Jumanne, 5 Mei 2026

JAJI MFAWIDHI SINGIDA ASISITIZA WATUMISHI KUIISHI KWA VITENDO SALAMU YA MAHAKAMA

Na EVA LESHANGE, Mahakama-Singida

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Singida, Mhe. Ayoub Mwenda amewasisitiza watumishi kuiishi salamu ya Mahakama ya Tanzania isemayo ‘Uadilifu, Weledi na Uwajibikaji.’

Mhe. Mwenda amewasisitiza watumishi hao hivi karibuni akiwa katika ziara yake ya kwanza ya ukaguzi iliyofanyika kuanzia tarehe 28 Aprili 2026 hadi 30 Aprili 2026 katika Wilaya za Iramba, Manyoni na Singida Mjini.

Katika ziara hiyo aliwakumbusha watumishi kuwa kazi ya kutoa haki sio jambo dogo hivyo watumishi wasijiingize katika vitendo viovu ambapo alisema, “ndugu watumishi nasisitiza kuwa waadilifu kwa kuwa ndio msingi mkubwa wa kutoa haki hivyo, muwe na tabia njema kazini na nje ya kazi.”

Aidha, Jaji Mwenda aliwapongeza watumishi wote kwa ujumla kwa kazi nzuri inayofanyika hususan ya usikilizwaji wa mashauri kwani katika taarifa zote zilizowasilishwa mashauri yote yanayofunguliwa yanaisha kwa wakati.

Kadhalika, amesisitiza kila mmoja kufanya kazi kwa bidii na kwamba asitokee mtu wa kumkwamisha mwingine, kuheshimiana, kufanya kazi kwa umoja na kufanya majukumu zaidi ya mengine pasipo kuangalia kada ili kuongeza ufanisi. Vilevile aliwashauri watumishi kuongeza maarifa kwa kujibidiisha kwenye mafunzo mbalimbali ili kuimarisha taaluma.

Katika ukaguzi huo alitembelea pia Gereza la Wilaya Manyoni na kujionea hali halisi na alipongeza ushirikiano uliopo kati ya Mahakama na Wadau wa Haki Jinai kwani katika Gereza hilo hakukuwa na msongamano wa Mahabusu hivyo akasisitiza kuendeleza ushirikiano huo ili kuhakikisha Magereza yanakuwa na nafasi ili yaweze kujiendesha.

Katika ziara hiyo, Viongozi walipanda miti ya matunda kusisitiza utunzwaji wa mazingira katika maeneo yote ya Mahakama.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya  Singida, Mhe. Ayoub Mwenda (aliyeketi katikati) akiwa katika picha ya pamoja na sehemu ya watumishi wa Mahakama ya Wilaya Iramba (waliosimama). Wa pili kushoto ni Naibu Msajili Mahakama Kuu Masjala Ndogo Singida, Mhe. Evodia Kyaruzi, wa pili kulia ni Mtendaji Mahakama Kuu Masjala Ndogo Singida, Bw. Filbert Matotay, wa kwanza kushoto ni Hakimu Mkazi Mfawidhi- Mahakama ya Hakimu Mkazi Singida, Mhe.Allu Nzowa na wa kwanza kulia ni Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya Iramba, Mhe.Luzango Khamsini.

Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya Manyoni, Mhe.Alisile Mwankejela (aliyesimama) akiwasilisha taarifa fupi ya utekelezaji mbele ya Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Singida, Mhe. Ayoub Mwenda (aliyeketi mbele katikati) wakati alipofanya ziara ya kikazi. Aliyeketi kushoto ni Naibu Msajili Mahakama Kuu Masjala Ndogo Singida, Mhe. Evodia Kyaruzi na kulia ni Mtendaji Mahakama Kuu Masjala Ndogo Singida, Bw. Filbert Matotay.

 Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Masjala Ndogo Singida, Mhe. Ayoub Mwenda akiwa na wadau wa Haki Jinai alipotembelea Gereza la Wilaya Manyoni.

Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Masjala Ndogo Singida, Mhe. Ayoub Mwenda akipanda mti wa Matunda katika Mahakama ya Wilaya Manyoni.

Naibu Msajili Mahakama Kuu Masjala Ndogo Singida, Mhe. Evodia Kyaruzi akipanda mtu wa matunda Mahakama ya Wilaya Manyoni.

Mtendaji wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Singida, Bw.Filbert Matotay akipanda mti wa matunda Mahakama ya Wilaya Manyoni.

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Njombe)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni