Ijumaa, 25 Agosti 2017

MAHAKAMA KUANZISHA KITUO CHA MAFUNZO DAR ES SALAAM

Na Mohamed Ali-Mahakama
Mahakama ya Tanzania inakusudia kuanzisha kituo cha Mafunzo kwa ajili ya watumishi wake pamoja na wadau ili kuwaongezea ujuzi utakaosaidia kuboresha huduma zinazotolewa na Mahakama.

Kituo hicho kinachojengwa katika eneo la Mahakama ya Kisutu jijini Dar es salaam kitawaunganisha watumishi wa Mahakama na wadau katika mafunzo kwa njia ya video (video conferencing).
Akizungumzia Kituo hicho, Kaimu Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof Ibrahim Hamis Juma alisema ujenzi wa kituo hicho ni sehemu ya Maboresho ya huduma za Mahakama ambacho pia wadau wa Mahakama watakuwa ni sehemu ya mafunzo yatakayokuwa yakitolewa.

Alisema badala ya Majaji, Mahakimu, watumishi na wadau wa Mahakama kwenda kupata baadhi ya mafunzo kwenye chuo cha Uongozi wa Mahakama- Lushoto (IJA), baadhi ya mafunzo watakuwa wakiyapata katika kituo hicho.
Naye Mratibu wa Mpango Mkakati wa Mahakama pamoja na maboresho ya Huduma za Mahakama Mhe. Zahara Maruma alisema ujenzi wa kituo hicho ni utekelezaji wa nguzo ya tatu ya mpango Mkakati wa miaka mitano wa Mahakama ya Tanzania ambapo kupitia nguzo ya pili ya Mpango huo, Majaji na Mahakimu hupatiwa mafunzo mbalimbali ili kurahisisha upatikanaji wa haki kwa wakati.

Akizungumzia nguzo ya tatu ya Mpango huo, Mhe. Maruma alisema nguzo hiyo inahusiana na urejeshaji wa imani ya wananchi kwa Mahakama na ushirikishwaji wa wadau katika shughuli za Mahakama ambapo kupitia kituo hicho wadau wa Mahakama watahusishwa kwenye Mafunzo mbalimbali ili kurahisisha suala la upatikanaji wa Haki.
Kuhusu suala la matumizi ya Teknolojia ndani ya Mahakama, Mratibu huyo alisema hivi sasa Mahakama inao mpango wa kujenga vituo vya aina hiyo kwenye maeneo mbalimbali nchini kwa lengo la kuunganisha Mahakama zote nchini kwa njia ya video (video conferencing).

Ujenzi wa kituo cha Mafunzo cha Mahakama ulioanza hivi karibuni kwa ushirikiano kati ya Mahakama ya Tanzania na Benki ya Dunia unatarajiwa kugharimu kiasi cha shilingi za kitanzania milioni 78. Aidha, Jengo la kituo hicho cha mafunzo linajengwa kwa kutumia teknolojia ya gharama nafuu iitwayo Moladi na linatarajiwa kukamilika ndani ya wiki nane.
  Kaimu Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati) akiwasili katika Mahakama ya Kisutu kukagua ujenzi wa kituo cha Mafunzo cha Mahakama ya Tanzania kinachojengwa jijini Dar es salaam. Kulia ni Mwakilishi wa Benki ya Dunia Nchini, Bella Bird na kushoto ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanznaia Mhe. Ferdinand Wambali. 
 Kaimu Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe Prof. Ibrahim Hamis Juma akisaini kitabu baada ya kuwasili katika Mahakama ya Kisutu kukagua ujenzi wa kituo cha Mafunzo cha Mahakama ya Tanzania kinachojengwa jijini Dar es salaam. Kulia ni Mwakilishi wa Benki ya Dunia Nchini, Bella Bird. 
 Kaimu Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe Prof. Ibrahim Hamis Juma akizungumza na Mwakilishi wa Benki ya Dunia Nchini, Bella Bird. Wa kwanza Kushoto ni Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Katarina Revokati akifuatiwa na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Hussein Katanga na wa mwisho ni Mtaalamu kutoka Benki ya Dunia, Waleed Malik 
  Kaimu Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe Prof. Ibrahim Hamis Juma akiwa na Mwakilishi wa Benki ya Dunia Nchini, Bella Bird.
  Mhandisi wa Mahakama ya Tanzania, Khamadu Kitunzi akielezea kuhusu Teknolojia inayotumika kujenga jengo la Kituo cha Mafunzo.
 Mtaalamu kutoka Benki ya Dunia, Waleed Malik akizungumza jambo na Wahandisi wanaosimamia ujenzi wa kituo cha Mahakama
  Picha ya pamoja
 Mwakilishi wa Benki ya Dunia nchini, Bella Bird, Mtaalamu kutoka Benki ya Dunia, Waleed Malik na Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. katarina Revokati wakizungumza jambo wakati walipotembelea ujenzi wa kituo cha mafunzo cha Mahakama.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Hussein Kattanmga akimwelezea jambo Mtaalamu kutoka Benki ya Dunia, Waleed Malik walipotembelea ujenzi wa kituo cha Mafunzo cha Mahakama.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni