Na EMMANUEL OGUDA, Mahakama-Shinyanga
Mahakama ya Tanzania imekuwa na inaendelea kushiriki katika kutoa
mchango mkubwa katika kuimarisha uchumi wa Nchi kupitia usikilizwaji wa
mashauri ya kimkakati yanayohusu kodi, benki, ardhi na uwekezaji ambapo kwa
upande wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga ilisikiliza na kumaliza
mashauri 84 kati ya 92 yaliyokuwepo katika Mahakama hiyo.
Hayo yalibainishwa tarehe 02 Februari, 2026 na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga, Mhe. John Kahyoza wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini ambayo kwa Kanda hiyo yaliadhimishwa katika viwanja vya Mahakama Kuu Shinyanga.
“Kwa upande wa Mahakama Kuu Kanda Shinyanga, tulikuwa na mashauri ya aina hiyo 92, yaliyoanza kusikilizwa kuanzia mwezi Oktoba hadi Desemba, 2025, tulikuwa tumesikiliza mashauri 84 na kubakiwa na mashauri nane tu hivyo kufanya Kanda yetu kutoa mchango katika maendeleo ya Taifa kwa kukwamua fedha zilizokuwa zimekwama Mahakamani kutokana na uwepo wa mashauri ya kikodi na uwekezaji,’’ alisema Mhe.Kahyoza.
Aidha, Jaji Kahyoza alisema kuwa, Mahakama itaendelea kutoa mchango katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ambayo inalenga kuwa na Taifa lenye ustawi wa Haki hivyo, mchango wa Mahakama katika kufanikisha adhma hiyo unahitajika ili Taifa liwe na uchumi imara zaidi, jumuishi na shindani, uwezo wa watu wake pamoja na uhifadhi wa mazingira.
“Tunatarajia kufikia mwaka 2050, tutaendelea kuwa na Taifa lenye kuheshimu Utawala Bora, Taifa lenye amani, usalama na tulivu na Mahakama lazima tutimize lengo letu la utoaji wa haki mapema ipasavyo na kwa watu wote kuchochea maendeleo ya Taifa na kupunguza gharama na muda wa kutatua migogoro,’’ Jaji Mfawidhi huyo.
Naye Wakili wa Serikali Mfawidhi Mkoa wa Shinyanga, Bw. Lameck Merumbe alisema kuwa, ustawi wa Taifa lolote Duniani ni matokeo ya Mihimili yote mitatu kwa maana ya Serikali, Bunge na Mahakama kushirikiana pamoja, kwa upande wa Mahakama ina jukumu la kikatiba la kutafsiri sheria hivyo kuweka mazingira wezeshi ya kisheria na utekelezaji bora wa Sera za kitaifa.
Aidha, Bw. Merumbe alibainisha kuwa, Mahakama huru inahakikisha usawa, haki na maendeleo ya nchi kwakuwa Mahakama ni kichocheo cha ukuaji wa uchumi ambapo Mhimili huo huhakikisha Mikataba ya kibiashara inatekelezwa hivyo kusaidia Wawekezaji kuwa na Imani na uwekezaji wao sambamba na uwepo wa mifumo thabiti ya utatuzi wa migogoro.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) Mkoa wa Shinyanga, Wakili Shaban Mvungi alisema kuwa, Taifa linapokuwa na mfumo mzuri wa utoaji haki nchini, ustawi wa kiuchumi, kijamii na kisiasa huimarika, Mahakama ina jukumu la kulinda haki za msingi za wananchi kwa kutoa maamuzi huru bila upendeleo pamoja na kujenga mazingira rafiki kwa wawekezaji sambamba na kukuza shughuli za kiuchumi.
Maadhimisho ya Siku ya Sheria Nchini kwa upande wa Shinyanga yalihudhuriwa
na wadau mbalimbali wa Mahakama wakiwemo Watumishi wa Mahakama, wanafunzi
kutoka shule mbalimbali pamoja na wananchi.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga, Mhe. John Kahyoza akisisiza jambo wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini yaliyofanyika katika viwanja vya Mahakama Kuu Shinyanga.
Mwenyekiti wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) Mkoa wa Shinyanga, Wakili Shaban Mvungi akiwasilisha salamu za Chama hicho wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini iliyoadhimishwa tarehe 02 Februari, 2026 katika viwanja vya Mahakama Kuu Shinyanga.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya
Shinyanga Mhe. John Kahyoza akikagua Gwaride maalum lililoandaliwa kuashiria
kuanza kwa mwaka mpya wa Mahakama, 2026.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga, Mhe. John Kahyoza akiwa tayari kwa ukaguzi wa Gwaride maalum kuashiria uzinduzi wa Mahakama mpya wa shughuli za Kimahakama kwenye Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini yaliyofanyika tarehe 02 Februari, 2026. Waliosimama nyuma ni Majaji, Mawakili na sehemu ya Wadau wengine wa Mahakama Kanda ya Shinyanga.
Kikundi cha Burudani cha Sungusungu kutoka Kata ya
Mwamalili kikitoa burudani wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Sheria tarehe 02
Februari, 2026 katika viwanja vya Mahakama Kuu Shinyanga.
Sehemu ya Watumishi wa Mahakama Kanda ya Shinyanga wakiwa katika Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini tarehe 02 Februari, 2026 Mahakama Kuu Shinyanga.
(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni