Alhamisi, 18 Mei 2017

MAHAKAMA-KANDA YA BUKOBA NA MAPAMBANO DHIDI YA RUSHWA



Na Lydia Churi- Mahakama, Bukoba
 Jaji Mfawidhi-Mahakama kuu kanda ya Bukoba Mheshimiwa Salvatory Bongole amewataka watumishi wa Kanda yake kuwa na utu na kutokupenda vitu ili waweze kuepukana na tamaa itakayowafanya waingie kwenye vitendo vya rushwa.

Akizungumza jana alipokuwa kwenye Mahakama ya Wilaya ya Karagwe mkoani Kagera, Jaji Bongole alisema Kanda yake inaendelea na utekelezaji wa Mpango Mkakati wa miaka mitano wa Mahakama ya Tanzania kwa kuhakikisha vitendo vya rushwa vinabaki kuwa historia katika kanda ya Bukoba ili wananchi wapate haki na kwa wakati.

“Rushwa inaweza kuwepo kwa baadhi lakini si tatizo kubwa kwa Kanda ya Bukoba ila wakati mwingine inaweza kuwa ni mitazamo ya watu kuwa Mahakimu na watumishi wengine wa Mahakama wanakula rushwa”, alisema Jaji Bongole.

Jaji Mfawidhi huyo alisema mara kwa mara amekuwa akikutana na Mahakimu pamoja na watumishi wengine wa Mahakama na kuwakumbusha kufuata maadili ya kazi zao kwa kutojishirikisha na vitendo vya rushwa.

Ametoa wito kwa watumishi wote wa Mahakama ya Bukoba kuridhika na wanachopata na kuacha tamaa kwa kuwa ndizo zinazosababisha rushwa. “Ukiwa na utu hutakula rushwa, rushwa inaletwa na tamaa ya vitu”, alisisitiza.

Wakati huo huo, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Karagwe na Kyerwa Mheshimiwa Magolyo Faustine Paul alisema Mahakama zake zinajitahidi kuwashughulikia wananchi  wanapofika Mahakamani ili kuendelea kujenga imani yao kwa chombo hiki muhimu.

Akizungumzia mabango na matangazo yaliyosambazwa na Mahakama ya Tanzania ya kupambana na vitendo vya rushwa, Hakimu huyo Mkazi alisema yamesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza idadi ya malalamiko yaliyokuwa yakiletwa na wananchi kwenye dawati la malalamiko.

Alisema hivi sasa idadi ya malalamiko imepungua kutoka 5 hadi 6 yaliyokuwa yakiletwa kwa mwezi kabla ya kusambazwa kwa mabango, na mpaka kufikia malalamiko 2 hadi 3 kwa mwezi baada ya kusambazwa kwa mabango hayo.

Katika mwendelezo wa mapambano dhidi ya Rushwa, Mahakama ya Tanzania kupitia Mradi wa Kupambana na Rushwa ndani ya Mahakama (STACA) ilisambaza vifaa mbalimbali kwa lengo la kupambana na rushwa yakiwemo mabango yenye jumbe mbalimbali zenye kukemea vitendo vya rushwa na vitendo vinavyohusiana na ukiukwaji wa maadili, simu za mkononi kwa ajili ya kupokea malalamiko mbalimbali, Vifaa vya kufanyia kazi kama Kompyuta, Vinakilishi (Photocopy machines) n.k

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni