Jumamosi, 29 Agosti 2026

MTENDAJI MKUU AZUNGUMZA NA WATUMISHI WA MAHAKAMA ZA CHINI DAR ES SALAAM

Na WINFRED NZILANO-Mahakama Kisutu, Dar es Salaam

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Dkt. John Jingu, tarehe 27 Agosti, 2026, alifanya kikaokatika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, kuzungumza na watumishi.

Watumishi hao walitoka katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na Kinondoni, wawakilishi kutoka Mahakama za Wilaya Kivukoni, Temeke, Kigamboni, Ilala na Ubungo.

Hii ni mara yake ya kwanza tangu ateuliwe na kuapishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kushika wadhifa huo. Dkt. Jingu aliambatana na Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Nkya.

Kikao hicho kililenga kufanya utambulisha kwa watumishi, kufahamu mwenendo wa utekelezaji wa majukumu na kusikiliza changamoto zinazowakabili katika mazingira yao ya kazi.

Akizungumza katika kikao hicho, Dkt. Jingu alitoa shukrani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uteuzi wake. Alieleza ujio wake ni sehemu ya juhudi za uongozi wa Mahakama kuendelea kuwa karibu na watumishi na kupata uelewa wa moja kwa moja kuhusu changamoto wanazokutana nazo katika kutekeleza majukumu yao.

Katika kikao hicho, watumishi walipata fursa ya kuwasilisha changamoto, hoja na mapendekezo mbalimbali yanayohusu mazingira ya kazi na utekelezaji wa majukumu yao. Dkt. Jingu aliahidi kuzifanyia kazi kwa kuzingatia taratibu na mamlaka zilizopo.

Kwa upande wake, Msajili Mkuu aliwasihi watumishi kuendelea kufanya kazi kwa bidii, uadilifu na kujituma katika kutekeleza majukumu yao. Alisisitiza umuhimu wa kutoa huduma bora kwa wote wanaofika mahakamani ili kujenga taswira nzuri ya Mahakama kwa wananchi.

Naye Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Mhe. Franco Kiswaga, alitoa shukrani kwa juhudi ambazo zimefanyika kuboresha masilahi ya watumishi na miondombinu ya Mahakama.

Kikao hicho kimeonesha dhamira ya uongozi wa Mahakama ya Tanzania ya kuwa karibu na watumishi, kusikiliza changamoto zao na kuweka mazingira bora ya utendaji kazi.


Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Dkt. John Jingu, akizungumza na watumishi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam. Picha chini ni sehemu ya watumishi kutoka Mahakama za chini za Mkoa wa Dar es Salaam.


Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Mhe. Franco Kiswaga, akifanya utambulisho wa watumishi waliohudhulia katika kikao.

Mmoja ya watumishi akiwasilisha hoja wakati wa kikao hicho.

Picha ya pamoja na Watendaji na Naibu Wasajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kivukoni.

Picha ya pamoja na Mahakimu Wafawidhi wa Mahakama za Wilaya na Mahakama za Mwanzo.

Picha ya pamoja na Maafisa utumishi Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kivukoni, Mahakama ya Wilaya Kinondoni, Mahakama ya Wilaya Ilala, Mahakama ya Wilaya Kigamboni, Mahakama ya Wilaya Ubungo na Mahakama ya Wilaya Temeke.

Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni