Jumanne, 13 Oktoba 2026

IDARA YA TEHAMA KATAVI YAUPIGA MWINGI

Na CHIMPAE MSELE – Mahakama, Katavi

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Katavi, Mhe. Godfrey Ntemi Isaya, ameipongeza Idara ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ya Mahakama Kuu Katavi kwa kuandaa mfumo wa kielektroniki wa kuhifadhi kumbukumbu za mirathi unaojulikana kama e-Mirathi Archive System (MAS).

Pongezi hizo zimetolewa tarehe 9 Oktoba, 2026 katika Ukumbi wa Mafunzo uliopo ndani ya jengo la Mahakama Kuu Katavi, wakati wa uzinduzi wa mfumo huo. Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Isaya ameipongeza Idara ya TEHAMA kwa kufanya kazi kwa weledi na kuanzisha mfumo unaolenga kurahisisha utunzaji na upatikanaji wa nyaraka za mirathi.

Amesema mfumo huo utasaidia kuharakisha upatikanaji wa haki mapema ipasavyo, kupunguza usumbufu unaojitokeza katika utafutaji wa kumbukumbu za mirathi, hususan katika Mahakama za Mwanzo mkoani Katavi.

Aidha, Mhe. Isaya ameonesha kuridhishwa na ubunifu huo wa kuandaa mfumo e-Mirathi Archive System uliofanywa na watumishi wa Idara ya TEHAMA kwa juhudi na kazi kubwa waliyoifanya. Akieleza kuwa utakuwa na mchango muhimu katika kuboresha utendaji wa shughuli za Mahakama.

Mhe. Isaya amebainisha kuwa mfumo huo utasaidia kupunguza changamoto zinazowakabili yatima, wajane na wagane katika kufuatilia masuala ya mirathi, kwa kuwezesha kumbukumbu kupatikana kwa haraka pale zinapohitajika. Hatua hiyo itasaidia kupunguza muda wa kusubiri nyaraka na kuondoa baadhi ya usumbufu ambao umekuwa ukijitokeza katika usimamizi wa mashauri ya mirathi.

Katika hatua nyingine, amewataka Mahakimu kuhakikisha kuwa mashauri yote ya mirathi yaliyofunguliwa hapo awali katika Mahakama wanazosimamia yanaingizwa kwenye mfumo huo. Amesisitiza kuwa kufanya hivyo kutasaidia kuboresha usimamizi wa mashauri na kupunguza ucheleweshaji wa utoaji wa haki katika masuala ya mirathi.

Kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa, mfumo wa e-Mirathi Archive System (MAS) umeandaliwa kuhifadhi kumbukumbu mbalimbali za mashauri ya mirathi, ikiwemo mienendo ya mashauri, nakala za hukumu, maamuzi na amri za Mahakama. Pia, mfumo huo utahifadhi vielelezo, taarifa za wasimamizi wa mirathi, wadhamini na wanufaika wa mirathi.

Vilevile, mfumo huo una uwezo wa kutuma ujumbe mfupi wa maandishi (SMS) kwa wasimamizi na wanufaika wa mirathi ili kuwakumbusha kuhusu hatua muhimu za mashauri yao, ikiwemo muda wa kufunga shauri la mirathi unapokaribia au unapofika.

Jaji Isaya amesema mfumo huo una manufaa makubwa kwa wanufaika wa mirathi, wasimamizi wa mirathi na watendaji wa Mahakama, kwa kuwa utasaidia kuhifadhi taarifa sahihi, kuimarisha usalama wa kumbukumbu na kupunguza uwezekano wa watu wasiohusika kujiingiza katika mashauri ya mirathi kwa lengo la kujipatia manufaa yasiyostahili. Amesema matumizi ya mfumo huo yanatarajiwa kuongeza ufanisi katika usimamizi wa mashauri ya mirathi na kuchangia utoaji wa haki kwa wakati, ikilinganishwa na changamoto zilizokuwepo awali.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala ndogo Katavi, Mhe. Godfrey Ntemi Isaya akizindua mfumo wa kielektroniki wa e-Mirathi Archive System (e-MAS)

Hakimu Mkazi Mwandamizi Mhe. Jackson Ryoba Irondo akitoa shukulani kwa uongozi Mahakama Katavi baada ya kupata mafuzo ya mfumo wa kielektroniki wa e-Mirathi Arhive System (e-MAS)

Muonekano wa ndani wa Mfumo wa e-Mirathi Archieve System (e-MAS)

Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Katavi, Mhe Godfrey Ntemi Isaya (katikati), Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Katavi Mhe. Silvia Lushasi, (kushoto) kulia ni Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo Katavi Bw. Epaphras Tenganamba wakiwa kwenye picha ya pamoja na Mahakimu pamoja na wataalam wa Idara ya TEHAMA.

