Ijumaa, 28 Agosti 2026

WATUMISHI MBEYA WATEMBELEA KITUO CHA KUFUA UMEME MTERA

Na MUKSINI NAKUVAMBA – Mahakama, Mbeya

Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya, Mhe. Fahamu Mtulya amewaongoza Watumishi wa Masjala hiyo kufanya ziara ya kujifunza katika Kituo cha kupooza na kusambaza umeme cha Mtera, kilichopo Bwawa la Mtera mkoani Iringa kwa lengo kuwajengea watumishi uelewa wa masuala ya uzalishaji wa nishati ya umeme kwa njia ya maji.

Watumishi hao, walipata elimu ya kina kuhusu mchakato wa uzalishaji wa umeme, kuanzia hatua za awali za uzalishaji hadi umeme unapofikia hatua ya mwisho ya kumwezesha mtumiaji kupata huduma hiyo.

Aidha, elimu hiyo iliambatana na uhamasishaji wa matumizi ya nishati safi, hususan katika matumizi ya majumbani na kwenye vyombo vya usafiri, huku watumishi wakifafanuliwa namna matumizi ya nishati safi yanavyoweza kuwa na mchango mkubwa katika kupunguza athari za kimazingira na kuboresha maisha na ustawi wa jamii.

Matumizi ya nishati safi yana manufaa mathalani kuokoa muda, kupunguza gharama, kutunza mazingira na kulinda afya za watumiaji, hivyo ni wito kwa jamii kuendelea kuhamasishwa na kuelimishwa kuhusu fursa na manufaa yanayotokana na matumizi ya nishati hiyo.

Watumishi hao wameaswa kuendelea kuwa mabalozi wazuri katika kutunza miundombinu ya umeme kwani umeme unachagiza maaendeleo ya Taifa, huku wataalum hao wakitoa wito kwa Majaji na Mahakimu kuchukulia kwa uzito wa aina yake suala uendeshaji wa mashauri yanayo husu uharibifu wa miundo mbinu ya umeme.

Ziara hiyo pia ilitoa fursa kwa watumishi hao kutembelea Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Iringa, ambapo walikutana na kufanya mazungumzo na viongozi pamoja na watumishi wa Mahakama Kuu Masjala hiyo.

Mazungumzo ambayo yaliweka msisitizo katika umuhimu wa kuendelea kujenga ushirikiano, mshikamano na kubadilishana uzoefu miongoni mwa watumishi wa Mahakama katika Masjala hizo, kwa lengo la kuimarisha utendaji na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma.

Sehemu ya watumishi na viongozi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya wakipewa maelezo na elimu mbalimbali juu ya namna umeme unavyochakatwa katika ziara hiyo.

Sehemu ya watumishi na viongozi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya wakipewa maelezo na elimu mbalimbali juu ya namna umeme unavyochakatwa katika ziara hiyo.

Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya Mhe. Fahamu Mtulya akiteta jambo na Waandishi wa Habari katika ziara hiyo. 

Sehemu ya matukio mbalimbali ya watumishi wakiwa katika kituo cha Mtera

Sehemu ya watumishi na viongozi wakiwa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Iringa ikiwa sehemu ya ziara hiyo.

Kaimu Meneja wa Kituo cha kupoza na kusambaza umeme cha Mtera Mhandisi William Modesti akiwapa elimu na kutoa historia ya kituo hicho na maendeleo yake kwa watumishi wa Mahakama Mbeya waliotembelea katika kituo hicho.

Mtendaji wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya, Bw. Festo Chonya akitoa utambulisho na kuzungumza machache katika ziara hiyo wakiwa Mtera.

Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya Mhe. Fahamu Mtulya (kushoto), akipewa Zawadi ya jiko la umeme la kupikia “Electrical pressure cooker” wakati walipotembelea katika kituo cha kupooza na kusambaza umeme cha Mtera.

(Habari Hii Imehaririwa na Innocent Kansha - Mahakama)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni