Jumamosi, 29 Agosti 2026

JAJI MKUU MASAJU AMUAPISHA MHE. DEOGRATIUS NDEJEMBI KUWA MAKAMU WA RAIS WA TANZANIA

  •   Rais, Mhe. Dkt. Samia ampongeza Mhe. Ndejembi kwa kushika wadhifa huo
  •    Amtaka Makamu wa Rais huyo kuwa tayari kujifunza
  •   Asema bidii, nidhamu, weledi na utayari vitamsaidia kutekeleza majukumu yake ipasavyo

Na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma

Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju leo tarehe 29 Agosti, 2026 amemuapisha Mhe.  Deogratius John Ndejembi kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Hafla ya Uapisho huo imefanyika katika Viwanja vya Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma na kushuhudiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na Viongozi mbalimbali wa kitaifa akiwemo pia Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Waziri Mkuu wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, Mawaziri, Viongozi wengine na Wageni waalikwa mbalimbali.

Uteuzi na uapisho wa Mhe. Ndejembi unakuja baada ya kujiuzulu kwa aliyekuwa Makamu wa Rais wa Tanzania, Mhe. Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi tarehe 25 Agosti, 2026 ikiwa ni pamoja na kupitishwa na kuidhinishwa kwa kauli moja ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Spika, Mhe. Mussa Azzan Zungu, kufuatia pendekezo lililoridhiwa na Kamati Kuu pamoja na Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Akizungumza mara baada ya hafla hiyo, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amempongeza na kumpa pole Mhe. Ndejembi kwa kupewa jukumu hilo kubwa katika umri wake mdogo, huku akibainisha kuwa, uamuzi huo ulilenga kurudisha nafasi hiyo kwa vijana wenye nguvu, ari, na kasi ya kujituma serikalini.

“Nitumie fursa hii kukupa pole Mhe. Ndejembi katika umri mdogo tumekutwisha jukumu kubwa bila kukushauri, lakini kipekee nivishukuru sana vikao vya Chama Cha Mapinduzi, Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi kwa kupendekeza na kuliridhia jina la Mhe. Deogratius John Ndejembi katika nafasi ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Na hii ni baada ya kuzingatia sifa na vigezo alivyo navyo, ikiwa ni pamoja na umri wake, ambao kwa kweli bado ni kijana mwenye nguvu, ari, na kasi ya kujituma na kutekeleza shughuli za Serikali. Kwa kauli moja tuliamua nafasi ile tuirudishe kwa vijana na tuendelee kulea, imetoka kwa kijana, tumeirudisha kwa kijana, sasa kijana tukuombe ukakue si kwa umri lakini ukakue akili,” amesema Rais, Mhe. Dkt. Samia.

Aidha, Mhe. Dkt. Samia amesema kuwa hana shaka na utendaji kazi wa Makamu wa Rais, Mhe. Deogratius Ndejembi kwani kabla ya wadhifa huo alishika nafasi mbalimbali za uongozi serikalini na sekta binafsi, hivyo, uzoefu huo utamsaidia katika kutekeleza majukumu ya dhamana hiyo aliyopewa.

“Hakuna shule inayosomesha Umakamu wa Rais, hakuna. Ila sifa zako za bidii, nidhamu, weledi, na utayari wako wa kujifunza, kufuatilia, na kusimamia utekelezaji wa shughuli mbalimbali zitakusaidia kutimiza majukumu hayo. Nakuhimiza neno kujifunza; kujifunza ni pamoja na kusoma kwa wengine waliopo nawe,” amesisitiza.

Mambo makuu aliyoyasisitiza Rais Samia kwa Makamu wa Rais mpya ni pamoja na Ukuaji wa Kiakili na Nidhamu, kuwa na bidii, nidhamu, weledi na utayari wa kujifunza kutoka kwa viongozi wengine na waliotangulia.

Kadhalika, Mhe. Dkt. Samia amemkumbusha Makamu wa Rais, Mhe.  Ndejembi kutambua kuwa, cheo alichopewa ni dhamana kutoka kwa Watanzania na sio ufalme, hivyo anapaswa kuwatumikia wananchi wote bila ubaguzi au kujali tofauti zao.

“Nakusihi uweke maanani kwamba cheo ni dhamana. Cheo hiki tulichokupa si ufalme; ni dhamana. Dhamana uliyopewa na Watanzania kupitia Chama Kikuu kinachoongoza Dola, Chama Cha Mapinduzi, na kupitia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa hiyo nenda ukawatumikie bila kujali tofauti zao,” amesisitiza Rais Samia.

Vilevile amemsisitiza kuwa na Uzalendo na Uadilifu kwa kutekeleza majukumu kwa utii, uaminifu, utu, busara, hekima na maarifa huku akimtanguliza Mwenyezi Mungu mbele.

Mbali na hayo, Rais, Mhe. Dkt. Samia amezungumzia kuhusu Utekelezaji wa Mipango ya Maendeleo: Kazi kubwa ya kusimamia utekelezaji wa Ilani ya CCM pamoja na Dira ya Taifa ya Maendeleo, 2050.

“Tunayo mambo mengi tuliyoahidi kupitia Ilani ya Chama chetu ya mwaka 2020-2025 na kwenda mbele 2030. Aidha, kama unavyofahamu, tumeanza utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya miaka 25 inayokuja, ambayo imebeba matamanio na matarajio makubwa ya maendeleo kwa wananchi wetu," amesema. 

Ameongeza kuwa, ili kutekeleza yote hayo kwa maslahi yanayostahili wananchi na taifa kwa ujumla, wanahitaji umoja, mshikamano, ushirikiano, utulivu, na uongozi bora na ushirikiano kwakuwa mambo hayo ni muhimu kuyazingatia katika utekelezaji majukumu na kuyafikia matamanio na matarajio ya Watanzania.

Aidha, Rais Samia amewashukuru Viongozi mbalimbali pamoja na Mabalozi na Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa waliohudhuria hafla hiyo, akieleza kuwa mahudhurio yao yanadhihirisha amani, utulivu, na uimara wa Katiba na mifumo ya kisiasa ya Tanzania katika kuendesha mabadiliko ya uongozi kwa amani bila misukosuko.

Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju akimuapisha Mhe. Deogratius John Ndejembi kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania leo tarehe 29 Agosti, 2026 katika Viwanja vya Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma. Anayeshuhudia katikati ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.


Mhe. Deogratius John Ndejembi akila kiapo cha kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mbele ya Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju leo (hayupo katika picha). Hafla ya Uapisho wake imefanyika leo tarehe 29 Agosti, 2026 katika Viwanja vya Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius John Ndejembi akisaini Hati ya Kiapo mara baada ya kula kiapo cha kushika wadhifa huo leo tarehe 29 Agosti, 2026 Ikulu Chamwino jijini Dodoma.

Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju akisaini Hati ya Kiapo mara baada ya kumuapisha Mhe. Deogratius John Ndejembi kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 29 Agosti, 2026 Ikulu Chamwino jijini Dodoma.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Watanzania mara baada ya Uapisho wa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan leo tarehe 29 Agosti, 2026 Ikulu Chamwino jijini Dar es Salaam.

Viongozi mbalimbali wa Serikali, Vyama vya Siasa na Wageni waalikwa wakishuhudia na kushangilia uapisho wa Mhe. Deogratius John Ndejembi wa kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania leo tarehe 29 Agosti, 2026 katika viwanja vya Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma.

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Dkt. John Antony Jingu pamoja na Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Kiaki Nkya ni miongoni mwa waliohudhuria katika Hafla ya Uapisho wa Makamu wa Rais, Mhe. Deogratius John Ndejembi leo tarehe 29 Agosti, 2026 katika viwanja vya Ikulu Chamwino jijini Dodoma.

Meza kuu ikiongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya Uapisho wa Makamu wa Rais mpya. Wa nne kushoto ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius John Ndejembi, wa nne kushoto ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, wa tatu kushoto ni Waziri Mkuu wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, wa kwanza kushoto ni Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju, wa tatu kulia ni Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mussa Azzan Zungu, wa pili kushoto ni Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Mhe. Zubeir Ali Maulid, wa kwanza kulia ni Katibu Mkuu Kiongozi, Mhe. Balozi Dkt. Moses Mpogole Kusiluka na wa kwanza kulia ni Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Ndugu Stephen Masato Wasira.

Meza kuu ikiongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan wakiwa katika picha ya pamoja na Mawaziri mbalimbali wa Kisekta waliohudhuria Hafla ya Uapisho wa Makamu wa Rais mpya, Mhe. Deogratius John Ndejembi (wa nne kushoto).

Meza kuu ikiongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan wakiwa katika picha ya pamoja na Viongozi wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama.

Meza kuu ikiongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan (katikati) wakiwa katika picha ya pamoja na sehemu ya Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania wakiongozwa na Jaji Kiongozi wa Mahakama hiyo, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani (aliyesimama wa tatu kushoto).

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na familia ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius John Ndejembi (wa tatu kushoto).













 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni