Jumatano, 23 Agosti 2017

JAJI MKUU MSTAAFU AAGWA NA CHUO CHA UONGOZI WA MAHAKAMA LUSHOTO


Na Ibrahim Mdachi, (IJA) Lushoto
Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto IJA, kiliandaa hafla fupi ya kumuaga Jaji Mkuu Mstaafu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Jaji Mohamed Chande Othman. 

Hafla hiyo iliyofanyika Agosti 19, 2017 ilihudhuriwa na wageni mbalimbali wakiongozwa na Mgeni rasmi Kaimu Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Jaji. Prof. Ibrahim Hamis Juma. 

Sherehe hiyo ilitanguliwa na hafla fupi ya chakula cha jioni kilichoandaliwa na Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo Jaji Mstaafu, Mhe. John A Mrosso kwa hisani ya Mhe. Kaimu Jaji Mkuu ambapo alipata fursa ya kukutana na wajumbe wa Baraza, wajumbe wa menejimenti pamoja na baadhi ya waalikwa katika chakula hicho.

Akitoa hotuba yake katika hafla hiyo, Kaimu Jaji Mkuu, Mhe. Prof. Ibrahim Juma alishukuru Baraza la Uongozi wa Chuo pamoja na Menejimenti ya Chuo kwa heshima kubwa aliyopewa kwa kualikwa kuwa mgeni rasmi ambapo ilikuwa ni fursa ya kukitembelea Chuo hicho kwa mara ya kwanza akiwa kama Kaimu Jaji Mkuu. 

“Naomba kuwashukuru sana kwa kunialika kuwa mgeni rasmi katika hafla hii ambayo imenipa fursa ya kukitembelea Chuo hiki kwa mara ya kwanza kama Kaimu Jaji Mkuu. Kwa hakika hii ni heshima kubwa mliyonipa ambayo ni fursa nyingine kwangu ya kukutana na wajumbe wa Baraza la Chuo, waheshimiwa majaji na viongozi wa Chuo chetu. Pia, nawashukuru kwa mapokezi mazuri niliyoyapata tangu nilipowasili hapa jana.” Alisema Mhe. Kaimu Jaji Mkuu.

Mgeni rasmi aligusia michango mbalimbali ya Mhe. Jaji Mkuu Mstaafu katika maendeleo ya Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto na kunukuu miongoni mwa maneno aliyowahi kuyasema huko nyuma.
“Kuimarisha Chuo Cha Uongozi wa Mahakama Lushoto ili kiwe chenye hadhi na kitoe mafunzo kwa maofisa wa Mahakama na wadau wengine.” 

Aidha, Mhe. Kaimu Jaji Mkuu aliahidi kuwa Mahakama itaendelea kuchota busara na uzoefu wa Mhe. Jaji Mkuu Mstaafu katika namna bora ya kuendesha Chuo hiki ili kiweze kuwa ni kitovu halisi cha mafunzo elekezi na mafunzo endelevu ya kimahakama yaani ‘Centre of Excellence in Judicial Training in Africa and beyond.’

Pamoja na hayo mgeni rasmi hakusita kusisitiza juu ya ushirikiano  wa moja kwa moja kati ya Baraza la Uongozi wa Chuo na Viongozi wakuu wa Mahakama ya Tanzania ili kuhakikisha kwamba vipengele vyote vilivyomo kwenye Mpango wa Maendeleo wa Mahakama ya Tanzania vinavyohusiana na Chuo ikiwemo uboreshaji wa miundombinu pamoja na kuwajengea uwezo watumishi vinatekelezwa.

Akitoa nasaha zake kwa Baraza la Uongozi wa Chuo, Menejimenti ya Chuo na watumishi waliohudhuria katika hafla hiyo, Jaji Mkuu Mstaafu, Mhe. Mohamed Chande Othman  alisema kuwa Chuo kimetoa mchango mkubwa sana katika Elimu ya Sheria kwa Mahakimu na Makarani wa Mahakama. Hata hivyo alisisitiza kuwa Chuo kiendelee kupeperusha bendera ya Mahakama. 

Mara baada ya kutoa nasaha zake, Mhe. Jaji Mkuu Mstaafu pamoja na mke wake walipewa zawadi mbalimbali kutoka Baraza la Uongozi wa Chuo  na watumishi wa Mahakama Kuu Kanda ya Moshi na Tanga ambazo ziliwasilishwa kwa niaba yao na Majaji Wafawidhi wa kanda hizo. 

Mheshimiwa Mgeni rasmi pamoja na Mhe. Jaji Mkuu Mstaafu walipata fursa ya kupanda miti ya kumbukumbu kama ilivyo desturi ya Chuo cha Uongozi wa Mahakama. 

Wageni wengine waliohudhuria hafla hiyo ni Mhe. Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu, Kanda ya Moshi (Mhe. Jaji. Ashiel Sumari), Mhe. Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu, Kanda ya Tanga (Mhe. Jaji. Iman Aboud), Majaji wa Mahakama Kuu, Kanda ya Tanga, (Mhe. Jaji. Amour Khamis na Mhe. Jaji. Dkt. Benhajj Masoud).

Wengine ni Jaji Mstaafu na Mkuu wa Chuo wa kwanza (Mhe. Emillian Mushi), Mtendaji Mkuu wa Mahakama (Hussein Kattanga), Msajili Mkuu wa Mahakama (Bi Katarina Revokati), Naibu Msajili Mahakama Kuu Kanda ya Tanga, Wajumbe wa Baraza la Chuo, Mhe. Hakimu Mkazi Mfawidhi (W) Lushoto, Mhe. Hakimu Mkazi Mfawidhi  (W) Korogwe, Katibu Tawala Mahakama (W) Korogwe, Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Halmashauri (W) Lushoto, Mkuu wa Polisi Wilaya ya Lushoto, Wajumbe wa Manejimenti, Wawakilishi wa watumishi wa Chuo  na Mwenyekiti wa Kitongoji cha Dochi.
 Jaji Mkuu Mstaafu, Mhe. Mohamed Chande Othman, akitoa neno katika hafla ya kuagwa kwake na Chuo cha Uongozi wa Mahakama-Lushoto (J) kufuatia kustaafu rasmi Januari, 2017 , hafla hiyo ilifanyika Agosti 19, chuoni hapo. katika nasaha zake, Mhe. Chande alishukuru kwa ushirikiano aliopewa katika kipindi cha uongozi wake na kuahidi kutoa ushirikiano zaidi.
Kaimu Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Juma, akitoa neno katika hafla ya kuagwa kwa Jaji Mstaafu Mhe. Mohamed Chande Othman kufuatia kustaafu kwake, katika nasaha zake Mhe. Prof Juma amemshukuru Mhe. Chande kwa mchango wake aliutoa katika Chuo hicho na Mahakama kwa ujumla katika kipindi chake cha kutumikia nafasi hiyo.
Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo Jaji Mstaafu, Mhe. John A Mrosso  akitoa neno katika hafla hiyo.
Badhi ya Watumishi wa Chuo na Wageni waalikwa wakiwa katika hafla hiyo.
Jaji Mstaafu na Mkuu wa Chuo wa kwanza, Mhe. Emillian Mushi (wa kwanza kulia) pamoja na watumishi wengine wa Chuo wakiwa katika hafla hiyo.
Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo Jaji Mstaafu, Mhe. John A Mrosso (wa kwanza kulia) akikabidhi zawadi kwa Jaji Mkuu Mstaafu, Mhe. Mohamed Chande Othman, anayeshuhudia katikati ni Kaimu Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Khamis Juma.
Mke wa Jaji Mkuu Mstaafu, Bi. Saada Chande akikabidhiwa zawadi katika hafla hiyo ya kuagwa kwa Jaji Mstaafu, Mhe. Mohamed Chande Othman.
Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu-Kanda ya Tanga, Mhe. Imani Aboud akitoa neno katika hafla ya kuagwa kwa Jaji Mstaafu iliyoandaliwa na Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA)-Lushoto.
Mhe. Aboud akimkabidhi zawadi, Mhe. Jaji Mkuu Mstaafu.
Katika pi  cha ya pamoja na Jaji Mkuu Mstaafu, (wa pili kushoto), katikati ni Kaimu Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Juma, wa pili kulia ni Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo Jaji Mstaafu, Mhe. John A Mrosso, wa kwanza kulia ni Mhe. Aishieli Sumari, Jaji Mfawidhi-Mahakama Kuu Kanda ya Moshi, na wa kwanza kushoto ni mke wa Jaji Mkuu Mstaafu, Mhe. Saada Chande, waliosimama nyuma wa kwanza kushoto ni Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA), Mhe.Dkt. Paul Kihwelo, wa pili kushoto ni Mtendaji Mkuu, Mahakama ya Tanzania, Mhe. Hussein Kattanga, wa tatu kushoto ni Msajili Mkuu-Mahakama ya Tanzania, Mhe. Katarina Revocatti na Watumishi wa Chuo hicho.
Jaji Mkuu Mstaafu akipanda mti wa kumbukumbu mara baada ya hafla kuagwa kwake baada ya kustaafu kwa mujibu wa sheria.
Kaimu Jaji Mkuu nae akipanda mti wa Kumbukumbu katika chuo hicho mara baada ya kuhitimisha hafla ya kumuaga Jaji Mkuu Mstaafu iliyofanyika wikiendi iliyopita. (Picha na Na Ibrahim Mdachi-IJA Lushoto)


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni