Na EVA LESHANGE, Mahakama-Singida
Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya
Tanzania Masjala Ndogo ya Singida na
Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi wa Mahakama hiyo, Mhe.Ayoub Mwenda
ameongoza kikao cha Baraza la Wafanyakazi
ambapo amewasihi Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi kutumia vizuri fursa ya kikao
hicho kuchangia hoja na kutoa mapendekezo mbalimbali yatakayoboresha mazingira
ya kazi.
Akifungua kikao hicho kilichofanyika
tarehe 02 Mei, 2026 kwenye ukumbi wa Mikutano wa Mahakama Kuu ya Singida, Mhe.
Mwenda alisema kuwa, Mabaraza ya Wafanyakazi yapo kisheria na yana umuhimu
mkubwa katika kulinda haki na maslahi ya watumishi mahala pa kazi sambamba na
kuleta amani na utulivu mahali pa kwa kazi kwa kutatua migogoro kwa njia ya
mazungumzo baina ya mwajiri na wafanyakazi.
“Matarajio yangu ni kuwa kila mjumbe
katika kikao hiki atashiriki kikamilifu na kwa pamoja tutaibua hoja nzuri za
kuwasilisha katika kikao cha Baraza Kuu la Mahakama ya Tanzania,” alisema Jaji
Mfawidhi huyo.
Aidha, katika Baraza hilo wajumbe
walipata fursa ya kufanya uchaguzi wa kuchagua Katibu, Katibu Msaidizi na Mjumbe
mmoja atakayewakilisha watumishi katika Baraza kuu la Wafanyakazi Taifa.
Uchaguzi huo ulisimamiwa na Ofisa
Kazi- Mkoa wa Singida, Bw. Boniface Ntalula ambaye aliwaelewesha wajumbe wa
kikao hicho kwamba, Mabaraza ya Wafanyakazi kazi yapo kisheria na yalianza
tangu mwaka 1970 na yana umuhimu mkubwa ikiwemo kushauri juu ya masuala mbalimbali
ya kiutumishi, kutatua migogoro kazini na pia kuimarisha mshikamano baina ya
mwajiri na waajiriwa.
Wakati wa ufunguzi wa kikao hicho, alitoa
utaratibu wa uchaguzi na wajumbe wanaopaswa kupiga kura kwa mujibu wa Mkataba. Baada
ya zoezi la kupiga kura kukamilika Msaidizi wa Kumbukumbu, Bw. Amiri Bakari
aliibuka kuwa Katibu mpya wa Baraza hilo, Bi. Anna Kisambale, Katibu Msaidizi
na Bi. Dorisi Busanji alichaguliwa kuwa Mwakilishi wa Chama cha Wafanyakazi wa
Serikali na Afya Tanzania (TUGHE) Baraza Kuu la Wafanyakazi Taifa.
Aidha, taarifa ya utekelezaji wa
bajeti kwa mwaka wa fedha 2025/2026 ilisomwa na kuona utekelezwaji wa masuala
mbalimbali hususan yanayolenga watumishi moja kwa moja, kuona mafanikio na
changamoto na namna zilivyotatuliwa kwa mwaka wa fedha ujao wa 2026/2027.
Akihitimisha kikao hicho cha Baraza
la Wafanyakazi, Mwenyekiti wa Kikao, Mhe. Mwenda aliwasisitiza watumishi kutekeleza
wajibu wao na kufanya kazi kwa bidii na kutumia mafanikio yao katika kujenga
hoja za kuboreshewa maslahi.
Vilevile aliwasisitiza viongozi wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania (TUGHE) Mkoa na wale wenyekiti wa Matawi ya TUGHE Mahakama kuendelea kuwasisitiza watumishi kujiunga na Chama hicho kwani ni muhimu na vipo kisheria.



Hakuna maoni:
Chapisha Maoni