe. Dkt. Adam Mambi  akikagua Gwaride la Heshima lililoandaliwa kuashiria kufunguliwa kwa rasmi kwa shughuli za Mahakama.

Watumishi wa Mahakama Tabora wakisakata rumba wakati wa sherehe za Maadhimisho ya Siku ya Sheria Nchini tarehe 02 Februari, 2026.


Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa, Mhe. Upendo Wella ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Tabora akitoa salamu kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora wakati wa sherehe za Maadhimisho ya Siku ya Sheria tarehe 02 Februari, 2026.

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni