Jumatano, 6 Mei 2026

BARAZA LA WAFANYAKAZI MAHAKAMA KUU MASJALA NDOGO SINGIDA LAKETI

Na EVA LESHANGE, Mahakama-Singida

Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo  ya Singida na Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi wa Mahakama hiyo, Mhe.Ayoub Mwenda ameongoza  kikao cha Baraza la Wafanyakazi ambapo amewasihi Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi kutumia vizuri fursa ya kikao hicho kuchangia hoja na kutoa mapendekezo mbalimbali yatakayoboresha mazingira ya kazi.

Akifungua kikao hicho kilichofanyika tarehe 02 Mei, 2026 kwenye ukumbi wa Mikutano wa Mahakama Kuu ya Singida, Mhe. Mwenda alisema kuwa, Mabaraza ya Wafanyakazi yapo kisheria na yana umuhimu mkubwa katika kulinda haki na maslahi ya watumishi mahala pa kazi sambamba na kuleta amani na utulivu mahali pa kwa kazi kwa kutatua migogoro kwa njia ya mazungumzo baina ya mwajiri na wafanyakazi.

“Matarajio yangu ni kuwa kila mjumbe katika kikao hiki atashiriki kikamilifu na kwa pamoja tutaibua hoja nzuri za kuwasilisha katika kikao cha Baraza Kuu la Mahakama ya Tanzania,” alisema Jaji Mfawidhi huyo.

Aidha, katika Baraza hilo wajumbe walipata fursa ya kufanya uchaguzi wa kuchagua Katibu, Katibu Msaidizi na Mjumbe mmoja atakayewakilisha watumishi katika Baraza kuu la Wafanyakazi Taifa.

Uchaguzi huo ulisimamiwa na Ofisa Kazi- Mkoa wa Singida, Bw. Boniface Ntalula ambaye aliwaelewesha wajumbe wa kikao hicho kwamba, Mabaraza ya Wafanyakazi kazi yapo kisheria na yalianza tangu mwaka 1970 na yana umuhimu mkubwa ikiwemo kushauri juu ya masuala mbalimbali ya kiutumishi, kutatua migogoro kazini na pia kuimarisha mshikamano baina ya mwajiri na waajiriwa.

Wakati wa ufunguzi wa kikao hicho, alitoa utaratibu wa uchaguzi na wajumbe wanaopaswa kupiga kura kwa mujibu wa Mkataba. Baada ya zoezi la kupiga kura kukamilika Msaidizi wa Kumbukumbu, Bw. Amiri Bakari aliibuka kuwa Katibu mpya wa Baraza hilo, Bi. Anna Kisambale, Katibu Msaidizi na Bi. Dorisi Busanji alichaguliwa kuwa Mwakilishi wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania (TUGHE) Baraza Kuu la Wafanyakazi Taifa.

Aidha, taarifa ya utekelezaji wa bajeti kwa mwaka wa fedha 2025/2026 ilisomwa na kuona utekelezwaji wa masuala mbalimbali hususan yanayolenga watumishi moja kwa moja, kuona mafanikio na changamoto na namna zilivyotatuliwa kwa mwaka wa fedha  ujao wa 2026/2027.

Akihitimisha kikao hicho cha Baraza la Wafanyakazi, Mwenyekiti wa Kikao, Mhe.  Mwenda aliwasisitiza watumishi kutekeleza wajibu wao na kufanya kazi kwa bidii na kutumia mafanikio yao katika kujenga hoja za kuboreshewa maslahi.

Vilevile aliwasisitiza viongozi wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania (TUGHE) Mkoa na wale wenyekiti wa Matawi ya TUGHE Mahakama kuendelea kuwasisitiza watumishi kujiunga na Chama hicho kwani ni muhimu na vipo kisheria.


Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo Singida na Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi wa Mahakama hiyo, Mhe. Ayoub Mwenda (aliyesimama) akisalimia wajumbe waliohudhuria kikao hicho cha baraza (hawapo katika picha).  Kushoto ni Ofisa Kazi Mkoa wa Singida, Bw. Boniface Ntalula na  kulia ni Bw. Tamsoni Mshigati, Katibu wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania (TUGHE) Mkoa wa Singida.

Ofisa Kazi Mkoa wa Singida, Bw.Boniface Ntalula (aliyesimama) akjitambulisha na kufungua Baraza la Wafanyakazi Mahakama Kuu Masjala Ndogo Singida.

Sehemu ya wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi Singida waliohudhuria kikao hicho kilichofanyika tarehe 02 Mei, 2026 kwenye Ukumbi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Singida.

 Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo Singida, Mhe. Ayoub Mwenda akikata keki kuashiria kuzinduliwa kwa Baraza la Wafanyakazi Singida ikiwa ni Baraza la Kwanza tangu Mahakama hiyo ilipotangazwa rasmi kuanzishwa kwa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Singida.

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Njombe)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni