Na AMANI MTINANGI, Mahakama-Tabora
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora, Mhe. Dkt. Adam Mambi ameongoza sherehe za Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini yaliyofanyika katika viwanja vya Mahakama Kuu Kanda ya Tabora tukio ambalo limeashiria mwanzo rasmi wa shughuli za Mahakama kwa mwaka huu, 2026.
Maadhimisho hayo yalianza kwa Viongozi wa Dini
mbalimbali kufanya sala maalum, wakiombea amani na Mahakama kutekeleza vizuri jukumu la utoaji wa haki nchini.
Akihutubia wananchi, Wadau wa Sheria na Watumishi
wa Mahakama waliojitokeza kwa wingi, Jaji Mfawidhi alisema Mahakama itaendelea
kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia misingi ya sheria, haki na utu wa
mwanadamu ili kuendelea kuchangia
katika ustawi na
maendeleo ya Taifa.
“Kwa kutambua
ukweli kuwa Mahakama
ina nafasi kubwa katika kuchochea ustawi na maendeleo ya Taifa, tutahakikisha
Mahakama
inaendelea
kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia misingi ya sheria, haki na utu wa
mwanadamu,” alisema Mhe. Dkt. Mambi.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Mhe. Upendo Wella ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya Tabora aliipongeza Mahakama Kuu Kanda ya Tabora kwa kuimarisha ushirikiano na wadau wake muhimu katika mnyororo wa utoaji haki na hivyo kufanya jukumu zima la utoaji haki kufanyika kwa ufanisi mkubwa.
Mhe. Wella ameahidi kwamba, Serikali itaendelea kushirikiana na Mhimili
wa Mahakama katika kuhakikisha wananchi wanapata haki kwa wakati na kwa gharama
nafuu.
“Mahakama katika Kanda
ya Tabora imeendelea kuimarisha ushirikiano na wadau wake muhimu katika
mnyororo mzima wa utoaji haki na hivyo kufanya jukumu zima la utoaji haki
kufanyika kwa ufanisi mkubwa. Napenda kuwaahidi kwamba, Serikali itaendelea
kutoa ushirikiano kwa Mahakama kama ambavyo imeendelea kutoa ili kuhakikisha
Mahakama inatekeleza majukumu yake kwa ufanisi,” alisisitiza Mwakilishi huyo wa Mkuu wa Mkoa wa Tabora.
Naye Wakili wa Serikali wa Mkoa wa Tabora kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Carson Nkya akihutubia katika hafla hiyo, alieleza kuwa Kaulimbiu ya mwaka huu inaonesha Mahakama inachangia ustawi na maendeleo ya Taifa kwa kuchochea ukuaji wa uchumi na uwekezaji, kulinda Utawala wa Sheria na amani ya kijamii, kuimarisha uwajibikaji na uwazi pamoja na kuhakikisha upatikanaji wa haki kwa wote na kulinda haki za msingi za binadamu.
“Mahakama inatoa mchango mkubwa katika ustawi na maendeleo ya Taifa kwa kuwa kichocheo cha ukuaji wa uchumi na uwekezaji kupitia utekelezaji wa kisheria wa mikataba, ulinzi wa haki za mali na utatuzi wa migogoro kwa wakati. Mahakama inahakikisha utawala wa sheria na utulivu wa kijamii kwa kusimamia mgawanyo wa madaraka, kudhibiti matumizi mabaya ya madaraka ya Serikali, kulinda haki za msingi za binadamu na kudumisha amani katika jamii. Aidha, Mahakama inakuza uwajibikaji na kuzuia rushwa kwa kuhakikisha uwazi na utii wa sheria katika utekelezaji wa sera na maamuzi ya Serikali," alisema Wakili Nkya.
Aliongeza kuwa, Mahakama inawezesha maendeleo ya
binadamu na jamii kwa kuhakikisha upatikanaji wa haki kwa wote, ikiwemo makundi
yaliyo katika mazingira magumu pamoja na kutekeleza misingi ya kimataifa ya
haki za binadamu na biashara, hivyo kuchangia maendeleo endelevu ya Taifa.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Mawakili Tanganyika Mkoa wa Tabora, Wakili Kelvin Kayaga alitambua na kupongeza jitihada kubwa zinazofanywa na Mahakama Kuu Kanda ya Tabora kwa kufanya kazi kwa kiwango cha juu cha taaluma, weledi na nidhamu ya kazi.
“Ni
vema tukatambua na kupongeza jitihada kubwa zinazofanywa na Mahakama Kuu -
Kanda ya Tabora, Kanda yetu imeendelea kuonesha kiwango cha juu cha taaluma,
weledi na nidhamu ya kazi.” alisema Wakili Kayaga.
Maadhimisho hayo yalipambwa na burudani
mbalimbali ikiwemo Kikundi cha JKT Msange, Kikundi cha Ngoma za Asili cha
Uaridi na Igizo lililoandaliwa na Wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana
Tabora.
Baada ya shughuli za Maadhimisho kukamilika,
shauri la kwanza la mwaka wa Mahakama lilisikilizwa ikiwa ni ishara rasmi ya
kuanza kwa shughuli za kimahakama kwa mwaka huu.
Maadhimisho ya Siku ya Sheria hufanyika kila
mwaka nchini na hutumika kama jukwaa la kutafakari mchango wa Mahakama katika
kujenga jamii yenye haki, amani na utawala wa sheria.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora, Mhe. Dkt. Adam Mambi akihutubia wananchi katika viwanja vya Mahakama Kuu Kanda ya Tabora kwenye Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini tarehe 02 Februari, 2026.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora, Mhe. Dkt. Adam Mambi akikagua Gwaride la Heshima
lililoandaliwa kuashiria kufunguliwa kwa rasmi kwa shughuli za Mahakama.
Watumishi wa Mahakama Tabora wakisakata rumba wakati wa sherehe za Maadhimisho ya Siku ya Sheria Nchini tarehe 02 Februari, 2026.




Hakuna maoni:
Chapisha Maoni