(Habari Hii Imehaririwa na Innocent Kansha & James Busanya - Mahakama)


MAHAKAMA KUU SUMBAWANGA YATOA ELIMU YA SHERIA KWA WANAFUNZI WA VETA

Na SHARIFU MOKIWA – Mahakama, Sumbawanga

Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Sumbawanga, imetoa elimu ya sheria kwa wanafunzi wa Chuo cha Ufundi Stadi na Huduma Mkoa wa Rukwa (RVTSC), lengo ni kuwaongezea uelewa kuhusu mifumo ya utoaji haki, majukumu ya vyombo vya kisheria, muundo wa Serikali Kuu na mchakato wa uchaguzi nchini Tanzania.

Mafunzo hayo yamefanyika Oktoba 8, 2026, katika Chuo hicho kilichopo Mtaa wa Eden B, Barabara ya Kashai, mjini Sumbawanga, Mkoa wa Rukwa, yalitolewa na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Sumbawanga Mhe. Pamela Mazengo akishirikiana na Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Rukwa Mhe. Victor Thomas Bigambo pamoja na Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mwanzo Sumbawanga Mjini Mhe. Yusuph Daud Sakara.

Akiwasilisha mada kuhusu mifumo ya usimamizi na utoaji haki nchini Tanzania, Mhe. Sakara alieleza majukumu ya vyombo mbalimbali vinavyohusika katika utoaji haki, vikiwemo Mahakama, Mabaraza ya ardhi, Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA), Jeshi la Polisi, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (NPS), pamoja na vyombo vingine vinavyoshiriki katika mchakato wa usimamizi wa sheria.

Pia alisisitiza umuhimu wa kufahamu mamlaka na majukumu ya kila chombo ili kuwawezesha wananchi kutambua sehemu sahihi ya kuwasilisha malalamiko au migogoro yao kulingana na aina ya suala husika na matakwa ya kisheria.

Kwa upande wake, Mhe. Mazengo aliwasilisha mada kuhusu Tume ya Utumishi wa Mahakama, akieleza maana ya Tume hiyo inavyotekeleza majukumu yake, muundo wake na utaratibu za kuwasilisha malalamiko.

Aidha, alieleza kuhusu Kamati za maadili kwa Maafisa Mahakama katika ngazi za Wilaya na Mkoa, akibainisha muundo wake, majukumu na taratibu za kuwasilisha malalamiko yanayohusu maadili ya Maafisa hao.

Naye, Mhe. Bigambo aliwaelimisha wanafunzi hao, kuhusu muundo wa Serikali Kuu kwa mujibu wa Katiba na namna inavyotekeleza majukumu yake. Pia alizungumzia kuhusu mchakato wa uchaguzi Mkuu nchini Tanzania, kuanzia uandikishaji wa wapiga kura, kipindi cha uchaguzi hadi hatua zinazofuata baada ya uchaguzi, pamoja na haki ya wananchi kushiriki katika uchaguzi kwa mujibu wa sheria.

Mafunzo hayo yalihitimishwa kwa kipindi cha maswali na majibu, ambapo wanafunzi walipata fursa ya kuuliza maswali na kupata ufafanuzi kutoka kwa wataalamu hao wa Mahakama kuhusu masuala mbalimbali ya kisheria.

Akizungumza baada ya mafunzo hayo, Kaimu Mkuu wa Idara ya Mafunzo wa Chuo hicho, Bi. Furaha Mgalla, alisema kuwa, mafunzo hayo yamewasaidia wanafunzi kupata uelewa wa masuala ya sheria kutoka kwa wataalamu hao, pamoja na kupata nafasi ya kuuliza maswali na kufafanuliwa masuala ambayo awali hawakuwa na uelewa nayo wa kutosha.

Bi. Mgalla aliongeza kuwa mafunzo hayo yamewasaidia wanafunzi kujiandaa kwa mtihani wa somo la Life Skills, unaotarajiwa kuanza Oktoba 26, 2026, sambamba na mitihani mingine.

Mafunzo hayo yamekua yakitolewa na Mahakama ya Tanzania kwa wananachi ni sehemu ya juhudi za kuimarisha elimu ya sheria kwa jamii na kuongeza uelewa wa vijana kuhusu haki, wajibu na taratibu za kisheria, huku yakichangia kuimarisha ushirikiano kati ya Mahakama na Taasisi za Elimu.

Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Sumbawanga Mhe. Pamela Mazengo (kushoto), Hakimu Mkazi Mahakama ya Mwanzo Sumbawanga Mjini, Mhe. Yusuph Daud Sakara (katikati) na Hakimu Mkazi Mkuu, Mahakama ya Hakimu Mkazi Rukwa Mhe. Victor Bigambo kwa pamoja wakifanya utambulisho kabla ya kuaza kutoa elimu ya sheria kwa wanafunzi wa Chuo cha Ufundi Stadi na Huduma Mkoa wa Rukwa (RVTSC).

Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Sumbawanga Mhe. Pamela Mazengo (wa tatu kushoto), Hakimu Mkazi Mahakama ya Mwanzo Sumbawanga Mjini, Mhe. Yusuph Daud Sakara (katikati) na Hakimu Mkazi Mkuu, Mahakama ya Hakimu Mkazi Rukwa Mhe. Victor Bigambo (wa pili kushoto) wakiwa kwenye picha ya pamoja na Wananfunzi hao.

Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Sumbawanga Mhe. Pamela Mazengo (aliyesimama) akitoa mada kuhusu Majukumu ya Tume ya Utumishi wa Mahakama.

Hakimu Mkazi Mahakama ya Mwanzo Sumbawanga Mjini, Mhe. Yusuph Daud Sakara akifundisha Mada ya Mifumo ya usimamizi na utoaji haki pamoja na Mamlaka za utoaji haki nchini Tanzania.

Hakimu Mkazi Mkuu, Mahakama ya Hakimu Mkazi Rukwa Mhe. Victor Bigambo akitoa Mada ya Muundo wa Serikali Kuu na mchakato wa kisheria wa Uchaguzi Tanzania 

Wanafunzi wa Chuo cha Ufundi Stadi na Huduma Mkoa wa Rukwa (RVTSC), wakifatilia kwa makini mafunzo hayo yakitolewa na maofisa Mahakama chuoni hapo.

Mwanafunzi akiuliza maswali kupata ufafanuzi kutoka kwa wataalamu hao kutoka mahakamani. 

Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Sumbawanga Mhe. Pamela Mazengo wakati akitoa Mada ya  Tume ya Utumishi wa Mahakama.

(Habari Hii Imehaririwa na Innocent Kansha & James Busanya - Mahakama)


MAHAKAMA KUU NJOMBE YAFANYA MAFUNZO YA UTOAJI NA UTEKELEZAJI WA ADHABU MBADALA

  • Yalenga kuwajengea uwezo Mahakimu, Wadau wa Haki Jinai kuhusu Utoaji na Utekelezaji wa Amri za Uangalizi na Huduma kwa Jamii

Na ABDALLAH SALUM, Mahakama-Njombe

Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Njombe imeendesha mafunzo kuhusu utoaji na utekelezaji wa adhabu mbadala, zikiwemo amri za uangalizi na huduma kwa jamii lengo likiwa ni kuwajengea uwezo Mahakimu na Wadau wa mfumo wa Haki Jinai kuhusu matumizi sahihi ya adhabu hizo kwa mujibu wa sheria.

Mafunzo hayo yalifanyika tarehe hivi karibuni na kuhudhuriwa na Mahakimu wa ngazi zote wakiwemo wa Wilaya za mbali walioshiriki kwa njia ya mtandao. Washiriki wengine walikuwa Mawakili wa Serikali, Maofisa wa Jeshi la Magereza na wadau wengine wa mfumo wa Haki Jinai.

Mafunzo hayo yaliratibiwa na Hakimu Mkazi na Msaidizi wa Sheria wa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Njombe, Mhe. Elisha Mwasomola na kutolewa na Wataalam kutoka Makao Makuu ya Wizara ya Mambo ya Ndani, Kitengo cha Huduma za Uangalizi na Huduma kwa Jamii jijini Dodoma.

Akizungumza wakati wa akitoa neno la utangulizi katika mafunzo hayo, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Njombe, Mhe. Joseph Luambano alisema kuwa, matumizi sahihi ya Adhabu Mbadala yanaweza kusaidia kupunguza msongamano wa wafungwa na mahabusu magerezani, pamoja na kupunguza gharama za uendeshaji kwa Serikali.

Alieleza pia kuwa, adhabu hizo zina nafasi muhimu katika kumrekebisha mkosaji bila kumuweka gerezani, pale ambapo sheria inaruhusu, huku akizingatia masharti yaliyowekwa na Mahakama.

Mhe. Luambano alisema kuwa, mafunzo hayo yameandaliwa kufuatia ukaguzi uliofanywa hivi karibuni na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Njombe, Mhe. Victoria Nongwa, ambao ulibaini maeneo yaliyohitaji kupewa kipaumbele katika kuboresha utoaji na utekelezaji wa Adhabu Mbadala.

Akifungua mafunzo hayo, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Victoria Nongwa alisema kuwa, kufuatia ukaguzi alioufanya katika Mahakama za Mmwanzo hivi karibuni, eneo la utoaji na utekelezaji wa amri za uangalizi na huduma kwa jamii ni miongoni mwa maeneo yenye changamoto za utekelezaji miongoni mwa Mahakimu.

Kwa sababu hiyo, aliona ipo haja ya kuandaa mafunzo hayo kwa haraka ili kuongeza uelewa kwa Mahakimu na wadau wa mfumo wa haki jinai kuhusu sheria na taratibu zinazopaswa kufuatwa katika utoaji wa amri hizo.

Mhe. Nongwa alieleza pia, umuhimu wa adhabu mbadala kuwa ni kusaidia kupunguza gharama kwa Serikali katika kuwatunza wafungwa Magerezani, kurudisha mamlaka ya urekebu kwa jamii, kulinda utu wa mkosaji na kuwezesha mkosaji kurekebisha mwenendo wake huku akihudumia familia yake.

Aidha, ameeleza kuwa, aliona umuhimu wa kuwashirikisha wataalamu kutoka Kitengo cha Uangalizi na Huduma kwa Jamii ambao, kwa kiasi kikubwa, wanahusika moja kwa moja katika eneo hili la usimamizi wa amri hizo.

Kwa sababu hiyo, Mhe. Nongwa aliwasisitiza washiriki kushiriki kikamilifu katika mafunzo hayo kwa kutoa mawazo yao, kuuliza maswali na kuelezea uzoefu wao katika eneo hilo.

“Ni imani yangu kuwa, baada ya mafunzo haya, sio tu kwamba matumizi ya adhabu mbadala yataongezeka, bali pia taratibu na michakato yote ya utoaji na utekelezaji wa adhabu hizo mbadala itazingatiwa kikamilifu. Ili kufanikisha hilo, nawaomba mshiriki kikamilifu mafunzo haya kwa kutoa mawazo na maoni yenu, kuuliza maswali na kuchangia kwa namna inayofaa, hususan wakati wa majadiliano,” alisema Mhe. Nongwa.

Katika mafunzo hayo, Afisa Uangalizi Mkuu na mmoja wa Wawezeshaji, Bw. Samweli Kabunga alitoa mada kuhusu utaratibu wa kisheria unaoongoza utoaji na utekelezaji wa amri ya huduma kwa jamii katika mfumo wa utoaji haki, hususan kwa makosa ambayo sheria inaruhusu mhusika kupewa adhabu mbadala badala ya kifungo gerezani.

Alifafanua kuwa, amri ya huduma kwa jamii inayotolewa kama adhabu mbadala kwa kuongozwa na Sheria ya Huduma kwa Jamii, sura ya 291, pamoja na Kanuni zake, humwezesha mkosaji kubaki katika jamii na kutekeleza kazi zenye manufaa kwa jamii kama njia ya kutumikia adhabu aliyopewa na Mahakama kwa kipindi kilichoamriwa na Mahakama.

Akifafanua zaidi juu ya mambo muhimu kuhusiana na amri ya huduma kwa jamii, Bw. Kabunga alieleza kuwa, amri hiyo inaweza kutolewa moja kwa moja mahakamani kwa kuzingatia masharti ya kifungu cha 3 cha Sheria ya Huduma kwa Jamii au kutolewa na Mahakama kwa mchakato kuanzia gerezani baada ya mkosaji kuhukumiwa kifungo gerezani kwa kuzingatia masharti ya kifungu cha 52 cha Sheria ya Magereza, sura ya 58.

Sambamba na hayo, Bw. Kabunga alisema kuwa kabla ya kutolewa kwa amri ya huduma kwa jamii yapo mambo kadhaa ambayo Mahakama inapaswa kujiridhisha nayo ikiwa ni pamoja na: ukomo wa adhabu iliyowekwa kisheria (kifungo kisichozidi miaka minne); uwepo wa mkosaji mahakamani; ridhaa ya mkosaji; uwepo wa mikakati ya kutosha ya utekelezaji wa amri; uwepo wa ripoti ya Ofisa Huduma kwa Jamii inayoonesha kuwa mkosaji anaweza kutoa huduma kwa jamii; na kadhalika.

Matumizi sahihi ya amri ya huduma kwa jamii, kwa maneno ya Bw. Kabunga, yanaweza kusaidia kupunguza msongamano magerezani, kumuwezesha mkosaji kurekebisha tabia na kuendelea kushiriki katika shughuli za kijamii huku akiwajibika kwa kosa alilolitenda.

Naye Afisa Uangalizi Mwandamizi, Bw. Deogratius Shirima aliwasilisha mada kuhusu masharti ya kisheria yanayohusu utoaji na utekelezaji wa amri za uangalizi na makundi ya wahalifu wanaoweza kuwekwa chini ya uangalizi huo. Alieleza kuwa, tathmini ya mkosaji haipaswi kuzingatia kosa alilolitenda pekee, bali pia mazingira yake binafsi na kijamii, huku mambo yanayoweza kuzingatiwa yakiwa ni pamoja na umri, tabia, hali ya afya ya akili na mazingira mengine yanayoweza kuwa na umuhimu katika kutoa uamuzi unaofaa kwa mujibu wa sheria.

Bw. Shirima alielezea amri ya uangalizi kwa kufafanua kuwa, mhalifu anayepewa adhabu hiyo anaachwa kwenye jamii na kuwekwa chini ya uangalizi na usimamizi wa Ofisa Uangalizi kwa kipindi kisichopungua mwaka mmoja na kisichozidi miaka mitatu kwa kuzingatia masharti ya kifungu cha 4 cha Sheria ya Uangalizi wa wakosaji (sura ya 247) pamoja na kanuni zake.

Kwa sababu hiyo, Bw. Shirima alifafanua kuwa, ni muhimu kwa Ofisa Uangalizi kuchunguza mazingira ya mkosaji kabla ya kutoa mapendekezo kwa Mahakama kuhusu adhabu inayofaa na kwa upande wa Mahakama ni muhimu kuchunguza mapendekezo ya Ofisa Uchunguzi kabla ya kuamua kutoa amri ya uangalizi kwa mkosaji.

Kwa upande wake, Afisa Uangalizi Mkuu, Bi. Sheroline Mzava aliwasilisha mada kuhusu Taarifa ya Uchunguzi wa Kijamii (TUK) na kuelezea umuhimu wake katika kuisaidia Mahakama kufanya uamuzi sahihi unaozingatia mazingira ya mkosaji na shauri linalosikilizwa wakati wa kutoa adhabu kwa mkosaji.

 Alisema kuwa, taarifa hiyo hujumuisha uchunguzi wa historia ya mkosaji, mwenendo wake wa maisha, mazingira ya kifamilia na kijamii, pamoja na mambo mengine yanayoweza kusaidia Mahakama kutathmini adhabu inayofaa.

Bi. Sheroline aliongeza kuwa, taarifa ya uchunguzi wa kijamii humuwezesha Ofisa Uangalizi kutoa tathmini na mapendekezo yanayoweza kuisaidia Mahakama kufanya uamuzi unaozingatia sheria, mazingira ya shauri husika na uwezekano wa mkosaji kurekebisha mwenendo wake ili asirudie tena kosa.

Kwa upande mwingine, Washiriki wa mafunzo hayo walipata fursa ya kujadili changamoto zinazoweza kujitokeza katika utoaji na utekelezaji wa amri za uangalizi na huduma kwa jamii, pamoja na kubadilishana uzoefu kuhusu namna ya kuimarisha ushirikiano kati ya Mahakama na wadau wengine wa mfumo wa haki jinai.

Mafunzo hayo yanatarajiwa kuimarisha uelewa wa pamoja miongoni mwa washiriki kuhusu matumizi sahihi ya adhabu mbadala, kwa kuzingatia sheria, mazingira ya kila shauri na maslahi mapana ya jamii, ili kuchangia utoaji haki wenye ufanisi.

Ofisa Uangalizi Mwandamizi, Bw. Deogratius Shirima akiwasilisha mada kuhusu masharti ya kisheria yanayohusu Utoaji na Utekelezaji wa Amri za Uangalizi wakati wa Mafunzo kuhusu utoaji na utekelezaji wa adhabu mbadala yaliyofanyika hivi karibuni Mahakama Kuu Njombe. Wengine walioketi ni Mahakimu, Mawakili wa Serikali, Maofisa wa Jeshi la Magereza na Wadau wengine wa mfumo wa Haki Jinai.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Njombe, Mhe. Victoria Nongwa (aliyeketi katikati) pamoja na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Njombe, Mhe. Joseph Luambano (kushoto) na Ofisa Uangalizi Mkuu, Bi. Sheroline Mzava wakimsikiliza kwa makini Mratibu wa Mafunzo kuhusu Utoaji na Utekelezaji wa Adhabu Mbadala ambaye ni Hakimu Mkazi na Msaidizi wa Sheria wa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Njombe, Mhe. Elisha Mwasomola (hayupo katika picha).

Hakimu Mkazi na Msaidizi wa Sheria wa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Njombe, Mhe. Elisha Mwasomola akiendelea na uratibu wa mafunzo hayo.

Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Njombe, Mhe. Joseph Luambano (aliyesimama) akitoa neno la utangulizi wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya Utoaji na Utekelezaji wa Adhabu Mbadala. Wanaoonekana pembeni ni sehemu ya Wataalam kutoka Makao Makuu ya Wizara ya Mambo ya Ndani, Kitengo cha Huduma za Uangalizi na Huduma kwa Jamii kutoka jijini Dodoma.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Njombe, Mhe. Victoria Nongwa akifungua mafunzo ya Utoaji na Utekelezaji wa Adhabu Mbadala.

Ofisa Uangalizi Mkuu, Bw. Samwel Kabunga akitoa mada kuhusu Utaratibu wa kisheria wa Adhabu mbadala (Huduma kwa Jamii) wakati wa mafunzo hayo.

Ofisa Uangalizi Mkuu, Bi. Sheroline Mzava (aliyesimama) akiwasilisha mada kuhusu Taarifa ya Uchunguzi wa Kijamii (TUK) wakati wa mafunzo hayo yaliyofanyika hivi karibuni.

Mkuu wa Mashitaka Mkoa (RPO) wa Njombe, Wakili Shaban Mwegole (aliyesimama) akichangia mada.

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)

MAHAKAMA, WADAU KIGOMA WASHIRIKIANA KUKABILIANA NA MVUA ZA EL NINO

·         Wajenga mitaro kupitisha maji ya mvua Barabara ya Mahakama Hiltop Kigoma

Na AIDAN ROBERT, Mahakama-Kigoma

Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Kigoma imechukua hatua madhubuti za kukabiliana na mvua kubwa za El NiƱo zinazotajwa kunyesha mapema mwezi huu kwa kushirikiana bega kwa bega na Wadau mbalimbali katika ujenzi na uimarishaji wa mitaro ya barabara kuanzia eneo la Mahakama Kuu hadi Hiltop mkoani humo.

Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Kigoma, Bw. Yusuph Kasuka, hivi karibuni alifanya ukaguzi wa uchimbaji, ujenzi na uzibuaji wa mitaro ya maji iliyopo katika barabara ya Mahakama kwenda hoteli ya kitalii ya Hilltop.

Hatua hiyo haioneshi tu umuhimu wa usalama wa miundombinu ya majengo ya Mahakama na barabara zinazowahudumia wananchi, bali pia inaakisi nguvu ya ushirikiano wa dhati baina ya Mahakama na jamii inayoizunguka.

“Leo, kazi ya ukarabati na usafishaji wa mitaro ya kupitisha maji ya mvua katika barabara inayotoka eneo la Mahakama hadi Hilltop Kigoma inaendelea kwa kasi. Hatua hii inalenga kuhakikisha maji ya mvua yanapita kwa urahisi bila kusababisha mafuriko, uharibifu wa miundombinu ya barabara, au hatari kwa watumiaji wa njia hiyo na wananchi wa maeneo ya jirani,” alisema Bw. Kasuka.

Aliongeza kwa kusema kuwa, "ushirikiano wetu na Wadau mbalimbali hapa Kigoma unadhihirisha kuwa usalama wa miundombinu na mazingira yetu ni jukumu la pamoja, hasa kipindi hiki cha kujiandaa na msimu wa mvua kubwa."

Aliendelea kusema kuwa, Mahakama inatambua na kupongeza mchango mkubwa wa wadau wote waliojitokeza kushirikiana katika zoezi hili muhimu na kwamba jitihada hizo inalenga kulinda mali, kupunguza athari za vyanzo vya maji vilivyoziba na kuweka mazingira safi na salama yatakayowezesha huduma za kimahakama na shughuli za wananchi kuendelea bila kikwazo.

Kwa upande wake, Mhandisi Dan suka kutoka Kampuni ya Hilltop, alisema kwa niaba ya Kampuni hiyo kuwa, “tunawashukuru kila mdau aliyeshiriki kwa namna moja au nyingine kufanikisha kazi hii ya haraka na yenye tija kubwa kabla ya mvua hizo kuanza kunyesha.”

Vile vile alimuhakikishia Mtendaji wa Mahakama Kuu Kigoma, kuwa ujenzi huo utakamilika mapema kabla ya muda waliojiwekea ili kuzikabili mvua zinazotarajiwa kunyesha mapema hivi karibuni.

Wadau waliojitokeza kujenga mitaro hiyo kwa kushirikiana na Mahakama Kuu Kigoma ni pamoja na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA)-Kigoma, Magereza pamoja na Hoteli ya Hilltop ambapo kwa pamoja walihakikisha mitaro hiyo inayopitisha maji mengi kuelekea ziwani inakarabatiwa na kuwa imara katika kukabiliana maji mengi.

Mhandisi Ujenzi wa Kampuni wa Hilltop Kigoma, Dan Suka (kushoto) akitoa maelezo ya maendeleo ya ujenzi wa mitaro ya barabara ya Mahakama kwenda Hilltop, kwa  Mtendaji wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Kigoma, Bw. Yusuph Kasuka. Ujenzi wa mitaro hiyo ni jitihada za kubabiliana Mvua za El Nino.


Mtendaji wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Kigoma, Bw. Yusuph Kasuka akiwaelekeza jambo Mafundi wa Ujenzi  mitaro ya barabara ya Mahakama kwenda Hilltop unaoendelea.


Mtendaji wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Kigoma, Bw. Yusuph Kasuka akitembea katika mtaro mpya unaoendelea kujengwa kwa ushirikiano na wadau wanaotumia barabara hiyo ya Mahakama kwenda Hilltop Kigoma.

Mtendaji wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Kigoma, Bw. Yusuph Kasuka akitazama mtambo unaofanya kazi ya kutengeneza mitaro ya barabara ya Mahakama kwenda Hilltop Kigoma.

Mtendaji wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Kigoma, Bw. Yusuph Kasuka akiendelea kukagua na kuona ubora wa ujenzi wa mitaro hiyo inayojengwa ili kukabiliana na Mvua za El Nino.

Mtendaji wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Kigoma, Bw. Yusuph Kasuka akitazama uchanganyaji wa saruji na mchanga kwa ajili ya ubora wa ukuta wa kingo za mtaro unajengwa kwa ajili ya kukabiliana na mvua za El Nino.

Mhandisi Ujenzi wa Kampuni wa Hilltop Kigoma,  Mhandisi Dan suka akiendesha Mtambo alipokuwa akichonga barabara na mitaro  kwa ajili ya kukabiliana na Mvua za El Nino.


(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)

 

 

 

MADALALI, WASAMBAZA NYARAKA ZA MAHAKAMA WAHIMIZWA KUZINGATIA MAADILI

Na IMAN MZUMBWE – Mahakama, Songwe

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Songwe, Mhe. Gabriel Malata, amewataka Madalali, Wasambaza nyaraka na Mahakimu kuimarisha umoja, mshikamano na ushirikiano wanapotekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria, kanuni na maadili ya taaluma zao.

Mhe. Malata alitoa wito huo tarehe 9 Oktoba, 2026 wakati wa kikao chake na madalali pamoja na wasambaza nyaraka za Mahakama kilichofanyika katika ukumbi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Songwe. Kikao hicho kililenga kujadili utekelezaji wa majukumu ya wadau hao ili kuboresha utoaji wa huduma za Mahakama kwa wananchi.

Akizungumza katika kikao hicho, Mhe. Malata alisisitiza umuhimu wa wadau hao kutekeleza majukumu yao kwa weledi, uadilifu na kuzingatia taratibu zinazowaongoza. Alieleza kuwa utekelezaji wa majukumu kwa kuzingatia misingi ya taaluma na maadili ni muhimu katika kuimarisha imani ya wananchi kwa Mahakama na kuongeza ufanisi katika utoaji wa haki.

Kikao hicho pia kilijadili nafasi na umuhimu wa Madalali na wasambaza nyaraka katika kuiwezesha Mahakama kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi, hususan katika kutekeleza amri za Mahakama na kuhakikisha nyaraka zinafikishwa kwa wahusika kwa wakati. Masuala mengine yaliyojadiliwa ni uwajibikaji, uadilifu, uzingatiaji wa sheria na kanuni pamoja na changamoto zinazoathiri utekelezaji wa majukumu ya wadau hao.

Kwa upande wake, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Songwe, Mhe. Joyce Minde, aliwashauri madalali na wasambaza nyaraka kuimarisha utaratibu wa kufanya vikao vya ndani kwa ajili ya kujadili changamoto zinazowakabili katika kazi zao. Alieleza kuwa changamoto zitakazobainika zinapaswa kuwasilishwa katika Ofisi ya Naibu Msajili ili ziweze kushughulikiwa kwa wakati, kwa kushirikiana na wadau wengine wa Mahakama na kwa kuzingatia taratibu zinazostahili.

Akiwasilisha taarifa fupi kuhusu shughuli za wasambaza nyaraka, Mwenyekiti wa Wasambaza Nyaraka Songwe, Bw. Joachim Gabriel Kalungwe, alisema kuwa orodha ya wasambaza nyaraka walioteuliwa na Mahakama kwa mwaka 2026/2027 ina jumla ya wasambaza nyaraka watatu.

Alieleza kuwa shughuli za usambazaji nyaraka zinaendelea, huku msisitizo ukiwa ni kuhakikisha nyaraka na hati za Mahakama zinafikishwa kwa wahusika kwa wakati na kwa usahihi, kwa mujibu wa sheria.

Naye, Mwenyekiti wa Madalali, Bw. Paulo Carlos Mtweve, akizungumza kwa niaba ya madalali na wasambaza nyaraka, alibainisha changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika utekelezaji wa majukumu yao. Changamoto hizo ni pamoja na umbali wa maeneo ya kufikika, kutopatikana au kuhama kwa wahusika, changamoto za usafiri na kupatikana kwa taarifa zisizo sahihi kuhusu wahusika.

Kutokana na changamoto hizo, Bw. Mtweve alipendekeza kuimarishwa kwa ushirikiano kati ya Mahakama, madalali, wasambaza nyaraka na wadau wengine ili kupunguza ucheleweshaji wa huduma na kuhakikisha wananchi wanahudumiwa kwa ufanisi.

Kikao hicho ni sehemu ya juhudi za Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Songwe, za kuimarisha mawasiliano na ushirikiano na wadau wake, kwa lengo la kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu na kuboresha utoaji wa huduma za mahakama kwa wananchi.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Songwe, Mhe. Gabriel Malata, akizungumza na madalali, wasambaza nyaraka na mahakimu wakati wa kikao kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Songwe.

Mwenyekiti wa Wasambaza Nyaraka Songwe, Bw. Joachim Gabriel Kalungwe, akiwasilisha hoja wakati wa kikao hicho.

Madalali na wasambaza nyaraka wa Mahakama ya Songwe wakiwa katika picha ya pamoja.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo Songwe Mhe. Gabriel Malata akizungumza na kutoa shukrani kwa wadau waliohudhuria kikao hicho.

Wadau wa Mahakama wakifuatilia maelezo ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo Songwe Mhe. Gabriel Malata wakati wa kikao hicho.

Mwenyekiti wa Madalali Songwe, Bw. Paulo Carlos Mtweve, akizungumza mbele ya Mhe. Gabriel Malata (hayupo katika picha) wakati wa kikao hicho.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo Songwe Mhe. Gabriel Malata (wa tatu kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na Naibu Msajili, Mahakimu, madalali na wasambaza nyaraka wa Mahakama ya Songwe.

(Habari Hii Imehaririwa na Innocent Kansha & James Busanya -Mahakama)