Na EUNICE LUGIANA, Mahakama-Pwani
Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhe. Abubakar Kunenge ameipongeza Mahakama ya Hakimu Mkazi Pwani kwa kushughulikia mashauri ya kimkakati kwa haraka ikiwemo mashauri nane (8) ya jinai na kuwezesha kuokoa miundombinu ya nchi na kuhakikisha kwamba nchi haipati hasara.
Mhe. Kunenge ambaye alikuwa Mgeni Rasmi kwenye Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini mkoani Pwani aliyasema hayo jana tarehe 02 Februari, 2026 alipokuwa akitoa salamu katika hafla ya maadhimisho hayo iliyofanyika katika viwanja vya Mahakama ya Hakimu Mkazi Pwani.
Mkuu wa Mkoa huyo ameipongeza Mahakama kwa kuondoa mazuio yasiyo na msingi ya kufanya ardhi kutotumika kwa wakati, wakati mashauri yako Mahakamani na hivyo kuwa changamoto kwa wawekezaji.
Alisema, “Nchi yetu ni sehemu ya uchumi wa Dunia inapotaka kukuza, kuboresha Maisha ya wananchi, haiwezi kuboresha maisha ya wananchi kama Serikali haina uwezo wa kifedha kama Serikali haijakaribisha Sekta Binafsi ambazo zina mitaji na utaalamu na teknolojia kuweza kufanya uwekezaji.”
Akizungumzia kuhusu Kaulimbiu ya Maadhimisho ya Siku ya Sheria isemayo; ‘Mchango wa Mahakama katika Ustawi na Maendeleo ya Taifa,’ Mhe. Kunenge alisema kaulimbiu hiyo inaonesha jinsi ambavyo Mahakama ina wajibu wa kuleta ustawi wa mtu mmoja mmoja na maendeleo ya Taifa kwa ujumla na inafanya hivyo kwa kutoa maamuzi kwa wakati pasipo kuchelewesha mashauri yote ya jinai na madai yanayofikishwa mahakamani.
“Naipongeza Mahakama ya Tanzania kwa kuchagua kaulimbiu hii kwani Taifa letu limeanza utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ambayo itaifikisha Tanzania katika uchumi wa ngazi ya juu au zaidi ikifika 2050,” alisema Mkuu wa Mkoa huyo.
Aliongeza kuwa, kupitia kaulimbiu hiyo, Wadau wote walioko kwenye mnyororo wa haki wanakumbushwa kuweka mikakati madhubuti inayolenga kuleta ustawi na maendeleo ya Taifa.
Naye Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Pwani, Mhe. Joyce Mkhoi alisema ustawi wa Taifa unategemea uwezo wa wanajamii kumudu mahitaji muhimu ya kibinadamu, yakiwemo chakula, mavazi na malazi na kwamba ili kuwezesha upatikanaji wa mahitaji hayo, Serikali ina wajibu wa kuweka mazingira wezeshi yatakayowawezesha wananchi kufanya kazi kwa uhuru, bila woga, ili kujipatia kipato halali katika mazingira ya amani.
Mhe. Mkhoi alisema katika kutekeleza hayo, Bunge hutunga sheria mbalimbali, Mahakama hutafsiri Sheria hizo na Serikali huzitekeleza.
Mfawidhi huyo alisema katika Maadhimisho ya Siku ya Sheria Nchini 2026, Mahakama imekuja na uchambuzi wa mikakati yake yenye lengo la kutengeneza mazingira wezeshi katika utoaji wa haki na kuchochea ustawi wa jamii na Taifa katika safari ya kufikia malengo ya Dira ya Taifa 2050.
Aliongeza kuwa, maeneo ya kimkakati yaliainishwa na kuanza kutekelezwa 2025 ni kusogeza huduma za Kimahakama karibu na mwananchi, kuwa na Mahakama Kuu kila Mkoa ingawa katika Mkoa Pwani bado Mahakama Kuu haijaanza kujengwa kutokana na muundo wa Mkoa huo.
Alisema kwamba, Mahakama ya Tanzania inategemea kufungua Masjala za kudumu za Mahakama ya Rufani katika kila Kanda za Dar es salaam, Arusha, Mbeya na Mwanza, kufanya mageuzi makubwa na maboresho ya matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ambayo yamewezesha uwazi na uwajibikaji wa Watumishi wa Mahakama na kurahisisha upatikanaji wa taarifa muhimu.
Mhe. Mkhoi alisema mkakati mwingine uliofanywa na Mahakama ni kushughulikia Mashauri ya Mikakati, mashauri hayo yanayohusu masuala ya biashara na uchumi yaliyokuwa yanashikilia pesa nyingi kwa Mkoa wa Pwani. Akitoa mfano wa mashauri nane (8) ya jinai yaliyofunguliwa mwaka 2025 yaliyohusu uhujumu uchumi yakihusisha uharibifu wa miundombinu.
Katika Mashauri hayo, jumla ya Tshs. 707,000,000/= ziliweza kufidiwa kwa Serikali na kuiepusha Serikali kuingia kwenye hasara kupitia ukarabati wa miundombinu ya Reli ya Umeme (SGR) iliyokuwa imefanyiwa uharibifu kwa kuibiwa.
Hakimu Mkazi Mfawidhi huyo, aliongeza kuwa kuna uhusiano mkubwa kati ya uwepo wa Mahakama na Amani na Utulivu katika jamii au Nchi.
Viongozi mbalimbali wa Serikali, Vyama vya Siasa, Viongozi wa Dini na Wadau wa Mahakama walihudhuria katika hafla ya Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini.
Meza Kuu ikiongozwa na Mgeni Rasmi wa Maadhimisho ya Siku ya Sheria Nchini ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhe. Abubakar Kunenge (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Pwani, Mhe. Joyce Mkhoi (wa pili kushoto), wa kwanza kushoto ni Hakimu Mkazi Mahakama ya Wilaya Kibaha, Mhe. Emmael Lukumai, wa kulia ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani, Bi. Pili Hassan Mnyema, na wa kwanza kulia ni Mkuu wa Mashtaka Mfawidhi Pwani, Bi. Faraja George.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhe. Abubakar Kunenge akitoa salamu kwenye sherehe za Maadhimisho ya Siku ya Sheria mkoani humo ambazo kwa upande Pwani zilifanyika katika viwanja vya Mahakama
ya Hakimu Mkazi.
Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Hakimu Mkazi Pwani, Mhe. Joyce Mkhoi akitoa Hotuba wakati wa Sherehe za Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini zilizofanyika tarehe 02 Februari, 2026 katika viwanja vya Mahakama ya Hakimu Mkazi Pwani.
Maandamano ya Watumishi na Wadau wa Mahakama kuelekea katika viwanja
vya Mahakama ya Hakimu Mkazi Pwani kushiriki katika Maadhimisho ya Siku ya Sheria Nchini 02 Februari, 2026.
Meza Kuu ikiongozwa na Mgeni Rasmi Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhe. Abubakar Kunenge (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi wa Dini (waliosimama nyuma). Wa pili kushoto ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Pwani, Mhe. Joyce Mkhoi, wa kwanza kushoto ni Hakimu Mkazi Mahakama ya Wilaya Kibaha, Mhe. Emmael Lukumai, wa pili kulia ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani, Bi. Pili Hassan Mnyema na wa kwanza kulia ni Mkuu wa Mashtaka Mfawidhi Pwani, Bi. Faraja George.









Hakuna maoni:
Chapisha Maoni