Na NOEL SYLIVESTER- Mahakama, Songea
Mahakama ya Tanzania ni muhimili pekee wenye wajibu wa mwisho katika utoaji haki na katika kutekeleza wajibu huo, Mahakama imekuwa ikitoa mchango mkubwa katika ustawi wa maendeleo ya taifa.
Hayo yamebainishwa na Jaji
Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Songea, Mhe. James
Karayemaha, kwenye Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini yaliyofanyika kikanda
jana tarehe 2 Februari, 2026 kwenye Viwanja vya Mahakama Kuu Songea.
‘Maendeleo ya Taifa ni
mchakato wa kuboresha hali ya maisha ya wananchi wote wa nchi husika kwa njia
endelevu. Yanahusisha maendeleo katika nyanja mbalimbali kwa lengo la kuleta
ustawi wa Taifa kwa ujumla,’
alisema.
Mhe. Karayemaha alieleza kuwa maendeleo yanaweza kuonekana katika nyanja mbalimbali, ikiwemo kiuchumi kwenye ongezeko la kipato, ajira, uzalishaji na kuimarika kwa
uchumi wa nchi; kijamii katika upatikanaji wa elimu bora, afya, usawa na haki na teknolojia katika matumizi ya sayansi na teknolojia ili
kurahisisha maisha.
Maeneo mengine ni kwenye siasa katika uawala bora, amani, usalama, demokrasia na ushiriki wa
wananchi; miundombinu kwenye uwepo wa miundombinu mizuri (barabara, umeme, maji) na kiutamaduni katika kuheshimu na kuendeleza mila na tamaduni chanya.
‘Mahakama ya Tanzania imekuwa
ikitoa maamuzi ya migogoro mbalimbali kama vile ya uhifadhi wa maliasili,
masuala ya kodi, ardhi na mikataba. Katika utatuzi wa migogoro hiyo, Mahakama
imekuwa ikitoa mchango mkubwa katika ustawi wa maendeleo ya Taifa letu,’ Jaji Mfawidhi
alisema.
Aliongeza kuwa Mahakama ya Tanzania imekuwa ikitoa elimu kwa jamii juu ya sheria
mbalimbali kupitia maamuzi, vyombo vya habari na kwa njia ya mitandao, hivyo
kuleta uelewa wa pamoja katika masuala yote ya kisheria.
Mhe. Mhe. Karayemaha alibainisha kuwa hatua hiyo huchangia kuongeza uelewa wa wananchi
kuhusu sheria na haki zao, hivyo kujenga jamii inayoheshimu sheria na kusaidia
kuleta usawa katika jamii na kila mmoja kutambua wajibu wake katika kukuza
ustawi wa maendeleo ya taifa.
‘Katika kutoa haki, Mahakama
kwa kushirikiana na Taasisi nyingine za Serikali na sekta binafsi, imekuwa
ikiimarisha amani na utulivu katika jamii, hivyo kusababisha wananchi
kujihusisha na shughuli za kiuchumi na za kijamii na kusaidia kukua kwa ustawi
wa maendeleo ya Taifa,’ alisema.
Aidha, Jaji Mfawidhi alisema kuwa Mahakama inaendelea
kuboresha upatikanaji wa haki kwa kuongeza huduma za Mahakama za Mwanzo karibu
na wananchi ili kupunguza umbali, kuhakikisha upatikanaji kwa gharama nafuu na
kwa wakati muafaka.
‘Mathalani, katika Kanda yetu ya Songea, Mahakama ipo
katika hatua za mwisho za ujenzi wa Mahakama mpya za Mwanzo katika maeneo ya
Msamala na Lilondo katika Wilaya ya Songea. Hapo awali wananchi wa maeneo hayo
walipaswa kusafiri umbali mrefu ili kupata huduma za Mahakama. Ujenzi na
uanzishaji wa Mahakama za Mwanzo umefanyika katika maeneo mbalimbali nchini,
hivyo kusongeza huduma karibu na wananchi. Lakini pia vituo kama Namasakata,
Lukumbule, Magazini, Ligera, Wabaki vilivyokuwa vimefungwa vimefunguliwa na
wananchi wa maeneo hayo hawasafiri umbali mrefu kutafuta haki kama ilivyokuwa
zamani,’ alisema.
Maadhimisho hayo yalihudhuriwa Viongozi mbalimbali wa
Mahakama, Serikali na kidini, akiwepo Jaji wa Mahakama Kuu Tanzania Kanda ya
Songea, Mhe. DKt Emmanuel Kawishe, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Bregedia Ahmed Abbas
Ahmed, Jaji Mstaafu wa Mahakama Kuu, Mhe. Sirilius Matupa, Naibu Msajili,
Mtendaji, Mahakimu, Wadau na watumishi wa Mahakama kwa ujumla.
Sambamba na maadhimisho hayo, kulikuwepo na burudani
iliyotolewa na kwaya ya Mahakama Kuu Kanda ya Songea pamoja na ngoma za asili.










Hakuna maoni:
Chapisha Maoni