Na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma
Jaji Mkuu wa Mahakama ya
Tanzania, Mhe. George Masaju leo tarehe 03 Februari, 2026 ametembelewa na
kufanya mazungumzo na Rais wa Mahakama ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EACJ), Mhe.
Nestor Kayobera.
Akizungumzia kuhusu lengo
la kumtembelea Jaji Mkuu ofisini kwake Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania
jijini Dodoma, Mhe. Kayobera amesema lengo mojawapo ni kumsalimia na kumpongeza kwa kuteuliwa kuwa Jaji Mkuu wa Tanzania
tangu Juni, 2025.
Aidha, Rais huyo wa EACJ
amesema kuwa, anafurahishwa na ushirikiano ambao Mahakama hiyo inapata kutoka Serikali ya
Tanzania na Mahakama kwa ujumla na kukiri kuwa, mazingira yaliyopo ya amani
yanawawezesha kutekeleza majukumu yao kwa amani na utulivu.
Kadhalika, Mhe. Kayobera
amemueleza Jaji Mkuu kwamba, katika kuhakikisha kuwa, Mahakama hiyo inaendelea
kufanya kazi ipasavyo na kwa diplomasia, tangu alipoingia katika Mahakama hiyo
mwaka 2021 aliweka Falsafa tatu muhimu ikiwa ni pamoja na Kufanya kazi kwa pamoja (Teamwork) ambapo amesema kuwa, Mahakama ni Taasisi ya pamoja na si ya mtu
mmoja, hivyo ushirikiano wa Majaji na wadau wengine ni muhimu na huchochea
ufanisi, uwajibikaji na utoaji haki kwa wakati.
Ametaja Falsafa nyingine
kuwa ni Kutekeleza majukumu kwa nia njema (Good Faith) na kwamba tafsiri na
utekelezaji wa Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ufanyike kwa uaminifu ili
kuepuka mbinu za kukwepa haki kwa ujanja wa kisheria.
Rais huyo wa Mahakama ya
Jumuiya Afrika Mashariki ameongeza kuwa, Falsafa nyingine anayotumia ni kuzingatia Diplomasia ya Kimahakama (Judicial Diplomacy) lengo likiwa
ni kudumisha mahusiano mazuri na Taasisi za Jumuiya na Nchi Wanachama, Kutoa
maamuzi yenye nguvu kisheria lakini kwa lugha na mtazamo unaojenga ujumuishaji,
si kuvunja wala kuyumbisha uhuru wa Mahakama, bali kusawazisha haki na uhai wa
Jumuiya.
Vilevile, Mhe. Kayobera amemshukuru Jaji Mkuu kufuatia Mahakama hiyo kupatiwa Ofisi kwa ajili ya Masjala ndogo ya Mahakama hiyo iliyopo ndani ya Jengo la Makao Makuu ya Mahakama jijini Dodoma.
Kwa upande wake Jaji Mkuu amemuhakikishia Rais huyo wa EACJ kuwa, Mahakama ya Tanzania itaendelea kutoa ushirikiano wa dhati katika utendaji kazi wake na kujenga mahusiano mazuri ya Mahakama hiyo na Mahakama ya Tanzania.
Mhe. Masaju ameonesha na kukiri kufurahishwa na ujio wa Mhe. Kayobera aliyeambatana na Jaji Kiongozi wa Mahakama ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Mhe. Yohane Masara, Msaidizi wa Rais wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Wakili Nina Sokoine na Afisa Masjala Mkuu wa Mahakama hiyo-Masjala Ndogo ya EACJ Dodoma, Wakili Mennas Mafwere na kuwaeleza kuwa wasisite kufanya mawasiliano wakati wowote wanapopata changamoto.
Kadhalika Jaji Mkuu ameikaribisha Mahakama hiyo kuja Mahakama ya Tanzania kufanyia vikao vyake kama ambavyo imefanya na kuendelea kufanya katika baadhi ya Nchi nyingine za Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju (kulia) akiwa katika picha ya pamoja na Rais wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EACJ), Mhe. Nestor Kayobera alipomtembelea Jaji Mkuu tarehe 03 Februari, 2026 ofisini kwake Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.
Rais wa Mahakama ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EACJ), Mhe. Nestor Kayobera (kulia) akisaini kitabu cha wageni leo tarehe 03 Februari, 2026 alipowasili ofisini kwa Jaji Mkuu wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma. Kushoto ni Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju na katikati ni Jaji Kiongozi wa Mahakama ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Mhe. Yohane Masara.
Jaji Kiongozi wa Mahakama ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Mhe. Yohane Masara akisaini kitabu cha wageni leo tarehe 03 Februari, 2026 alipowasili ofisini kwa Jaji Mkuu Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.
Mazungumzo yakiendelea. Wa kwanza kushoto ni Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju , wa kwanza kulia ni Rais wa Mahakama ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EACJ), Mhe. Nestor Kayobera, wa pili kushoto ni Jaji Kiongozi wa Mahakama ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EACJ), Mhe. Yohane Masara na wa pili kulia ni Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Kiaki Nkya.


Sehemu ya Watumishi wa Mahakama ya Tanzania na Mahakama ya Jumuiya ya Afrika Mashariki wakifuatilia mazungumzo kati ya Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe.George Masaju na Rais wa Mahakama ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EACJ), Mhe. Nestor Kayobera yaliyofanyika ofisini kwa Jaji Mkuu Makao Makuu ya Mahakama jijini Dodoma. Kutoka kushoto ni Msaidizi wa Rais wa Mahakama ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EACJ), Wakili Nina Sokoine, anayefuata ni Afisa Masjala Mkuu wa Mahakama hiyo-Masjala Ndogo ya EACJ Dodoma, Wakili Mennas Mafwere, Naibu Msajili wa Mahakama na Katibu wa Jaji Mkuu, Mhe. Venance Mlingi na Katibu Msaidizi wa Jaji Mkuu, Mhe. Clarence Mhoja.

Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe.George Masaju na Rais wa Mahakama ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EACJ), Mhe. Nestor Kayobera (hayupo katika picha).
Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe.George Masaju (kulia) akimpatia Jarida na Kalenda za Mahakama Rais wa Mahakama ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EACJ), Mhe. Nestor Kayobera alipomtembelea Jaji Mkuu tarehe 03 Februari, 2026 ofisini kwake Makao Makuu ya Mahakama jijini Dodoma.
Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe.George Masaju (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Rais wa Mahakama ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EACJ), Mhe. Nestor Kayobera (kushoto) pamoja na Jaji Kiongozi wa Mahakama ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Mhe. Yohane Masara alipomtembelea Jaji Mkuu tarehe 03 Februari, 2026 ofisini kwake Makao Makuu ya Mahakama jijini Dodoma.
Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe.George Masaju (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Rais wa Mahakama ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EACJ), Mhe. Nestor Kayobera (wa tatu kushoto), Jaji Kiongozi wa Mahakama ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Mhe. Yohane Masara (wa pili kulia), Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Kiaki Nkya, Naibu Msajili na Katibu wa Jaji Mkuu, Mhe. Venance Mlingi (wa kwanza kushoto), Msaidizi wa Rais wa Mahakama ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EACJ), Wakili Nina Sokoine pamoja na Afisa Masjala Mkuu wa Mahakama hiyo-Masjala Ndogo ya EACJ Dodoma, Wakili Mennas Mafwere.
(Picha na MARY GWERA, Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni