· Mahakama Sports yashinda Makombe manne Njombe mashindano ya michezo Mei Mosi
· Asisitiza umuhimu wa Michezo
Jaji
Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Njombe, Mhe. Victoria Nongwa
amewasisitiza Wanamichezo wa Mahakama Sports na Watumishi wengine Mahakama juu
ya umuhimu wa Michezo na kusema kuwa ina faida nyingi ikiwemo kulinda afya ya mwili, pia ni ajira,
vilevile huleta furaha pamoja na ushirikiano.
Mhe. Nongwa aliyasema hayo hivi karibuni alipohudhuria hafla ya usiku ya kuhitimisha michezo Mkoani Njombe iliyofanyika kwenye ukumbi wa Hoteli ya ‘Agreement’ mkoani Njombe.
Katika
hafla hiyo, alikuwepo pia Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Njombe, Mhe. Joseph
Luambano, Mwenyekiti wa Mahakama Sports, Mhe. Martine Mushi, Makamu Mwenyekiti
wa Mahakama Sports, Mhe. Maria Mayalla na Wanamichezo wa Mahakama Sports.
Naye,
Katibu wa Mahakama Sports, Bw. Robert
Donald Tende aliwasilisha taarifa aliyoisoma mbele ya Mhe. Nongwa pamoja
na Wanamichezo ambapo alimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwalinda na kuwajaalia
afya njema na kuwakinga na maradhi na majeraha mbalimbali wakati wote wa
mashindano.
“Pili,
naushukuru Uongozi wa Mahakama ya Tanzania kwa kutupatia ruhusa na uwezeshaji wa
rasilimali fedha wa kutuwezesha kushiriki kikamilifu katika mashindano ya Mei
Mosi, 2026,” alisema Bw. Tende.
Vilevile,
aliwashukuru Wachezaji wa Mahakama Sports walioshiriki mazoezi na mashindano kwa
kujituma na kujitoa kwao katika kipindi chote kwa manufaa ya Timu ya Mahakama
ya Tanzania.
Katibu
huyo wa Mahakama Sports aliendelea
kusema kuwa, “Wafanyakazi wanaoshiriki michezo ni kundi mojawapo la
wafanyakazi wanaotegemewa na Taifa kiuchumi, kijamii na huduma mbalimbali kwa
umma.”
Bw. Tende aliongeza kuwa, Timu ya Michezo ya Mahakama
ya Tanzania (Mahakama Sports) ilishiriki kikamilifu katika Mashindano ya Mei
mosi yaliyofanyika kitaifa mkoani Njombe kuanzia tarehe 13 Aprili, 2026 hadi 01
Mei, 2026.
Alisema
kuwa, Mashindano hayo yalifunguliwa rasmi tarehe 20 Aprili, 2022 na Mgeni Rasmi
aliyekuwa Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri
Mkuu Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Rahma Kisuo.
Mashindano ya Mei Mosi yamelenga kusherehesha Sikukuu ya Wafanyakazi ili kuboresha mahusiano baina ya watumishi wa umma, kutoka Wizara, Mashirika, Taasisi na Idara mbalimbali za Serikali, pamoja na jamii lengo likiwa ni kuboresha na kulinda afya za watumishi na kuimarisha nguvu kazi katika utumishi wa umma.
Bw. Tende alibainisha kupitia taarifa yake kuwa katika michezo hiyo jumla ya Wizara, Idara, Taasisi za Umma, Mashirika ya Umma 61 walishiriki mashindano hayo ikiwemo Mahakama ya Tanzania.
Alieleza
kuwa, Timu ya Mahakama ilijumuisha washiriki 84 na Timu
ya ‘Mahakama Sports Club’ ilishiriki jumla ya michezo saba ambapo iliweza kunyakua jumla ya Makombe manne ambayo ni Kamba
mshindi wa tatu, Karata mshindi wa kwanza, Baiskeli mshindi wa pili na Mchezo
wa Bao ni mshindi wa pili.
Wanamichezo wa Mahakama Sports ni watumishi kutoka katika Mahakama mbalimbali zilizopo nchini Tanzania ambapo wanamichezo hao wamejikita katika michezo kama vile Mpira wa Miguu, Netiboli, Kamba Wanawake, Kamba Wanaume, Riadha, Kurusha Tufe, Drafti Karata, Baiskeli na Bao.
Katibu wa Mahakama Sports Club, Bw. Robert Tende akisoma taarifa ya michezo tangu walipoanza mpaka walipomaliza na mashindano ya michezo ya Mei Mosi, 2026.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni